2014-03-11 10:29:18

Sala ya Baba Yetu kiwe ni kioo cha maisha yako!


Sala ya Baba yetu ni sala tuliyofundishwa na Kristo mwenyewe. Huu ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu kwa wafuasi wake, kama yalivyo Mafundisho ya Heri za Mlimani na Amri kuu ya Mapendo kwa Mungu na jirani. Mitume wa Yesu waliwaona wanafunzi wa waalimu wengine wakifundishwa kusali na waalimu wao na ndipo wakamwomba Kristo wakisema “Bwana utufundishe nasi kusali kama Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake” (Lk 11: 1).

Kristo aliweka mbele yao sala hii yenye mistari mizito kabisa. Pengine sote tu hodari katika kuisali sala hii. Kila siku katika ibada ya misa, katika sala za familia na hata katika sala za jumuiya. Lakini nachelea kusema kuwa tunaweza kuwa tumebaki katika kiwango cha kukariri tu sala hiyo bila kuona na kuonja uzito wa maneno yake kiroho, bila kuona jinsi inavyopaswa kutuunganisha na kutuhusianisha na Mungu.

Katika moja ya makanisa niliyobahatika kusali hapa mjini Roma nilikutana na maandishi fulani ambayo nimeyaona kama yana chachu fulani katika kuitendetea haki sala ya Baba yetu na hatimaye kuwa na tija katika maisha yangu kiroho. Maandishi hayo kwa ujumla yananikataza kutamka kila neno la sala hii ya Baba yetu kama maisha yangu binafsi hayaakisi au hayamaanishi maneno ninayotamka. Napenda kuwashirikisha maneno hayo kama yalivyoandikwa na iwe fursa kwetu kutafakari vizuri uzuri na ukuu wa sala hii katika maisha ya kiroho.

•Usiseme “Baba” wakati hujiweki mbele yake kama mwana

•Usiseme “yetu” wakati unaishi katika ubinafsi wako

•Usiseme “uliye mbinguni” wakati daima unafikiri juu ya mambo ya ulimwengu tu

• Usiseme “ufalme wako uje” wakati daima umechanganywa na kupagaishwa na ufanisi wa malimwengu

•Usiseme “utakalo lifanyike duniani kama mbinguni” wakati unakuwa mgunu kutokubali wakati mapenzi ya Mungu yanapokuwa yanaumiza

• Usiseme “utupe leo mkate wetu wa kila siku” wakati hujali wengine walio wahitaji na wanaoteseka kwa njaa

• Usiseme “utusamehe dhambi zetu” wakati hauko katika hali ya kusamehe wengine

• Usiseme “usitutie kishawishini” wakati bado tunaendelea kufanya dhambi

• Usiseme “utuopoe maovuni” wakati wewe mwenyewe haupingani na uovu

• Na usiseme “amina” wakati huyatilii maanani mafundisho ya sala ya Baba yetu

Tutafakari katika kipindi hiki cha Kwaresma japo maneno haya na kuyaoanisha na maisha yetu ya kawaida kwani sala kama anavyosema Mtakatifu Yohane Krisostomi “haifungwi na ratiba maalum tu bali ni hali inayodumu mchana na usiku. Mtu anapaswa kumwuelekea Mungu sio tu pale anapomkumbuka kwa sala bali hata anapokuwa anafanya mambo mengine” Sala ni maisha.


NAWATAKIENI KWARESMA NJEMA.
Padre Joseph Mosha.
Jimbo kuu la Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.