2014-03-13 12:22:33

Marehemu Askofu mstaafu Fortunatus Lukanima kuzikwa Kagunguri, Jimbo Katoliki la Bunda


Waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema nchini Tanzania wanaendelea kuomboleza kifo cha Askofu mstaafu Fortunatus Lukanima wa Jimbo Katoliki Arusha, kilichotokea kwenye Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza, Jumatano tarehe 12 Machi 2014 kwa Ibada ya Misa Takatifu na Rozari Takatifu.

Ratiba elekezi ya maziko inaonesha kwamba, Alhamisi tarehe 13 Machi 2014 majira ya jioni, Waamini wa Jimbo kuu la Mwanza wanaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Tokeo la Bwana, Jimbo kuu la Mwanza. Ijumaa tarehe 14 Machi 2014, majira ya asubuhi, kutakuwa na Ibada ya Neno la Mungu katika Hospitali ya Rufaa Bugando na baada ya hapo, msafara utaanza safari kuelekea Kagunguri, Kisiwani Ukerewe, Jimbo Katoliki la Bunda.

Wakiwa Nansio, waamini wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu majira ya mchana na baadaye kutakuwa na mkesha wa Sala kwenye Kanisa la Kagunguri, moja ya Makanisa Mama Jimbo kuu la Mwanza kwa wakati huo.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Mazishi ya Askofu mstaafu Fortunatus Lukanima, yatafanyika Jumamosi, tarehe 15 Machi 2014, majira ya asubuhi. Ni Ibada inayotegemewa kuhudhuriwa na waamini wengi kutoka Jimbo kuu la Arusha, Jimbo kuu la Mwanza na Jimbo Katoliki la Bunda. Apumzike kwa Amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.