2014-03-15 10:16:26

Professa Giuseppe Profiti kuendelea kuwa Rais wa Hospitali ya Bambino Gesu, Roma


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa madaraka aliyokabidhiwa na Baba Mtakatifu Francisko amemteua Professa Giuseppe Profiti kuendelea kuwa ni Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuongozwa na Vatican kwa kipindi cha miaka mitatu yaani kuanzia Mwaka 2014 hadi Mwaka 2016. Kardinali Parolin ameteuwa pia Baraza Jipya la Hospitali litakalofanya kazi zake kwa kipindi cha miaka mitatu pia.

Professa Giuseppe Profiti mwenye umri wa miaka 52, tangu Mwaka 2008 amekuwa ni Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù. Katika kipindi cha uongozi wake, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika utoaji wa tiba kwa watoto wagonjwa, huduma za utafiri kiasi cha kuifanya Hospitali hii kuwa ni Kituo kikuu cha utafiti wa magonjwa ya watoto Barani Ulaya. Hospitali imepanua huduma zake kwa kuongeza matawi mengine nje ya Mji wa Roma.

Hospitali ya Bambino Gesù imeendelea kuwa ni kielelezo cha huduma ya upendo na mshikamano kwa watoto wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kwa kukosa huduma bora za tiba kama vile: Cambodia, Yordan, Lebanon na Tanzania ambako imesaidia kujenga Kliniki ya Upasuaji kwa watoto wenye ugonjwa wa moyo, kwenye Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Sindiga, Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.