Serikali ya Tanzania inaadhimisha Juma la Maji kila mwaka kuanzia tarehe 16 hadi tarehe
22 Machi. Lengo ni kuwahamasisha wananchi kutambua umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya
maji pamoja na kubainisha mikakati inayopewa kipaumbele ili kukabiliana na changamoto
za huduma ya maji nchini Tanzania. Ni fursa kwa wadau mbali mbali wa maji kuweza kubadilishana
uzoefu, mang’amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo. Maadhimisho ya Maji Kitaifa
kwa Mwaka 2014 yanafanyika Mkoani Dodoma kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Maji na Nishati”
Serikali
ya Tanzania imesema ipo changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira katika vyanzo
vya maji nchini hali inayosababisha upatikanaji wa maji kuwa wa taabu. Kauli hiyo
ilitolewa hivi karibuni na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe wakati akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya maji kitaifa yanayotarajiwa kufanyika
Mkoani hapa.
Alisema mbali na mabadiliko ya tabia nchi, uharibufu huo unasababishwa na
ongezeko la watu pamoja na shughuli za kibinadamu wanazozifanya katika vyanzo
hivyo vya maji "Ukitaka kujua tatizo la upungufu wa maji ni kuangalia miaka 15 liyopita
ambapo kila mtanzania alikuwa akitumia meta za ujazo 2500kwa mwaka lakini kwa sasa
imepungua na itakapofika mwaka 2020 kila mtanzania atatumia meta za ujazo 1700 tu,"
alisema.
Profesa Maghembe alisema hali hiyo inaonyesha jinsi ambavyo upatikanaji
wa maji unavyozidi kupungua mwaka hadi mwaka alibainisha kwamba changamoto ni kubwa
na zinahitaji uelewa wa wananchi katika shughuli zao za kimaendeleo na kuchukua hatua
ili kuhakikisha maji yanaendelea kuwepo. Kuhusu miundombinu alisema kumekuwepo na
tatizo la watu kuifuata miundombinu ya maji kwamba sheria za adhabu zilizopo ni ndogo
hivyo wanajipanga kupeleka mabadiliko katika sheria hiyo ili kuwa na kifungo kukomesha
tabia hiyo.
Akizungumzia kuhusu miradi ya maji, Profesa Maghembe alisema zaidi
ya miradi 1600 ya maji inatekelezwa vijijini katika wilaya zote nchini katika
kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14. "katika miradi hiyo mpaka kufikia mwishoni mwa
mwezi Februari 2014, zaidi ya watu milioni 17 wanapata majisafi na salama "Ifikapo
mwishoni mwa mwaka 2015 tunatarajia idadi ya upatikanaji wa maji iongezeke kutoka
watu asilimia 51.09 kufikia asilimia 74 nchini kote kwa idadi ya wanaoishi vijijini
ambao ni asilimia 77," alisema Waziri huyo.
Aidha, alisema pia kwamba Serikali
inapania kufikisha katika miji mikuu yote huduma ya majisafi kwa asilimia 85 katika
kipindi cha Mwaka 2014. Upande wa Mkoa wa Dodoma, alisema miradi 69 katika vijiji
64 itakelezwa na itakapokamilika itakuwa imeinua kiwango cha upatikanaji wa maji.