2014-03-14 09:00:31

Salam na matashi mema kwa Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha kumbu kumbu ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kwa sala na mafungo ya kiroho. Hata hivyo amepokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kati ya viongozi wa kimataifa waliotuma salam zao ni pamoja na Rais Giorgio Napolitano wa Italia anayekiri kwamba, maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko umewagusa watu wengi ndani na nje ya Kanisa Katoliki. Papa anaonesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wote wanaoteseka kutokana na ukosefu wa misingi ya haki, amani na usawa. Mwanadamu na haki zake msingi anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Patriaki wa Kanisa la Kiorthodox Mosco, Cyril anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kiekumene, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo; mambo ambayo yamejionesha kwa namna ya pekee, tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.

Professa Foad Aodi kwa niaba ya Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiislam wanaoishi nchini Italia ametuma pia salama na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuwa makini katika majadiliano ya kidini yanayopania kujenga na kudumisha: haki, amani, upendo na upatanisho wa kweli.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linampongeza Baba Mtakatifu kwa msukumo wake wa pekee kwa Kanisa kuwaendelea watu wanaoishi pembezoni mwa Jamii, ili kuwaonjesha: Injili ya Furaha, Huruma na Upendo wa Mungu kwa watu. Jitihada za kudumisha dhamana na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, ambazo zimevaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu ni kati ya mambo ambayo wanaendelea kumshukuru ili Kanisa liweze kutoa majibu muafaka kwa changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika mikakati yake ya kichungaji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linasema: huruma na upendo wa Mungu ni kati ya kauli mbiu zinazofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, mwaliko wa kuendelea kutangaza Injili ya Furaha, ili kuwawezesha kukutana na Yesu Kristo anayewakomboa kutoka katika dhambi na mauti; anayewapatia furaha ya ndani na faraja kutokana na upweke hasi wanaokumbana nao katika maisha yao ya kila siku. Changamoto kwa Wakristo kujifunga kibwebwe katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya ni dhana inayofanyiwa kazi na Kanisa Katoliki nchini Ireland. Maaskofu Katoliki Ireland wanamtakia kheri na baraka Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema, linaendelea kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wanaunga mkono changamoto ya toba na wongofu wa ndani pamoja na kuendelea kukuza ari na moyo wa Kimissionari ndani ya Kanisa, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu ndani ya Kanisa. Kanisa Katoliki nchini Italia linapenda kushikamana na Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake kwa Kanisa la Kiulimwengu.







All the contents on this site are copyrighted ©.