Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya Kipapa, katika mahubiri ya Kipindi
cha Kwaresima yaliyofanyika kwenye Kikanisa cha Redemptoris Mater mjini Vatican Ijumaa
tarehe 14 Machi 2014 amekazia mambo makuu yafuatayo: umuhimu wa jangwa katika maisha
ya kiroho; aina mpya za kufunga na kusali zinazokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu;
majaribu katika maisha na umuhimu wa waamini kumfuasa Yesu katika Jangwa la maisha
yao, ili kufunga, kusali na kutafakari kwa kina Neno la Mungu.
Padre Cantalamessa
anasema, mwaliko wa kumfuasa Yesu Jangwani ni kwa ajili ya Wakristo wote ingawa kuna
baadhi ya Wamonaki walioguswa kwa namna ya pekee wakaacha yote na kujitenga na malimwengu
kwa ajili ya kusali na kulitafakari Neno la Mungu. Kila mwamini anapaswa kuchagua
Jangwa la maisha yake ya kiroho, ili kuweza kuingia katika undani wa maisha yake,
ili hatimaye, aweze kugundua ile sura na mfano wa Mungu iliyo ndani mwake, kwa kukazia
mambo msingi katika maisha.
Hii ni changamoto ya kujenga na kukuza amani na
utulivu wa ndani ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu. Kwenda Jangwani
kuna maanisha kutenga muda maalum kwa ajili ya kusali na kulitafakari Neno la Mungu,
tayari kuanza hija mpya ya maisha ya kiroho.
Padre Cantalamessa anasema kufunga
kunakokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu kunajikita katika kwanza kabisa kuguswa na
mahangaiko ya wengine, tayari kuwashirikisha kile ambacho Mwenyezi Mungu amekukirimia
katika maisha kwa njia ya matendo ya huruma na mapendo. Ni hali ya kujinyima kwa ajili
ya wengine pamoja na kudhibiti vilema vya maisha ya binadamu, ili kuomba huruma na
upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.
Kufunga ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji
wa haki jamii kwa kuwasaidia wengine kuweza kupata maisha bora zaidi ili kuondokana
na baa la njaa, ujinga na maradhi. Ni harakati za kujenga na kudumisha misingi ya
haki, amani, upendo na mshikamano kama kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa
katika uhalisia wa maisha ya mwamini.
Padre Cantalamessa anasema, Yesu alipokuwa
Jangwani akifunga na kusali kwa siku arobaini alijaribiwa na Shetani. Uwepo wa Pepo
wachafu ni jambo ambalo linawakumba watu wengi wa nyakati hizi, kiasi cha kuwafanya
kuwa ni mateka wa imani za kishirikina ambazo kimsingi zimekuwa ni chanzo hata cha
maafa ya watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali za dunia. Wakristo wanafundishwa
kwamba, Yesu alimshinda mwovu Shetani kwa njia ya Msalaba, ili kutekeleza kazi ya
ukombozi aliyokuwa amedhaminishwa na Baba yake wa mbinguni.
Yesu alitekeleza
kazi ya ukombozi kwa njia ya utii, unyenyekevu na mateso makali, kinyume kabisa na
Shetani aliyekuwa anamtaka Yesu kuchukua njia ya mkato katika utekelezaji wa kazi
ya ukombozi. Shetani anajitokeza katika mambo ambayo yanamvuto na mashiko kwa binadamu
kama vile: fedha na utajiri wa haraka haraka; madaraka na sifa kemkem; chakula, vinywaji
pamoja na ngono! Waamini wakiendekeza mambo haya wataweza kujikuta wametumbukizwa
pabaya katika maisha yao!
Padre Cantalamessa anasema, baada ya Yesu kubatizwa
Mto Yordan alikwenda Jangwani ili kusali na kufunga kwa kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa uwepo wa Mungu katika maisha na utume wake. Hili ndilo fundisho kubwa linalotolewa
kwa Wakristo wakati huu wa Kwaresima, kwamba, kuna haja kila mara kuhakikisha kwamba,
wanajitenga na malimwengu kwa ajili ya kusali, kufunga na kutfakari Neno la Mungu,
kama njia ya kujichotea nguvu ya maisha ya kiroho, tayari kupambana na changamoto
mbali mbali zinazojitokeza katika maisha.
Jangwa ni mwaliko wa kuingia katika
undani, ili kuzungumza na Mwenyezi Mungu, katika ukweli na haki. Hata leo hii anasema
Padre Raniero Cantalamessa, Yesu bado anawasubiri wafuasi wake katika Jangwa la maisha
ya miyo yao, kamwe wasimwache pweke!