2014-03-15 10:42:51

Anameremeta, yaani we acha tu!, Je, wewe?


Toka Jangwani kwenye mchanga, mawe na miamba hadi kufikia kumeremeta mlimani. Toka kwenye kiti moto hadi kwenye kidedea cha ushindi. Toka kwenye vishawishi hadi kwenye kugeuka sura. Hiyo ndiyo safari ya Kristu, ambayo pia ni safari ya kila mwanafunzi na mfuasi wake, yaani safari ya kupanda hadi kufikia uhuru kamili: Toka kwenye giza la majaribu hadi kwenye mwanga wa Mungu.

Mwanga wa Mungu ni nguvu na uzuri. Nguvu kwa ajili ya mwili, kwa sababu inatunza, inahifadhi maisha yetu ya kimwili; nguvu ya akili kwa sababu inatusaidia kuona na kuelewa; Nguvu ya moyo, kwa sababu inatuwezesha kupenda vizuri. Ni nguvu na uzuri kusudi nasi tuweze kung’aa katika mtazamo wetu, katika maneno, katika mawazo na moyoni.

“Yesu aligeuka sura mbele yao, na uso wake uling’aa kama jua na mavazi yake meupe kama nuru.” Mara ngapi Mungu katika Biblia anatokea kama jua au kama mwanga wa asubuhi. Jua lina maana ya uhai, maisha. Jua linakuza linakomaza, linazalisha matunda, linachipusha mimea na maua. Jua linachipusha uzuri wa rangi na machoni. Kama vile mmea unavyoonekana unavyokuwa, unavyong’aa mbele ya mwanga na kuubadili kuwa na uhai, ndivyo sisi. Tunakuwa kama majani mbele ya Bwana, tunavyoweza kubadilika mbele ya mwanga na kugeuka kuwa na nguvu za kiutu au kibinadamu za furaha na uzuri.

Yesu anaonesha uso wa kumeremeta kutokana jua la ndani mwake kwa sababu anataka kutueleza kwamba Mungu ni nuru. Uso wa jua ni pia uso wa kila mmoja wetu, yaani ni uso wa kila binadamu, kwa sababu kila mmoja wetu analo jua ndani mwake au hazina ya jua, ambayo ni kule kufanana na Mungu. Tumeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Maisha yote ya kiroho siyo tu ni ya fatiki, ya kuchoka, ya taabu la hasha, bali ni maisha ya furaha, ni maisha ya kuuruhusu mwangauliofunikwa ndani mwetu uweze kutoka na kuangaza wengine.

Petro anaweweseka ““Bwana! ni vizuri sana kuwepo hapa” anataka kusema: “Tubaki hapa hapa pamoja.” Hii ndiyo hamu kubwa ya Petro, ni kilio chake kinachoonesha mshangao mkuu anaposema:“ni vizuri sana”. Anatufanya nasi tuelewe kwamba, ili imani iwe na uhai na ya kweli lazima ianze na kupenda sana na tena ianze kwa mshangao na kusema “ni nzuri sana” kwa kizungu tungesema “waw” ni mshangao mzuri unaotoka kwenye moyo uliojaa mshangao.

Kwa hiyo, Injili ya leo ya kung’ara sura Yesu yataka kutuambia kwamba kipindi cha Kwaresima ni zaidi ya maombolezo na kujitesa, yaani ni kipindi kukutana na wewe mwenyewe kisha unaongokea kwenye nuru na baadaye unameremeta na kuangaza wengine.

Kuwa na imani maana yake ni kuwa na mwanga na uzuri wa kuishi, kujisikia kwamba, kupenda wengine ni kuzuri, kuwa na upendo ni kuangaza. Mtakatifu Paulo anamwandikia Timoti sentensi nzuri sana akisema: “Kristo amefika na kung’arisha maisha” (2Tim 1:10). Uzuri wake siyo tu wa uso na mavazi na kuishia pale mlimani Tabor, bali sasa ni maisha ya kudumu na ni nuru ya wote. Yesu anameremeta ili kuupa mwanga uzuri uwepo wetu, amewasha mambo moto, amezitupa cheche za moto ulimwenguni, ametoa ndoto na nyimbo nzuri katika msafara wetu hapa duniani.

Ingetosha kurudiarudia bila kuchoka kusema: “Amefanya ulimwengu ung’ae. Sasa maisha yanameremeta katika kuona, kukuta / kuujua ukweli furaha ya kumsadiki Mungu huyu. Kwa hiyo uumbaji wote unakuwa wazi na mwanga wa Mungu unaking’aria kila kilichopo na kila uso wa binadamu sasa unameremeta!”

Kilichobaki sasa ni zamu yetu kumeremeta, ni muda wetu wa kugeukia mwanga, kwa sababu mwanga uko tayari hapa: Ni Mungu ambaye tunamchukua, tunambeba ndani mwetu na ndiye anabidi alivunje ndani mwetu giza kama jua linavyovunja giza la usiku. Siku ya Pasaka ataligeuza au kulipindua jiwe ikimaanisha kwamba usiku umeshindwa na mwanga umeshinda daima.

Zaburi yatuambia: “Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, wala nyuso zao hazitaona haya.” (Zab. 34:5). Kwa hiyo tujenge hekalu letu mbele ya Kristu, tujiweke mbele ya mwanga wake, tuishi, tufurahie mwanga ule kama vile mwezi unavyofaidi na kufurahi kuakisiwa na mwanga wa jua. Sisi siyo jua na wala si jua letu, lakini sisi tunaweza kama mwezi kuwepo mbele ya jua, kulifaidi, kulinyonya jua, na halafu kuangaza, kumeremeta, macho yanayoangaza, mwili unaomeremeta, kuwa kama nyota ambazo katika historia zilikuwa zinaongoza wasafiri usiku. Hivi ndivyo walivyofanya mitume, ndivyo alivyofanya Mama Maria, aliye ung’aro wa kutuangazia.
Sisi sote tumeitwa kuwa kama Mama Bikira Maria, yaani mbalamwezi inayoakisi nuru ya jua. Ndani yake huyu dada aliyetutangulia mbele, tumfuate nyuma tukiimba kwa furaha.
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.