Changamoto kwa waamini ni kuwa waaminifu kwa Kristo sanjari na kuchuchumilia utakatifu
wa maisha!
Askofu Alvaro del Portilo alikuwa ni Padre mchapakazi aliyesimika maisha yake ya imani
katika mwamba imara ambao ni Yesu Kristo. Ni ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko
ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda
kwa washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu alipozaliwa
Askofu Portilo, Mkuu wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Santa Croce, kilichoko mjini Roma,
ambaye anatarajiwa kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri hapo tarehe 27 Septemba 2014.
Askofu
Portilo alijitahidi katika utume wake, kiasi kwamba, alibahatika kutembelea Mabara
yote, huku akifuata nyayo za Mtakatifu Josemarìa. Ni mfano na kielelezo cha maisha
yanayojikita katika unyenyekevu, uchangamfu na ukimya, lakini unaopania kuendeleza
mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha na ushirikiano katika kazi ya kumkomboa
mwanadamu.
Kongamano hili limefunguliwa, Jumatano, tarehe 12 Machi 2014 kwa
hotuba ya utangulizi iliyotolewa na Askofu Javier Echevarrìa, Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Santa Croce na Mkuu wa Shirika la Kazi ya Mungu, maarufu kama Opus Dei. Anamshukuru
Baba Mtakatifu Francisko anapofanya kumbu kumbu ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa
kuliongoza Kanisa Katoliki, changamoto kwa kila Mkristo kuhakikisha kwamba, anawatangazia
wengine Injili ya Furaha kwa kuwashirikisha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na
mipaka.
Papa Francisko ni mtu wa sala, aliyebahatika kuwa na kipaji cha kusikiliza
kwa makini pamoja na kukutana na watu, sababu msingi ya kumshukuru Mungu kwa uwepo
na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Anasema, Askofu Portilo kwa muda zaidi ya miaka
arobaini alionesha uaminifu wake kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kwa Mtakatifu
Josemarìa, mwanzilishi wa Shirika la Opus Dei.
Ni kiongozi aliyefaulu kumwilisha
karama ya mwanzilishi wa Shirika la Opus Dei linaloundwa na Makleri pamoja na Waamini
Walei na kwamba ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa Mungu na jirani. Washiriki
wa Kongamano hili wamekusanya fedha kwa ajili ya kugharimia miradi mbali mbali kwa
Mwaka 2014 inayolenga kuwasaidia watu wa Nigeria kupata tiba; watoto wanaoishi nchini
Pwani ya Pembe kupata huduma ya lishe bora pamoja na kuendeleza maboresho ya huduma
ya afya Kinshasa, DRC.
Wajumbe wamechagia pia fedha kwa ajili ya kusaidia
masomo kwa Mapadre kutoka Afrika wanaosoma kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Santa
Croce, kilichoko mjini Roma. Kongamano hili linafungwa rasmi, Ijumaa tarehe 14 Machi
2014.