Jacques Maritaini mfuasi mkuu wa Yesu na mtetezi wa ukweli!
Taasisi ya Kimataifa ya Jacques Maritain inaadhimisha Miaka 40 tangu ilipoanzishwa
na imekuwa na mchango mkubwa sana katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii kwa ujumla.
Ni Taasisi ambayo imejitahidi kumwilisha mawazo na mafundisho ya Mtakatifu Toma wa
Akwino katika kutetea utu na heshima ya binadamu katika kazi ya uumbaji. Maritain
alifanikiwa kutoa nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto zilizokuwa zinajitokeza
katika ulimwengu mamboleo.
Ni maneno yaliyosemwa hivi karibuni na Kardinali
Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika maadhimisho ya Miaka 40 tangu Taasisi
ya Kimataifa ya Jacques Maritaini ilipoanzishwa. Mafundisho yake yake yamewajengea
watu uwezo wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; bila
kutenganisha mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Akaonesha umuhimu wa utakatifu
wa maisha, jambo msingi katika ulimwengu wa utandawazi.
Jacques Maritain katika
baadhi ya kazi zake msingi anaonesha kwa kina na mapana kuhusu: Ukristo na Demokrasia,
jambo ambalo limelisaidia mchakato wa Kanisa kujihusisha na masuala ya kidemokrasia.
Alizungumzia kuhusu haki msingi za binadamu na sheria asilia; mambo ambayo aliyaandika
mara tu baada ya vita kuu ya Pili ya Dunia, alipokuwa uhamishoni huko Manhattan, ambako
wafungwa wengi kutoka Barani Ulaya, walimwona kuwa ni kiongozi wa maisha ya kiroho.
Aliandika
kitabu kinachoonesha uhusiano kati ya mtu na serikali; mambo yanayoonesha mabadiliko
makubwa yaliyojitokeza huko Ufaransa na Marekani, kuhusiana na haki msingi za binadamu
mintarafu mtazamo wa Kanisa. Huyu ni kati ya wasomi waliotayarisha mazungumzo kuhusu
Tamko la Haki Msingi za Binadamu kunako mwaka 1948. Kazi zote hizi anasema Kardinali
Parolin zimekuwa ni msaada mkubwa katika maandalizi ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Kutokana
na mchango wote huu, Kardinali Parolin ameipongeza Taasisi ya Kimataifa ya Jacque
Maritain kwa mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla
wake. Taasisi hii inaendelea kujadiliana na mabingwa katika Falsafa ili kuhuisha mchango
wa Jacque Maritain kwa kusoma alama za nyakati katika Karne ya ishirini na moja.
Kanisa
linaendelea kuonesha matumaini yake ya dhati katika mchango unaotolewa na Taaisi hii
kwa sasa na kwa siku za usoni. Kanisa linamshukuru Jacques Maritain kwa mawazo na
ushuhuda wake katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Kwa hakika anasema Kardinali
Pietro Parolin, Jacques Maritain ni mfuasi mkubwa wa Yesu na mtetezi wa ukweli.