Cor Unum, kielelezo cha mshikamano wa upendo kwa waathirika wa maafa duniani
Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum ndicho kitengo
maalum cha misaada inayotolewa na Kanisa Katoliki kwa watu kutoka sehemu mbali mbali
duniani. Kwa maneno mengine, Cor Unum ndio mkono wa upendo wa Baba Mtakatifu kwa watu
wanaokabiliana na maafa sehemu mbali mbali za dunia.
Baraza hili
lilianzishwa na Papa Paulo VI kunako tarehe 15 Julai 1971 na tangu wakati huo, Cor
Unum limekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia watu kiroho na kimwili kama kielelezo
cha mshikamano wa huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Hivi ndivyo anavyobainisha Askofu mkuu Giampietro Dal Tosso, Katibu mkuu wa
Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum katika mahojiano
maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano, linalomilikiwa na Vatican. Cor Unum ni kielelezo
makini cha udugu na mshikamano wa mapendo unaooneshwa na Mama Kanisa kwa watu wanaoteseka:
kiroho na kimwili; watu wanaokabiliana na maafa asilia, vita na majanga mengine ya
maisha.
Kwa Mwaka 2013, Kanisa limeonesha mshikamano wa huruma na mapendo
kwa wananchi wa Ufilippini waliokumbwa na tufani kubwa iliyopelekea maelfu ya watu
kupoteza maisha na mali zao. Kanisa bado linaendelea kuchangia kwa hali na mali nchini
Syria ambako kuna maelfu ya watu wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha yao
na wengine wanalazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali
zao. Idadi inaonesha kwamba, kuna wakimbizi zaidi ya millioni sita kutoka Syria wanaohitaji
msaada wa hali na mali.
Licha ya Baba Mtakatifu Francisko kuwasindikiza wananchi
wa Syria kwa njia ya sala na kufunga, kama alivyofanya hapo tarehe 7 Septemba, 2013,
bado Mashirika mbali mbali ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanashiriki kusaidia kutoa
huduma kwa wananchi wa Syria na kwa nchi jirani.
Kuna zaidi ya Mashirika 25
yaliyoko chini ya mwamvuli wa Kanisa Katoliki yanayotoa misaada ya kiutu huko Mashariki
ya Kati. Mashirika haya yanasaidiana kutoa huduma makini kwa wananchi wa Syria bila
ya ubaguzi wala upendeleo wa kisiasa, kidini au mahali anapotoka mtu! Wote wanapata
huduma sawa sawa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Mashirika ya Misaada
ya Kanisa Katoliki yanaendelea pia kutoa huduma ya kiutu kwa wakimbizi na wahamiaji
wanaoishi nchini Lebanon. Cor Unum ina mpango mkakati wa kuanzisha hospitali kwa ajili
ya watoto wadogo nchini Lebanon, itakayokuwa inashirikiana na Hospitali ya Bambino
Gesù inayomilikiwa na Vatican, ili kutoa huduma kwa watoto huko Mashariki ya Kati,
hasa kwa ajili ya kuwahudumia watoto wa wakimbizi kutoka Syria.
Askofu mkuu
Giampietro dal Tosso anasema, huduma ya upendo ni asili ya Kanisa kama ambavyo anabainisha
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita; kwani inawahusisha waamini katika
uhuru wao kama wafuasi wa Kristo wenye dhamana ya kushuhudia imani katika matendo
kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa, ili yote yafanyike kwa ajili ya sifa na utukufu
wa Mungu.
Maaskofu mahalia hawana budi kuhakikisha kwamba, wanaratibu huduma
na misaada inayotolewa na Mama Kanisa kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi; upendo
na mshikamano wa dhati kati ya watu! Hii ni huduma inayotolewa kwa kuzingatia Mafundisho
Jamii ya Kanisa, lengo ni kushuhudia imani kwa njia ya huduma ya upendo. Cor Unum
imepewa dhamana na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inaratibu misaada ya Kanisa Katoliki
kwa kushirikiana na Mashirika mbali mbali ya Misaada ya Kanisa Katoliki yaliyoenea
sehemu mbali mbali za dunia.
Askofu mkuu Giampietro Dal Tosso anasema, Mfuko
wa Yohane Paulo II kwa ajili ya Sahel pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya watu Amerika
ya Kusini, ni mashirika mawili ambayo yanasimamiwa moja kwa moja na Cor Unum, katika
mchakato wa kudhibiti kuenea kwa Jangwa la Sahara, Barani Afrika sanjari na kusaidia
mbinu mkakati wa maendeleo na majiundo kwa wananchi wa Amerika ya Kusini.
Mwaka
2014 kutafanyika mkutano wa viongozi wakuu wa Mfuko wa Maendeleo ya watu Amerika ya
Kusini, ili kuangalia vipaumbele kadiri ya maagizo ya Kanisa kwa ajili ya wananchi
wa Amerika ya Kusini.
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.