2014-03-11 09:03:07

Balozi Francesco De Nittis amefariki dunia


Askofu mkuu Francesco De Nittis, aliyewahi kuwa Balozi wa Vatican katika nchi mbali mbali duniani, amefariki dunia tarehe 10 Machi 2014, huko Vieste, Foggia, nchini Italia. Alizaliwa tarehe 3 Julai 1933 na baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe 15 Julai 1956. Alifaulu kupata shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa.

Kunako Mwaka 1961 akajiunga na Utume wa Kidiplomasia mjini Vatican. Katika maisha yake alibahatika kufanya kazi za kitume nchini: Vietnam, Colombia, Nigeria, Syria, Marekani, India na Misri. Kunako tarehe 7 Machi 1981 aliteuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Papua New Guinea.

Mwaka 1985 akahamishiwa nchini El Salvador na Mwaka 1986 akapangiwa kazi nchini Honduras. Mwishoni, kunako Mwaka 1990 alihamishiwa nchini Uruguay na mwezi Agosti 1999 akang'atuka kutoka madarakani. Marehemu Askofu mkuu Francesco De Nittis anazika Jumanne tarehe 11 Machi 2014 majira ya jioni huko Vieste, Foggia.







All the contents on this site are copyrighted ©.