Wanawake tunzeni nidhamu ya matumizi ya fedha ya mkopo; vingenevyo "itakula kwako"!
Mke wa Waziri mkuu wa Tanzania, Mama Tunu Pinda amewaasa wanawake nchini Tanzania
wawe na nidhamu ya matumizi ya fedha za mikopo wanayochukua kwa ajili kuendeshea miradi
kama kweli wanataka kufanikiwa na kutimiza malengo waliyojiwekea.
Ametoa wito
huo Jumapili, Machi 9, 2014 wakati akifungua Tamasha la Wanawake (Women Dialogue Front
-2014) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika kwenye
hoteli ya JB Belmont, jijini Mwanza.
Akizungumza na washiriki wa tamasha hilo
lililoandaliwa na asasi ya Mikaela Women Empowerment Initiatives ya jijini Mwanza,
Mama Tunu Pinda alisema: “Japokuwa kwenye ujasiriamali kuna changamoto nyingi lakini
kuna wenzenu walioweza kufanikiwa. Hivyo nina imani kubwa kuwa nanyi mtafanikiwa,
ili mradi muwe na nia ya dhati katika kutekeleza malengo mliyojiwekea.”
Akisisisitiza
haja ya kuwa na uthubutu kwenye ujasiriamali, Mama Pinda alisema: “...Lakini niwatake
wanawake wenzangu kuwa wajasiri na wenye kuthubutu na kuwa na mipango inayotekelezeka
ili muweze kutimiza ndoto zenu.”
“Sisi wanawake tunapaswa kujitambua na kuzitumia
fursa zilizopo ambazo kama tutazizingatia ipasavyo, zitatusaidia kujenga ustawi wa
maisha yetu na jamii kwa maana kukua kwa uchumi kwa mwanamke ni kukua kwa uchumi wa
familia, kaya na jamii pia.”
Aliwataka akinamama nchini watumie vizuri fursa
za mikopo na wawe waaminifu katika kutumia na kurejesha mikopo hiyo. “Tumieni fursa
za mikopo kwa kukopa kwa uaminifu, kimkakati na kwa malengo ili kuendeleza miradi
yenu na jamii kwa ujumla,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mama Tunu Pinda alisema
ana imani kwamba taasisi za fedha zitatoa kipaumbele katika kutoa mikopo yenye riba
na masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali ili kuleta maendeleo ya kweli miongoni
mwa akinamama.
Akizungumzia kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU)
katika jiji la Mwanza, Mama Tunu Pinda aliwataka wanawake hao kuwa makini kwa kujikinga
na maambukizi mapya ya VVU kwa vile Jiji hilo lina kiwango cha juu cha maambukizi
ya ugonjwa huo.
“Utafiti unaonyesha kwamba Jiji la Mwanza linashika nafasi
ya 11 kati ya mikoa 30 ya Tanzania sawa na asilimia 4.2. Na kati ya hao wanawake ndio
wanaongoza kuliko wanaume. Hii inasababishwa na wengi wao kukosa uelewa wa kutosha
katika masuala ya afya ya UKIMWI pamoja na kukosekana kwa usawa wa kijamii, kiuchumi
na unyanyasaji wa wanawake na wasichana walio ndani na nje ya mahusiano,” alisema
Mama Pinda.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha ni jinsi gani mwanamke anaweza
akuchukua tahadhari mapema na ya haraka katika kupambana na ugonjwa huo hatari. “Lakini
pia mimi niseme tu, mwanamke una nafasi kubwa sana katika kupambana na ugonjwa huu
kwa kuchukua hatua za dhati na za makusudi katika kujikinga wewe na familia yako kama
mwanamke unayejitambua,” aliongeza.
Mapema, akisoma risala yao mbele ya mgeni
rasmi, Mwenyekiti wa asasi ya Mikaela Women Empowerment Initiatives, Bibi Edith Mudogo
alisema asasi hiyo inayojishughulisha na utoaji wa mikopo midogodogo kwa akinamama,
ina jumla ya wanachama 102 ambao wanajihusisha na biashara, kilimo na ufugaji.
Alisema
wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo kunyimwa mikopo na taasisi za kifedha kutokana
na masharti yasiyo rafiki yaliyowekwa na taasisi hizo; ukosefu wa fedha unaowanyima
fursa ya kuwafikia wanawake waishio vijijini na usumbufu unaopatikana katika kukopa
na kurejesha mikopo ingawa ni kwa kiasi kidogo.