Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, amemwandikia ujumbe wa pongezi na
shukrani Professa Achim Buckenmaier mratibu wa Kongamano la Kimataifa linalonyika
kwenye Chuo Kikuu cha Jordan, Jimbo Katoliki Morogoro, Tanzania, ili kujifunza kwa
kina na mapana taalimungu kuhusu Yesu wa Nazareti, kama inavyochambuliwa na Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto XVI.
Hili kongamano la pili kufanyika Barani Afrika, baada
ya kongamano la kwanza kufanyika nchini Benin, Septemba 2013. Kongamano hili linaongozwa
na kauli mbiu " Wewe unatoka wapi?.
Lengo ni kuwajengea uwezo wanafunzi wa
vyuo vikuu Barani Afrika, kutambua taalimungu ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, kwa kuondoa vizingiti vinavyokwamisha watu kufahamu utajiri mkubwa
unaofumbatwa katika vitabu vilivyoandikwa na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita.
Kongamano hili limefunguliwa Jumatatu, tarehe 10 na linatarajiwa kuhitimishwa tarehe
12 Machi 2014. Linahudhuriwa na Maaskofu, Mapadre, watawa na waamini walei kutoka
ndani na nje ya Tanzania.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anasema, Yesu
Kristo ni kiini cha imani ya Kanisa, kumbe kukutana naye kunamwezesha mwamini kuweza
kukutana pia na Mwenyezi Mungu aliye hai. Hii ni changamoto kubwa kwa Mama Kanisa
kwani leo hii kuna upinzani juu ya uelewa wa Yesu wa Nazareti, jambo ambalo limemsukuma
kuandika vitabu juu ya Yesu wa Nazareti, ili kutoa nafasi kwa Waamini na watu wenye
mapenzi mema kumkaribia na hatimaye, kumfahamu Kristo.
Ni matumaini ya Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwamba, Kongamano hili la kimataifa litawawezesha
washiriki kukutana na hatimaye kutoka kifua mbele kutangaza kwa nguvu na moyo mkuu
Injili na kwamba, Yesu ni chemchemi ya maji ya uzima.