Usawa wa kijinsia katika Bunge Maalum la Katiba Tanzania wapongezwa
Mtandao wa Wanawake na Katiba wenye mashirika zaidi ya 50 yanayotetea haki za wanawake
katika Katiba mpya, umepokea kwa furaha mchakato na matokeo ya uchaguzi wa kuwapata
viongozi wa Bunge Maalum la Katiba (Mwenyekiti na Makamu wake) ambao umezingatia usawa
wa jinsia.
Pamoja na kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya
Mwaka 2012 haikuanisha kuwa uchaguzi wa uongozi wa Bunge hili uzingatie usawa wa jinsia,
tumetambua busara na hekima za wajumbe za kuonyesha nia ya kujenga msingi wa usawa
wa jinsia katika uongozi na vyombo vya maamuzi nchini. Kwetu sisi, hili si suala la
uwepo wa mwanamume na mwanamke katika uenyeketi wa Bunge Maalumu tu, bali pia ni
ukomavu wa kipekee wa wajumbe katika kuuona ukweli kuwa suala la kuimarisha sauti
za wanawake na wanaume ni nyeti sana, haswa wakati wa ujenzi wa maridhiano muhimu
kikatiba.
Tunawapongeza waliochaguliwa ambao ni Mhe. Samweli Sitta (Mwenyekiti)
na Mhe. Samia Hassan Suluhu (Makamu Mwenyekiti) kwa kuaminiwa katika nyadhifa hizo
muhimu. Mtandao wa Wanawake na Katiba unatambua uwezo wao katika utendaji na una
matumaini makubwa kuwa pamoja na mengine mengi watakayoyasimamia, watatoa uongozi
ulio imara na wenye weledi wakati wakiongoza Bunge hili katika kujadili na kupitisha
misingi muhimu itakoyopelekea katika ujenzi wa usawa wa kijinsia nchini.
Tunategemea
kuona usawa wa jinsia ndani ya Katiba mpya, ambao sio ule tu wa kuongeza ushiriki
wa wanawake katika ngazi mbalimbali, lakini pia usawa ulio na nia ya kujenga misingi
ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi walio wengi na haswa wanawake nchini.
Kwa
mtazamo huu, tunatarajia kuwa busara za Wenyeviti hawa na washauri wao zitatumika
pia kuzingatia usawa wa kijinsia katika Kamati zitakozoundwa pamoja na kuwa kuzingatia
ustadi na uzoefu wa wanakamati unahitajika. Nia kubwa ikiwa kuona wanawake kwa wanaume
watatoa sauti zao kuhakikisha na kulinda, pamoja na mengine, uzingatiwaji wa usawa
wa jjinsia katika vifungu vyote vya Katiba mpya.
Vilivile, Mtandao wa Wanawake
na Katiba, unawapongeza wajumbe wote wanawake kwa umoja wao, mshikamano na ushirikiano
imara, ambao umeleta mafanikio makubwa katika michakato inayoendelea huko Dodoma kwenye
Bunge Maalumu. Huu ni mwanzo wenye kuonyesha mifano mizuri, na ambao tunapenda kuuona
ukiendelezwa na kusimamiwa imara wakati wote Bunge Maalumu litakapokuwa likifanya
kazi yake ya kuchambua na kupitisha vifungu mbalimbali vya Katiba,