2014-03-10 09:10:37

Usijibishane na Shetani, atakubwaga chini! Silaha pekee ni Neno la Mungu!


Liturujia ya Neno la Mungu , Jumapili ya kwanza ya kipindi cha Kwaresima, tarehe 9 Machi 2014, inaonesha jinsi Yesu alivyojaribiwa na Shetani baada ya kufunga kwa siku arobaini Jangwani na kabla ya kuanza utume wake hadharani. Shetani alitaka kumng'oa Yesu kutoka katika mpango wa Mungu unaofumbatwa katika sadaka kama kielelezo cha hali ya juu cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu na badala yake achukue njia ya mkato, lakini Yesu anamshinda kwa kutumia Maandiko Matakatifu.

Shetani alitaka kumwondolea Yesu Fumbo la Msalaba kwa kumwahidia ustawi wa kiuchumi na miujiza ikiwa kama atamsujudia. Hivi ni vishawishi kuhusu, Yesu Kristo Mwana wa Mungu, kugeuza mawe ili yawe mkate; Anaambiwa kama kweli ni Mwana wa Mungu ajirushe chini kutoka kwenye mnara na tatu Shetani anamtaka Yesu amsujudie. Hivi ni vishawishi vinavyofahamika kwa Wakristo.

Ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili ya kwanza ya Kwaresima, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petrio mjini Vatican. Yesu aliweza kushinda vishawishi vyote hivi akawa imara katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha yake, akashinda vishawishi vyote hivi kwa njia ya Neno la Mungu. Yesu hakufanya majadiliano na Shetani bali anatumia nguvu ya Neno la Mungu inayokoa.

Yesu anawakumbusha wafuasi wake kwamba, mtu hawezi kuishi kwa mkate peke yake, bali kwa kila Neno litokalo katika kinywa cha Bwana. Neno la Mungu ni silaha madhubuti katika kupambana na malimwengu pamoja na kukuza njaa ya kutaka kukutana na upendo wa Mwenyezi Mungu ambaye ni mkweli, mwema na mzuri.

Yesu anawaalika Wakristo kutokumjaribu Mungu, kwani njia ya imani ina mapito mengi lakini inarutubishwa kwa uvumilivu na subira inayovuta heri. Waamini wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayepaswa kuabudiwa, changamoto ya kusimika maisha katika mambo msingi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maneno haya ya Yesu yamemwilishwa katika maisha na matendo yake, kielelezo cha hali cha juu ya uaminifu kwa Mungu katika utekelezaji wa Mpango wa Mungu, kazi aliyoitekeleza kwa kipindi cha miaka mitatu, akafunga ukurasa huu kwa kukumbatia Fumbo la Msalaba, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini katika kipindi hiki cha Kwaresima kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kujipima kikamilifu kwa Neno la Mungu, pamoja na kujitahidi kuishi ahadi za Ubatizo kwa kumkataa Shetani na mambo yake yote. Ni mwaliko wa kutembea katika hija ya Mungu, ili baada ya Mfungo wa Kwaresima waweze kusherekea Pasaka ya Bwana.

Kipindi cha Kwaresima kisaidie kutekeleza mikakati ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani. Baba Mtakatifu mwishoni, amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika Sala wakati huu wa Mafungo ya Maisha ya Kiroho pamoja na Wasaidizi wake wa Karibu.







All the contents on this site are copyrighted ©.