Watu wanatamani kuona Bara la Afrika limesimikwa katika amani ya kweli!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, linaloundwa na Cape
Verde, Guinea Bissau, Mauritania na Senegal katika ujumbe baada ya maadhimisho ya
mkutano mkuu wa mwanzo wa Mwaka 2014 linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kuwa ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki na amani. Ni jukumu la kila mtu
kufanya tafakari ya kina ili kung'amua umuhimu wa kusimama kidete kujenga, kulinda
na kutetea haki na amani katika Jamii.
Maaskofu wanawataka waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashahidi wa amani Barani Afrika kwa kuzingatia kwanza
kabisa mafundisho yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu: ufukara, amani
na mazingira. Waamini hawana budi kuwa ni wadau na wajenzi wa haki, amani na upatanisho,
changamoto iliyotolewa na Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika.
Waamini wanahimizwa kujisomea na kuutafakari ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko
katika kipindi hiki cha Kwaresima, unaoongozwa na kauli mbiu "Maana mmejua neema ya
Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri,
ili kwamba, ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.
Maaskofu wanasema,
ili haki, amani na upatanisho viweze kushamiri Barani Afrika, kuna haja ya kuwashirikisha
wadau mbali mbali: viongozi wa Kanisa na Serikali; wanasiasa na wanaharakati ili kujikita
daima katika njia ya majadiliano na amani ili kuweza kufikia malengo mbali mbali wanayojiwekea.
Kwa wanasiasa wengi Barani Afrika, vita na kinzani za kijamii limekuwa ni suluhisho
la migogoro na changamoto za maisha, jambo ambalo kwa sasa haliwezi kamwe kukubalika.
Watu wajifunze kujadiliana na kutafuta suluhu ya migogoro kwa njia ya amani.
Maaskofu
wanawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho
ya Liturujia na Ibada mbali mbali za Kanisa ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na
mwanadamu kutakatifuzwa. Familia za Kikristo zijenge na kuimarisha utamaduni wa kusali
na kutafakari Neno la Mungu kwa pamoja, bila kusahau kumwombea Baba Mtakatifu Francisko
katika maisha na utume wake.
Maaskofu wanasema kipindi cha Kwaresima ni muda
muafaka uliokubalika kwa waamini: kufunga na kusali, kutafakari Neno la Mungu na kulimwilisha
katika matendo adili. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kuonjeshana upendo na mshikamano
wa kidugu kwa njia ya huduma makini. Waamini wanapofunga na kujinyima, sadaka yao
ilete mafao kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Waamini waguswe
na mahangaiko ya watu walioathirika kutokana na maafa asilia ndani na nje ya nchi
zao, tayari kuwasaidia kwa hali na mali.