2014-03-18 09:44:44

Changamoto zinazoendelea kufanyiwa kazi na Papa Francisko!


Tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa mwaka mmoja uliopita amejielekeza zaidi katika kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii; haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu kati ya watu wa mataifa, kwa kuguswa na mahangaiko ya watu wanaowazunguka.

Papa ameendelea kuombea amani na upatanisho kati ya mataifa na kwamba, majadiliano ya kina yawe ni msingi wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazoendelea kuukabili ulimwengu. Mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia huko Sudan ya Kusini bila kusahau sehemu ambazo kwa sasa zinakabiliana na vita pamoja na kinzani za kijamii ni kati ya mambo ambayo yanamgusa Baba Mtakatifu kwa sasa.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya, katika hafla ya kumbu kumbu ya Mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Upendo na mshikamano; haki, amani, upatanisho na msamaha wa kweli, ni changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Kanisa linapaswa kuendelea kujikita katika ukweli, haki, amani na uhuru kamili katika utekelezaji wa dhamana na utume wake sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya mafao ya wengi na ustawi wa Jamii husika. Baba Mtakatifu Francisko alichaguliwa hapo tarehe 13 Machi 2013 na kuanza rasmi utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro hapo tarehe 19 Machi 2013 sanjari na Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, Mchumba wa Bikira Maria na Mlinzi wa Kanisa.

Wakati huo huo, Serikali ya Kenya imelipongeza Kanisa kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwaletea wananchi wa Kenya maendeleo endelevu yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu, hasa katika maeneo ya vijijini. Kanisa Katoliki nchini Kenya linamiliki na kuendesha shule za msingi na sekondari 8, 000. Kanisa lina vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu 5. Kanisa lina hospitali, vituo vya afya na zahanati zaidi ya 500 pamoja na vituo 5 kwa ajili ya watoto yatima.

Maendeleo ya sekta ya elimu nchini Kenya ni mchango mkubwa uliotolewa na unaoendelea kutolewa na Kanisa, sanjari na kuhakikisha kwamba, huduma hii inazingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa. Serikali ya Kenya inasema kwamba, itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kulinda na kutetea: haki na amani; maendeleo na ustawi wa wananchi wote wa Kenya







All the contents on this site are copyrighted ©.