Askofu Dallu ateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Songea, Tanzania
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Damian Denis Dallu wa Jimbo Katoliki Geita,
Tanzania kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Songea. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu
mteule Dallu alizaliwa kunako Mwaka 1956 huko Kiponzelo, Jimbo Katoliki la Iringa.
Baada ya masomo
na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe 15 Novemba 1984. Tarehe 6 Mei 2000
akateuliwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Tanzania. Askofu Dallu aliwekwa
wakfu na hatimaye kusimikwa kuwa ni Askofu wa pili wa Jimbo la Geita hapo tarehe 30
Julai 2000.
Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu mteule Dallu
anazungumzia umuhimu wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki kama muhtasari wa imani
inayoungamwa na kuadhimishwa na Mama Kanisa. Hii ni imani inayomwilishwa katika maisha
adili kwa kufuata Amri za Mungu na kumwilishwa katika sala. Katekisimu Mpya ya Kanisa
Katoliki imetoa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kutoa kipaumbel
cha kwanza kwa binadamu na haki zake msingi.
Askofu mkuu mteule Damin Denis
Dallu anasema, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni nyenzo msingi katika maisha na utume
wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mbali mbali za kichungaji katika ulimwengu
mamboleo. Ni mwaliko kwa Kanisa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene
ili kujenga misingi ya haki na amani kwa Familia nzima ya binadamu. Kumbe, Katekisimu
Mpya ya Kanisa Katoliki na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni mafundisho mfungamano
kwa binadamu wote.