2014-03-12 07:52:35

Mwaka mmoja tangu Papa Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitekeleza dhamana na utume wake katika mazingira magumu na kwamba kuchaguliwa kwa Papa Francisko kulivuta hisia kubwa miongoni mwa vyombo vya habari. RealAudioMP3

Haikuwa rahisi anasema Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican kuwaridhisha waandishi wote wa habari waliokuwa wanafuatlia mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Takwimu zinaonesha kwamba, kulikuwa na waandishi wa habari elfu sita kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Waandishi wengi wa habari walikuwa na mtazamo hasi kuhusu maisha na utume wa Kanisa, kashfa za nyanyaso za kijinsia, wizi wa nyaraka za siri ni mambo ambayo yalichafua hali ya hewa ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Benedikto XVI alisimama kidete kuhakikisha kwamba, anaanza mchakato wa kulisafisha na kulitakasa Kanisa, hata hivyo bado alikabiliana na mwono hasi kutoka kwa vyombo vya habari, daima walionesha mashaka na hatua mbali mbali zilizokuwa zinachukuliwa na Papa mstaafu Benedikto XVI pamoja na kusahau kwamba, hata katika mazingira kama haya, bado kulikuwa na idadi kubwa ya viongozi wa Kanisa walioendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa uaminifu, ukweli, uwazi na weledi.

Wizi wa nyaraka za siri kutoka mjini Vatican ni swala la kiufundi linalopaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa anasema Padre Lombardi katika mahojiano na Shirika la Habari la Zenit, kama sehemu ya tafakari ya kina, mwaka mmoja tangu Papa Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Wizi wa nyaraka za siri, sakata la Askofu mkuu Carlo Maria Viganò pamoja na Benki ya Vatican ni kati ya mambo yaliyokuwa yanachanganya vichwa vya watu wengi mjini Vatican.

Baadhi ya watu walihitimisha kwa kusema kwamba, ukosefu wa mawasiliano sahihi ulikuwa ni chanzo cha wizi na kuvuja kwa nyaraka za siri kutoka Vatican. Sekretarieti ya Vatican ikaliona hilo na kuamua kumwajiri Bwana Greg Burke, mshauri katika masuala ya mawasiliano ndani ya Sekretarieti ya Vatican. Hapa kunaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya uongozi wa Kanisa, maamuzi yanayofikiwa katika vikao halali pamoja na mchakato wa kuandaa hati na nyaraka mbali mbali. Mambo kwa sasa anasema Padre Lombardi yako shwari.

Wazo la kung’atuka kutoka madarakani, lilikwishaoneshwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika mahojiano yaliyofanywa na Peter Seewald na baadaye kuchapishwa kwenye kitabu cha “Mwanga wa Dunia”. Hapa Baba Mtakatifu mstaafu anasema wazi kabisa kwamba, kuna wakati ambapo Khalifa wa Mtakatifu Petro anaweza kuonesha utashi wa kung’atuka kutoka madarakani kwa uhuru kamili, kama inavyojionesha kwenye hotuba yake aliyoitoa tarehe 11 Februari 2013 kwamba, baada yak usali na kutafakari kwa kina, kwa hiyari yake mwenyewe anaona ang’atuke kutoka madarakani ili kutoa nafasi kwa Makardinali kumchagua Khalifa mwingine wa Mtakatifu Petro. Anafanya hivi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.

Katika kipindi cha mchakato wa uchaguzi kinachojulikana kama “Sede Vacante”, wahusika wakuu waliomwezesha Padre Lombardi kutekeleza utume wake kwa ufanisi ni: Sekretarieti ya Vatican, Kardinali Tarcisio Bertone, Dekano wa Makardinali, Vikosi vya ulinzi na usalama, Mkuu wa Nyumba ya Kipapa; wanasheria na wanahistoria waliochimba historia ya Mikutano ya Makardinali, ili kuwawezesha waandishi wa Habari kupata majibu sahihi, ingawa haikuwa kazi rahisi!

Padre Lombardi anasema, alijitahidi kutoa habari msingi na kumwachia kila mwandishi wa habari kutekeleza wajibu wake akiongozwa na dhamiri yake. Anasema, hawakuwahi kufahamiana kwa karibu na Papa Francisko kabla ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki. Ni kiongozi anayetoa changamoto endelevu katika mchakato wa kumilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Anaonesha hija ya kutaka kutekeleza mapenzi ya Mungu katika utume na maisha yake katika hali ya kawaida pasi na makuu.

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha dira na mwelekeo mpya katika mawasiliano kwa kuvunjilia mbali kuta na vizingiti vinavyosababisha utengano kati ya watu. Anapenda kuwatangazia na kuwaonjesha watu Injili ya Furaha inayojikita katika huruma, msamaha na upendo wa Mungu usiokuwa kifani. Anataka kujenga uhusiano wa karibu na Familia ya Mungu kwa njia ya Kanisa. Licha ya makundi makubwa ya watu anayokutana nao, lakini bado anapenda kuzungumza na mtu mmoja mmoja kadiri ya shida na mahangaiko yake ya ndani. Yote haya ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia na wala si kwa ajili ya ”Papa kujitafutia ujiko”.

Papa Francisko Mwaka 2013 amechaguliwa na Jarida la TIME kuwa mtu mashuhuri wa Mwaka, hili ni jambo la kumshukuru Mungu, ikiwa kama wamelifahamu lengo la utume na maisha ya Kanisa na kwamba, Papa anapenda kuwaonjesha watu Injili ya Furaha, Huruma, Upendo na Msamaha unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Padre Lombardi anasema, ikiwa kama uchaguzi huu umezingatia vigezo hivi basi wana haki ya kumpatia Papa umaarufu huu, vinginevyo Baba Mtakatifu haguswi na ”Mapambio ya vyombo vya habari”.

Padre Lombardi anasema, waandishi wa habari wanapaswa kutambua dhamana na lengo la maisha na utume wa Kanisa. Wajitahidi kutafsiri matukio ya Kanisa si katika mwelekeo wa kisiasa au jukwaa la kiuchumi, vinginevyo watakosa dira na mwelekeo sahihi. Kanisa ni taasisi yenye asili mbili: asili ya Kimungu kwa vile imeanzishwa na Kristo na asili ya kibiniadamu kwa vile inongozwa na binadamu wenye karama na mapungufu yao. Kanisa linaendelea kupambana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wake kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Linafanya hivi kwa kuangalia: sheria, kanuni na maadili; umuhimu wa ushuhuda wa Kiinjili. Litatekeleza mikakati hii wala si kwa ajili ya kujiami dhidi ya mashambulizi ndani na nje ya Kanisa anasema Padre Federico Lombardi.

Mahojiano haya yamehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.