Wajibu wa kuuishi, kuulinda na kuusimamia ukweli kishuhuda!
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea sehemu ya pili ya Ujumbe wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2014. Mara ya
mwisho, tuliwashirikisha utangulizi, leo tunaendelea na sura ya kwanza inayopembua
wongofu wa kweli unaomweka mtu huru na sehemu ya pili inajadili wajibu wa kuuishi,
kuulinda na kusimamia ukweli kishuhuda. Ndani ya viunga vya Radio Vatican kukujuza
zaidi ni Sr. Gisela Upendo Msuya. SURA YA KWANZA WONGOFU
WA KWELI HUTUWEKA HURU
Mungu alipenda kujifunua kwa wanadamu kupitia manabii
na mwanawe wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Hata leo, Roho Mtakatifu analiongoza Kanisa
katika kuendelea kuujua ukweli wa kiimani katika safari ya pamoja ya kiroho kuelekea
uhuru kamili wa roho zetu. Ukweli wa kiimani huleta uhuru wa kiroho. Mwaka uliopita
Kanisa liliadhimisha Mwaka wa Imani ikiwa ni sehemu ya kuwakumbusha wanakanisa wote
juu ya wajibu wao wa kiimani katika Kanisa na katika jamii.
Kwa kuishi ipasavyo
imani yetu ya kikristo tunashiriki wajibu wa kuujenga Ufalme wa Mungu ambao mojawapo
ya nguzo zake saba za msingi ni ukweli! Hakika, ufalme wa Mungu, kama Mama Kanisa
anavyotangaza katika utangulizi wa Misa ya sherehe ya Kristo Mfalme ni ufalme wa UZIMA
na KWELI, ufalme wa NEEMA na UTAKATIFU, ufalme wa HAKI, MAPENDO na AMANI. Mungu wetu
ni UKWELI na ni MKWELI. Tunasadiki na kukiri kwamba hadaganyi wala hadanganyiki. Imani
ni wajibu wa kushiriki kuujenga Ufalme wa Mungu, ufalme ambao msingi wake ni ukweli,
kwa sababu Mungu ni ukweli.
Mwanadamu aliyekombolewa kwa damu ya thamani kubwa
sana ya Kristo iliyomwagika pale Kalvari, amepata kurudishiwa hadhi ya kuwa mwana
huru wa Mungu akikombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Uhuru anaoupata mwanadamu una
gharama kubwa na thamani kubwa. Uhuru wa kweli ni uhuru ndani ya Mungu; ni uhuru katika
Mungu. Uhuru wa kweli huambatana na utii wa sheria ya Mungu na uwajibikaji unaodai
unyenyekevu na nidhamu ya hali ya juu. Uhuru huu ni kinyume na uhuru usio na mipaka
ambao jamii ya sasa inadai,uhuru ambao hupingana na malengo ya Muumba na taratibu
na miongozo halali mbele za Mungu iliyowekwa na jamii.
Kanisa, ukweli na
uhuru
Kanisa ambalo ni ishara ya wokovu na alama ya uwepo hai wa Kristo
aliye njia, ukweli na uzima katika ulimwengu wa sasa ni sisi tulioalikwa kuwa Familia
ya Mungu. Kwa kumkiri Kristo na kwa kubatizwa kwetu tumekuwa Rafiki na wadau wake
Yesu Kristo (Yn 15: 14). Kwa namna hiyo sisi sote Familia ya Mungu – Wakleri, Watawa
na Waumini Walei – tu chombo mikononi mwa Kristo kwa kushiriki kikamilifu kazi ya
Kristo ya kuwakomboa watu.
Kwa mantiki hiyo, Kanisa linao wajibu wa kwanza
kabisa kuulinda ukweli, kuusimamia, kuushi na kuutangaza. Kanisa ni chombo kiletacho
wokovu kwa ulimwengu na kuwaweka huru wanadamu walio katika utumwa unaojidhihirisha
katika sura mbalimbali kama vile, umasikini, ufisadi, rushwa, ushirikina, magonjwa,
siasa chafu, kutokuwajibika, ubinafsi,nk.
Kanisa ni chombo cha Kristo cha kuwaletea
watu uhuru wa kweli. Roho wa Bwana, aliye juu ya Yesu (Lk 4:18,19) yuko pia juu ya
Kanisa lake ambalo analituma kuwafungulia watu vifungo vyao mbalimbali na kuwaachia
huru waliosetwa (Lk 4:18-19).
Ukweli kama tunu ya kimungu lazima uote mizizi
katika mioyo ya wanadamu walioumbwa kwa sura na mfano wake (Kut 1:26). Ni wajibu wa
kila mwanadamu kuutafuta ukweli na kuujua. Kwa njia ya ufahamu, mwanadamu anaalikwa
kuutafuta ukweli kwani ndio njia pekee ya kumweka huru na kuufikia wokovu. Maana Mungu
amemwachia mwanadamu uhuru kusudi aifuate nia yake (YBS 14:15), na hivyo amtafute
Muumba wake kwa hiari, na hatimaye aufikie ukamilifu ulio bora na wenye heri, pasipo
shuruti na kwa kuambatana na Mungu. Kanisa linamsaidia mwandamu kufanikisha kuufikia
ukweli na kwa uhuru kupitia neema za Mungu.
SURA YA PILI WAJIBU
WA KUUISHI, KUULINDA NA KUUSIMAMIA UKWELI KISHUHUDA
Waamini waliowekwa
huru na Kristo, wanao wajibu wa kuujua ukweli, kuutafuta, kuulinda na kuusimamia kwa
lengo la kuleta huru wa kweli kwa manufaa ya wote. Huko ndiko kuwa mfuasi wa Kristo
aliyesema: “Mimi nilikuja ulimwenguni; ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli
hunisikia sauti yangu” (Yn 18:38).
Jamii leo hii imegawanyika juu ya uhuru
ambao wanajamii wanapaswa kuwa nao. Wazazi wanaamini kuwa uhuru ni kutenda jambo lolote
bila kubughudhiwa na yeyote, hata kama tendo hilo ni kinyume na misingi ya maadili.
Watoto wanataka uhuru binafsi katika kupanga na kuamua mambo yanayowahusu. Watoto
wasingependa kupokea malezi na maelekezo iwe ni ya wazazi au ya jamii. Vijana wanapenda
kuamua mambo yao kama wanavyoona, wakipuuzia uzoefu na ushauri wa wakubwa wao. Tujiulize:
Je, huu ndiyo uhuru tuutafutao? Katika mazingira kama haya kinachotafutwa si uhuru
bali kuishi kwa kuheshimu vionjo binafsi. Ni muhimu sana kwa wanafamilia kuwa na uhuru
wa pamoja katika kupanga na kuamua masuala kifamilia.
Tukijiruhusu kama wanajamii
kuishi katika uholela upendo unatoweka. “Usikubali kitu chochote kuwa ni ukweli kama
kinakosa upendo. Na usikubali kitu chochote kuwa ni upendo kama kinakosa ukweli! Hali
moja bila nyingine ni uongo unaoharibu”. Kwa sababu “ni katika ukweli tu ndipo upendo
inang’aa, ni katika ukweli tu ndipo tunapoweza kuuishi upendo kwa hakika."