2014-03-14 10:37:15

Watoto na vijana wanaongoza katika idadi ya watu Tanzania


Piramidi ya Idadi ya Watu nchini Tanzania inaonesha kuwa idadi kubwa ya watu nchini Tanzania ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 na vijana. Asilimia 44 ya watu wote hapa nchini ni watoto wenye umri chini ya miaka 15, ambapo utafiti wa Mama na Mtoto wa Mwaka 2010 unaonesha kuwa kiwango cha uzazi ni wastani wa watoto 5.4 kwa kila mama mwenye umri wa kuzaa ambao ni miaka 15-49.

Sera ya Vijana Tanzania ya Mwaka 2007 inatambua Vijana kuwa ni watu wote wenye umri wa miaka 15-35, ambapo kulingana na Sensa ya Mwaka 2012 ni asilimia 34.7 ya watu wote nchini Tanzania

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Ikulu wakati akimkabidhi vitabu na majedwali yenye matokeo na machapisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Kulingana na Takwimu, idadi ya watu Tanzania imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka watu Milioni 12.3 kwa Mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 Mwaka 2012.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia kubwa ya Vijana wenye umri wa miaka kati ya 15-35 wakati Mkoa wa Singida ukiwa na asilimia ndogo zaidi.

Kulingana na Takwimu, zaidi ya nusu ambayo ni asilimia 52.2 ya watu wote nchini, wako katika umri wa kufanya kazi ambapo Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya watu wenye umri huu wa kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu uko chini zaidi kwa kuwa na asilimia 45.5 ya watu hawa. Katika takwimu hizo, zaidi ya nusu ya watu katika Mikoa ya Simiyu, Rukwa na Geita ni Watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.

Dk. Chuwa pia amebainisha kuwa Takwimu zinaonesha kuwa rasilimali watu kwa ajili ya kuzalisha na kuongeza Uchumi na kupunguza Umaskini sio tatizo hapa nchini na kinachotakiwa ni watu wote kutumia fursa zilizopo nchini kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuinua uchumi wa Nchi.

Kulingana na takwimu asilimia 5.6 ya watu hapa nchini ni wazee na takwimu hizi zinaonesha kuwa wazee kwa asilimia kubwa wako katika Mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo asilimia ndogo zaidi wapo katika Mikoa ya Dar es Salaam na Mjini Magharibi. Kwa mujibu wa Sera ya wazee Tanzania, Mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 au zaidi.

Takwimu pia zinazidi kuonesha kuwa asilimia ya watu wanaoishi Mijini imeongezeka zaidi ya mara tano ambapo ni asilimia 6.4 mwaka 1967 na kufikia asilimia 29.6 kwa mwaka 2012. Jiji la Dar es Salaam lina asilimia 10 ya watu wote hapa Tanzania Bara wakati Mjini Magharibi ina asilimia 46 ya watu wote wa Zanzibar. Sensa pia imeonesha kuwa Wanawake ni wengi zaidi, kwa asilimia 51 ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 49 kama ilivyo katika nchi nyingi Barani Afrika.








All the contents on this site are copyrighted ©.