2014-03-13 09:52:38

Papa Francisko ni mfano wa kuigwa na wengi!


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kupokea salam na matashi mema kutoka katika Mabaraza mbali mbali ya Maaskofu, viongozi wa Serikali pamoja na watu binafsi kwa kutimiza Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki hapo tarehe 13 Machi 2013.

Tangu wakati huo Kanisa likaanza utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii pamoja na Familia ya binadamu katika mwanga wa Injili ya Kristo. Utu na heshima ya mwanadamu vimeendelea kupewa umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa, kwa njia ya ushuhuda wa unyenyekevu na maisha manyofu ynayooneshwa na Papa Francisko. Lengo ni kumwonjesha binadamu huruma na upendo wa Mungu.

Hivi ndivyo anavyosema Askofu mkuu Joseph Edward Kurtz, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika salam na matashi mema kutoka katika Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, wakati huu Baba Mtakatifu anapoadhimisha Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Amekuwa ni mfano bora wa kuigwa na viongozi wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Ni kielelezo bora cha kuigwa katika maisha na utume: kama Mchungaji, Padre na kama Kiongozi Mkatoliki, lakini zaidi kama binadamu. Baba Mtakatifu amesaidia kuleta nguvu na mwamko mpya kwa viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao; amekazia na kuhimiza Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayojikita katika: maisha, utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha kipaumbele cha pekee kwa Familia na changamoto zake ili kukabiliana na changamoto hizi za kichungaji, huku Kanisa likiwa limeshikamana katika umoja na udugu. Kanisa linapenda kuangalia wapi ambako ni chimbuko la matatizo ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo, kwani kuanguka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ni kuporomoka kwa Jamii nzima ya mwanadamu. Kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha ya ndoa na familia ni kutaka kuwajengea watu matumaini mapya katika maisha yao, licha ya magumu na majanga wanayokumbana nayo!

Kwa upande wake Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulichangamotisha Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, Umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, Neno la Mungu linalopaswa kutangazwa kwa furaha na bashasha kubwa na wala si kama watu walionjeshwa pilipili kichaa!

Umoja, usawa na udugu ni changamoto kuu zinazopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko. Jimbo kuu la India, linaendelea kumuenzi Baba Mtakatifu kwa Ibada ya Misa Takatifu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili aweze kufanikisha nia njema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.

Mjini Assisi, Wafranciskani kwa namna ya pekee wanaendelea kumwimbia Mungu utebnzi wa sifa na shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko kumuenzi Mtakatifu Francisko wa Assisi katika maisha na karama yake kwa ajili ya Kanisa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ufukara wa Kiinjili, Amani na Utunzaji bora wa mazingira ni mambo muhimu katika ulimwengu unaoendelea kukabiliwa na maafa mbali mbali. Katika mambo yote, Yesu, Kanisa na Mwanadamu wapewe kipaumbele cha kwanza.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.