TANZIA: Kardinali Josè Cruz Policarpo amefariki dunia
Kardinali Josè da Cruz Policarpo, Patriaki mstaafu wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno,
amefariki dunia, Jumatano tarehe 12 Machi 2014 akiwa na umri wa miaka 78. Watu wengi
ndani na nje ya Kanisa Katoliki wameguswa sana na msiba huu kwani ni kiongozi aliyeonesha
imani kubwa, uvumilivu pamoja na kujitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa Mungu
na jirani zake.
Kardinali Policarpo kwa miaka kumi na mitano alibahatika kuliongoza
Jimbo kuu la Lisbon, yaani kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2013. Mwenyeheri Yohane Paulo
II akamteua na kumsimika kuwa Kardinali kunako Mwaka 2001. Kwa sasa Baraza la Makardinali
linaundwa na Makardinali 217, kati yao kuna Makardinali 120 wenye haki ya kupiga na
kupigiwa kura wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na wengine
97 waliobaki hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura.
Marehemu Kardinali
Policarpo alizaliwa tarehe 26 Februari 1936 huko Alvorninha, Ureno. Akapadrishwa tarehe
15 Agosti 1961. Kuanzia Mwaka 1988 hadi mwaka 1996 alikuwa ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Kanisa Katoliki Ureno na ni mwandishi wa vitabu na makala mengi.
Tarehe 26
Mei 1978 aliteuliwa kuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Lisbon, akawekwa wakfu
tarehe 29 Juni 1978. Tarehe 5 Machi 1997 aliteuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II
kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo kuu la Lisbon na akamrithi Kardinali Antonio Ribeiro
kama Patriaki wa Jimbo kuu la Lisbon hapo tarehe 24 Machi 1998. Alikuwa pia ni Mkuu
wa Chuo Kikuu cha Ureno.
Mwaka 1999 hadi mwaka 2005 alikuwa ni Rais wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Ureno. Tarehe 3 Mei, 2011 alichaguliwa tena kuwa ni Rais wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Ureno. Tarehe 18 Mei 2013 akang'atuka kutoa madarakani kama Patriaki
wa Jimbo kuu la Ureno.