2014-03-14 12:28:25

Figo huzeeka kama wewe. Jali afya ya figo zako!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda aagiza huduma za upimaji wa figo zitolewe kwa kuzunguka katika kanda zilipo nchini na kuacha utamaduni wa kutoa huduma hizo wakati wa maadhimisho hayo tuu. Alisema hayo Alhamisi, tarehe 13 Machi 2014 wakati wa akifunga kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Afya ya Figo Duniania yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyerere mkoani Dodoma, yenye kauli mbiu Figo Huzeeka kama wewe. Jali Afya ya Figo zako.

Akizungumza na wananchi wakati wa kilele hicho Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi kujenga utamaduni wa kujali na kupima afya zao mara kwa mara: ‘‘Tumieni fursa hii ya uwepo wa huduma hizi karibu nanyi kujua hali ya afya ya figo zenu ili mchukue hatua stahiki mapema, kuchelewa kujua afya yako kunaweza kuathiri pia urahisi wa matibabu kama ukigundulika kwamba umeathirika na Ugonjwa wa Figo“.

Alisema, huduma kama hizi za Klinic ya Umma yaani Public Clinic zitolewe mara kwa mara kikanda bila kusubiria maadhimisho ili kuweza kuwafikia wananchi kwa wakati na kuendelea kuhamasisha huduma za afya za aina hii kwa wananchi, walau kuweza kutoa huduma hizi katika Kanda ya juu Kusini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kaskazini mtakuwa mmefanya jambo la busara sana kwa watanzania.

Waziri Pinda alisema, zipo njia muhimu za kuzingatia ili kuepukana na ugonjwa wa figo kama inavyoelezwa na wataalum kuwa ni pamoja na kufanya mazoezi kwa wingi, kunywa maji glass 6 hadi 8 kila siku, kuacha kuvuta sigara, kuzingatia uzito wa mwili na kuacha kutumia dawa kabla ya maelekezo ya daktari, aliongezea Waziri Pinda.

Waziri Mkuu alisema, ‘‘Dawa hapa ni Kinga na Sio Tiba“ hivyo aliwaomba wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kufahamu na kupunguza madhara makubwa ya ugonjwa huu.

Changamoto kubwa iliyopo mbele yetu kama serikali ni upungufu wa madaktari bingwa wa kutosha wa kutibu magonjwa ya figo, kupandikiza figo na gharama kubwa za matibabu ya figo ambayo huduma hiyo haipatikani hapa nchi hivyo: ‘‘Serikali itachukua jukumu la kuongeza idadi ya wataalamu wa figo na kwa kuzingatia suala hili tutaliweka katika bajeti ya Serikali ya mwaka“, alisema Waziri Mkuu.

Alieendelea kusema kuwa, kuna Sera ya Magonjwa ya Afya ya mwaka 2007, Miongozo na Mikakati ya kupambana na ugonjwa huu hivyo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Figo Tanzania, itazindua ripoti ya Wiki ya Afya ya Figo 2013 Tanzania, ambapo ripoti hiyo itaonesha kuwa watu 4,325 walijitokeza kupima afya za figo zao na kati ya hao asilimia 15 (623/325) walipatikana na matatizo ya figo.

Ni dhahiri kuwa, juhudi hizi za kubaini ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa Figo, zinazofanywa na Serikali zitarahisisha na kuwezesha wananchi wengi kupata taarifa mbalimbali kutoka ndani na nje ya Nchi kuhusu afya ya figo.

Pamoja na kuhudhuria Kilele cha maadhimisho hayo, Waziri Mkuu alizindua rasmi tovuti ya Taasisi ya Taifa ya Figo ambayo itakuwa inalezea masuala yote yanayohusu figo na kusisitiza wananchi kutumia tovuti hiyo kujifunza masuala yote masuala mbalimbali ya figo.

Mapema, Prof. Ephata Kaaya, ambaye ni Mjumbe wa Bodi Taasisi ya Taifa ya Figo alieleza kuwa dira na malengo ya taasisi hiyo ni kuwa kitovu cha taifa katika kuendeleza na kuthibiti magonjwa ya figo kwa kuendelea kutoa elimu kwa wingi, kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kufaham takwimu halisi za ugonjwa huo, kwani katika maadhimisho haya jumla ya wananchi 3800 wameweza kusajiliwa na wananchi 3120 wamefanyiwa uchunguzi.

Taasisi ya Taifa ya Figo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya, Sekta Binafsi na wananchi kuendesha masuala ya matibabu ya figo na kubuni mbinu mbadala ya upatikanaji wa fedha ili kuweza kuendesha Taasisi hiyo ambayo hivi sasa inatoa huduma za matibabu ya figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Rufaa Mbeya, na huduma hizo pia zitaanzishwa katika Hospitali za Rufaa Bugando na KCMC.








All the contents on this site are copyrighted ©.