Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka A wa Kanisa
Tunaendelea na kipindi cha Kwaresima, tafakari masomo Dominika II mwaka A. Neno la
Mungu latualika kutafakari juu ya wito wetu kielelezo kikiwa wito wa Abramu.
Mpendwa msikilizaji,
Somo la kwanza latuonesha jinsi historia ya wokovu ilivyosimika miguu, pale Mungu
anapomwita kwanza Abramu awe Baba wa imani. Kwa kumwita Abramu Mungu atuonesha lile
pendo na namna yake ilelile ya kumwendea mwanadamu kabla ya mwanadamu hajanyanyua
mguu kumtafuta Mungu. Tunatambua kuwa Abramu aliishi Mesopotamia miaka 2000KK na katika
nchi yake hiyo kulikuwa na kila aina ya utajiri, hata hivyo kulikuwa na machafuko
wakati fulani.
Mungu anamwita, na Abramu anasikia sauti ya Mungu pamoja na
kwamba kulikuwa na kelele nyingi katika nchi yake hiyo. Abramu anasikia sauti ya Mungu
kwa sababu ya imani yake na anaondoka kadiri ya matakwa ya Mungu. Hata hivyo yafaa
kujiuliza hivi ilikuwa rahisi kuondoka hapo nyumbani na kuelekea nchi asiyoijua? Kwa
vyovyote vile alipata ugumu fulani lakini kwa sababu ya imani aliondoka!
Mpendwa
msikilizaji, Abramu anaitwa kuacha uhakika wa maisha na kwenda ambapo hakuna uhakika,
hili ni jambo la ajabu, lakini linasukumwa na ahadi za Mungu yaani atapewa ardhi mpya,
atakuwa na ustawi na baraka tele. Katika hili twajifunza nini! Twajifunza maisha ya
kujitoa kiaminifu na kujibandua katika fikira zetu za kizamani, yaani, pingamizi kwa
imani na kuanza maisha mapya, maisha yenye baraka toka kwa Mungu. Safari ya Abramu
ni safari yetu ya imani, ndiyo kwaresima yetu yaani kubadilika na kubadilisha maisha
yetu. Yote haya yatawezekana katika tumaini na imani kama Abramu alivyotumaini bila
kuona.
Katika somo II Mt. Paulo anamtia moyo Mt. Timoteo, Askofu wa Efeso,
kuvumilia mateso na taabu, pamoja na changamoto za kitume katika jumuiya yake. Wakati
Mt. Paulo anaandika ujumbe huu, kulikuwa na migongano na malumbano katika Efeso na
hivi kuleta hatari kwa maisha ya kitume. Basi Mt. Paulo akisimika ujumbe wake katika
Bwana wetu Yesu Kristu, anasema, mauti yatabatilishwa katika yeye, kumbe Mt. Timoteo
asiwe na mashaka, cha msingi amtegee yeye aliyemwita katika mwito mtakatifu.
Katika
somo la Injili mwinjili Matayo atuambia Yesu ni nani akitumia alama na ishara kadhaa
katika Injili yake. Leo Bwana yuko mlimani, akiwa na Mitume watatu na anageuka sura,
mavazi yanakuwa meupe na hatimaye kunaonekana Bwana akizungumza na Musa na Eliya.
Si hayo tu bali kutatokea wingu jeupe na sauti kutoka katika wingu hilo ikitangaza
huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye, msikieni yeye.
Katika
ishara ya mlima tunatambua mara zote Bwana anapotaka kutenda jambo muhimu katika Injili
ya Mathayo daima anakwenda mlimani. Ndiyo kusema, matukio ya mlimani tuyafamuyo ni
kama ifuatavyo: Tangazo la heri Nane, majaribu tuliyoyasikia katika Dominika iliyopita,
ongezeko la Mikate, na mwisho wa Injili Bwana mfufuka anapowatuma Mitume kwenda duniani
kote anakutana nao mlimani. Jambo hili tunalikuta katika Agano la Kale ambapo Musa
atathibitishiwa Agano na kupokea amri za Mungu akiwa mlimani, (Kut. 24:12).
Mpendwa
mwana wa Mungu, kuhusu habari ya kuwa na Mitume pale mlimani si jambo jipya bali lina
uhusiano na uwapo wa Musa mlimani pamoja na Yoshua wakati wengine wakiachwa chini
ya mlima. Pale mlimani Musa atafunikwa na wingu na utukufu wa Mungu utatua mlimani
Sinai kwa SIKU SITA na siku ya saba, Mungu anamwita Musa toka wingu lile. Mpendwa
msikilizaji matukio haya yanajionesha katika Bwana, kumbe Mwinjili Matayo ataka kutumbia
Kristu Masiha, ni Musa mpya, ni yule atakayeongoza taifa jipya la Mungu linalowakilishwa
na Mitume watatu pale mlimani. Ni yule anayetoa sheria mpya na ukamilifu wa ufunuo
wa Mwenyezi Mungu.
Mpendwa msikilizaji Bwana anaonekana katika mavazi meupe,
ikiwa ni alama ya uwapo wa Mungu katika nafsi ya Yesu Kristu, hili linaambatana na
wingu jeupe ambao lamwakilisha Mungu. Kumbukeni Waisraeli wanapotoka utumwani Misri
wataongozwa na wingu jeupe, ambayo ni alama na ishara wazi ya ulinzi wa Mungu katika
safari yao hiyo ya kurudi nyumbani, (Kut. 13:20-22).
Mpendwa msikilizaji, Mwinjili
anaweka pia mbele yetu ishara ya sauti toka juu, ambayo tuliisikia wakati wa ubatizo
wa Bwana, lakini katika tukio hili ataongeza MSIKIENI YEYE. Ni Mungu anayesema na
watu wake kwa njia ya Mwanae mpenzi. Basi unaalikwa katika kwaresima hii kusikia anachosema
Bwana kwa njia ya Neno lake. Ishara nyingine muhimu ni uwepo wa Musa na Elia.
Hawa
wanawakilisha Agano la Kale na hivi wanapotoweka wanaonekana Mtume watatu wakimtazama
Bwana. Ndiyo kusema Kristo Masiha ndiye sasa sheria mpya kwa ajili ya Agano Jipya,
sheria tutakiwayo kuitazama na kuishika na hivi msikieni yeye. Wakati ndo huu, wakati
wa kupanda, wakati wa kupalilia na kuondoa magugu na vinyemelezi katika mashamba ndiyo
mioyo yetu.
Mpendwa msikilizaji, jambo jingine la kutusaidia kukua kiroho ni
lile la Mtakatifu Petro kumwambia Bwana, yakuwa, yafaa kukaa hapo mlimani na kujenga
vibanda vitatu. Katika hili Petro anadhani Yesu ni mtu mkubwa katika uzito uleule
wa manabii, wakati kwa hakika ni mkuu kuliko wao, ni Mwana wa Mungu na hivi kila mmoja
analikwa kumsikia yeye tu. Mpendwa mwana wa Mungu, kwako wewe wajibu ni kutafakari
haya yote na kuyaweka moyoni lakini hasa kujenga usikivu wa kudumu, hujachelewa katika
kwaresima hii mpaka mwisho wa maisha yako hapa duniani.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.