2014-03-18 15:33:41

Historia fupi ya maisha ya Marehemu Askofu Fortunatus Lukanima


Marehemu Askofu mstaafu Fortunatus Lukanima aliyefariki dunia hivi karibuni kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza, Tanzania, amezikwa tarehe 15 Machi 2014 kwenye Kanisa la Kagunguli, Ukerewe, Jimbo Katoliki la Bunda katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Mwanza. Ibada ya Mazishi iliongozwa na Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda. Kanisa la Kagunguli ni Kanisa Mama Kisiwani Ukerewe na lina utajiri mkubwa wa hazina ya historia ya Ukristo Kisiwani hapo.


MAISHA YA AWALI:

Askofu Fortunatus Lukanima alizaliwa tarehe 08\12\1940 katika kijiji cha Ilondo, Ukerewe, parokia ya Kagunguli, akiwa ni motto wa tatu kati ya watoto sita, wavulana wane (4) na wasichana wawili (2) kwa familia ya Baba Yohane Musyeto na Mama Sabina Mugala.

Alibatizwa tarehe 02\01\1952 na kupokea Komunio ya Kwanza siku hiyo katika Parokia ya Kagunguli.

ELIMU:
Askofu Lukanima alipata elimu ya msingi (darasa la Kwanza mpaka la Nne) Kagunguli shule ya Msingi mwaka 1947 hadi 1954. Baada ya kuhitimu elimu hiyo alijiunga na Seminari ndogo ya Mtakatifu Maria Nyegezi kwa ajili ya elimu ya kati na ya Sekondari (darasa la tano hadi la kumi na mbili) mwaka 1952 hadi 1962.

Mwaka 1963, alijiunga na Seminari ya kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala,Tabora kwa ajili ya masomo ya Falsafa na Taalimungu hadi mwaka 1968 alipohitimu. Alipewa daraja la Upadre tarehe 08\12\1968 katika Parokia ya Kagunguli na Askofu Renatus Butibubage.

UTUME:
Baada ya Upadrisho wake, amefanya kazi katika parokia ya Itira muda wa miezi sita (6) akiwa paroko msaidizi. Baadaye alifundisha katika Seminari ndogo ya Nyegezi kama mwalimu, Gombera msaidizi na mlezi wa Chama cha Vijana Wakristo (YCS), Jimbo la Mwanza.

ELIMU ZAIDI:
Mwaka 1972 alikwenda Marekani kusomea Uhusiano wa Kimataifa na Utawala katika Chuo kikuu cha Detroit, akapata shahada ya “Master of Arts”. Akiwa masomoni, alifanya pia kazi ya uchungaji kama Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Bernard, jijini Detroit.

Wakati huohuo, alifundisha Biblia katika Chuo cha Ushemasi wa kudumu, Jimbo kuu la Detroit mwaka 1973 hadi 1975. Mwishoni mwa mwaka 1975 alikwenda Chuo Kikuu cha Michigan kusomea Siasa na elimu ya Utafiti. Baadaye aliongeza elimu ya Siasa ya Uchumi akapata Shahada ya Ph.D. Wakati huohuo alihudumia Vyuo na hospitali mbalimbali.

Baada ya masomo yake Marekani, alirudi Jimboni Mwanza akapewa kazi ya kuwa ni Paroko msaidizi katikaPparokia ya Itira, Ukerewe mwaka 1982.

· Mwaka 1984 mwezi Machi alipewa kazi ya Ukatibu katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu, Afrika Mashariki na Kati, AMECEA.

· Mwaka 1984 Septemba alichaguliwa na Chama cha Ulimwengu cha Mawasiliano ya Kikristo (WACC) kama mwakilishi katika Bodi ya Utawala (ACIS) iliyokuwa na makao makuu Nairobi.

· Mwaka 1984 Oktoba, Baraza la Maaskofu lilimteua kama mwakilishi katika Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo cha Fasihi (ALC) kilichopo Kitwe, Zambia, kwa kipindi cha miezi sita (6).

· Mwaka 1986 Aprili, Maaskofu wa AMECEA walimchagua awe Katibu Mkuu.

· Mwaka 1987 Januari, Pd. Lukanima alichaguliwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Menejimenti ya Huduma ya Mawasiliano ya Kanisa (ACIS).

· Tarehe 15\04\1989, Pd. Lukanima alichaguliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Arusha. Amefanya kazi katika jimbo hilo muda wa miaka tisa (9) kisha akajiuzulu na karudi Jimboni Mwanza. Akiwa Jimboni, makao yake yalikuwa Murutunguru, Ukerewe.

UGONJWA:
Askofu Lukanima alijisikia vibaya mwilini kwa miezi kadhaa bila kujua kinachomsibu. Alipokwenda kupimwa ndipo Madaktari walipogundua kuwa alikuwa na saratani ya ini. Walijitahidi kumtibu, lakini ugonjwa ulizidi matibabu. Hatimaye, tarehe 12\03\2014 alfajiri, Askofu Lukanima aliaga dunia.

SHUKRANI:
Tunawashukuru nyote mliomsaidia na kumhudumia: Madaktari na Wauguzi katika hospitali ya Rufaa Bugando, ndugu, jamaa na marafiki.



RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA
NA MWANGA WA MILELE UMWANGAZIE.

APUMZIKE KWA AMANI - AMINA.










All the contents on this site are copyrighted ©.