2014-03-12 15:10:50

Miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Marekani


Vatican na Serikali ya Marekani mwaka 2014 kwa pamoja wanaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 30 tangu Marekani ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican, hapo tarehe 10 Januari 1984. Rais mstaafu Ronald Reagan alitangaza mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Tarehe 8 Machi 1984, Serikali ya Marekani ikatuma Balozi wake wa kwanza mjini Vatican. Tarehe 26 Machi 1984 Mwenyeheri Yohane Paulo II akamteuwa wakati huo Askofu mkuu Pio Laghi kuwa ni Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Marekani.

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, si bure kwamba, Rais Barack Obama wa Marekani ameamua kutembelea Vatican ili kukutana na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 27 Machi 2014 wakati wa ziara yake ya kikazi Barani Ulaya Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Obama kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Viongozi hawa wawili wanakubaliana kimsingi katika agenda moja ya kupambana kufa na kupona na umaskini, ili kujenga mshikamano wa kidugu kati ya watu.

Katika kipindi cha miaka thelathini ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Marekani, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika majadiliano na mchango wa nchi hizi mbili katika medani za Jumuiya ya Kimataifa. Tangu mwaka 1984 hadi kufikia mwaka 2014, Marekani imekwishatuma Mabalozi wake kumi kama wawakilishi wa Serikali ya Marekani mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, tarehe 21 Oktoba 2013 Bwana Kenneth Francis Hackett, Balozi wa Marekani mjini Vatican aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Huyu ni mwanasiasa ambaye kwa miaka mingi amekuwa ni Makamu wa Rais wa Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, Mjumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Kuanzia mwaka 1994 hadi kufikia mwaka 2012 alikuwa pia ni mjumbe wa Shirika la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum. Ni matumaini ya Balozi Kenneth Francis Hackett kwamba, Marekani na Vatican wataendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa.








All the contents on this site are copyrighted ©.