2014-03-15 12:16:45

Kanuni maadili ni jambo la msingi katika mchakato wa maendeleo ya binadamu!


Wakimbizi, maendeleo na mikakati ya kilimo mintarafu mafundisho Jamii ya Kanisa ndiyo mada inayofanyiwa kazi na Padre Gabriele Bentoglio, Katibu mwambata, Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum katika ziara yake ya kichungaji kwenye Chuo Kikuu cha St. Petersburg, kilichoko nchini Russia, kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 21 Machi 2014.

Mama Kanisa anapojikita katika mikakati ya maendeleo ya binadamu anaongozwa na kanuni msingi zifuatazo, yaani: haki na mafao ya wengi yanayojikita katika ukweli na upendo, mambo msingi katika kukuza na kudumisha mahusiano kati ya watu, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa Kichungaji, Ukweli katika Upendo.

Kuhusu mustakabli wa wakimbizi sehemu mbali mbali duniani, Kanisa linakazia kwa namna ya pekee haki ya wahamiaji kuhama kutoka sehemu moja ya dunia kwenda sehemu nyingine. Watu wana haki msingi ya kubaki katika nchi zao asilia, ikiwa kama hali inaruhusu. Haki msingi za wakimbizi na wahamiaji zinapaswa kulindwa na kuheshimiwa na wote. Serikali zina haki pia ya kuratibu mchakato wa wahamiaji katika nchi husika kwa kuzingatia haki msingi za binadamu na mafao ya taifa husika.

Padre Bentoglio anasema kwamba, leo hii kuna mamillioni ya watu ambao wana kiu ya kuona watu wanashirikishwa katika mchakato wa maendeleo endelevu na haki inatendeka. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wahamiaji millioni 232 wanaofanya kazi sehemu mbali mbali duniani. Watu zaidi ya millioni 900 wanaishi na kutekeleza majukumu yao vijijini.

Yote haya ni makundi ambayo Mama Kanisa anayapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Katika nyakati hizi ambamo Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuonja athari za mtikisiko wa uchumi kimataifa, kuna haja ya kujenga na kudumisha kanuni na sera bora za kilimo, ili kuinua kiwango cha uzalishaji katika sekta ya kilimo ili kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula pamoja na Familia nyingi vijijini kuinua kipato chake.

Padre Gabriele Bentoglio anasema kwamba, mada ya utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya kazi ya uumbaji ina mguso wa pekee sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, aliyechagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa sababu alikuwa ni Mtakatifu aliyethamini sana utunzaji bora wa mazingira. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wana wajibu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao na maendeleo ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Dunia na rasilimali zake itumiwe kwa uwajibikaji mkubwa, ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Lakini inasikitisha kuona kwamba, mwanadamu amekuwa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira na athari zake zinaonekana sehemu mbali mbali za dunia. Ardhi itumiwe kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu, kwa kuzingatia sheria na kanuni bora za kilimo na kwa ajili ya mafao na ustawi wa Jumuiya ya Kimataifa.

Kanuni maadili kiwe ni kigezo kikubwa katika sera na mikakati ya maendelo ya mwanadamu, vinginevyo watu watajikuta wanatumbukia katika maafa makubwa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira. Watu wawajibike kikamilifu na kwamba, kila mtu anapaswa kufaidika na mrasilimali ya dunia, kama ambavyo Mama Kanisa anakazia katika Mafundisho Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.