2014-03-10 10:48:01

Umuhimu wa sala katika maisha ya ndoa na familia!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tena katika kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani. Tukiwa ndani ya Kipindi cha Kwaresma, tunaendelea kuitikia mwito wa kumrudia Mungu atualikaye akisema “nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote kwa maana mimi ni mwenye rehema na upole”. RealAudioMP3

Katika kipindi hiki ambapo tunashughulikia kwa namna ya pekee zaidi wongofu wa mwenendo wetu, tunakiri udhaifu wetu mbele za Mungu na mbele za wanadamu wenzetu, na hivyo kwa roho ya unyenyekevu toba na majuto ya kweli, tunataka kurekebisha yale yote yanayotuweka mbali na Mungu wetu na pia yanayotutenga na wanadamu wenzetu. Kipindi cha Kwaresma ni kipindi cha Kusali sana, kutoa sadaka na kufunga.

Mpendwa msikilizaji, kwa siku ya leo, tuone kwa ufupi juu ya tunu hii ya sala katika maisha yetu ya kila siku. Sisi sote, kila mmoja kwa nafsi yake, anautafakari na kuukiri wema na ukuu wa Mungu. Lakini kwa udhaifu wetu sisi wenyewe na kwa hila za yule mwovu, hatujafaulu sana kumpa Mungu utukufu. Daima tunamsahau Mungu, ila Mungu hatusahau kamwe, anasikitika pale tunapomkimbia kwa maisha yetu ya dhambi, na ndiyo maana anatuita akisema “nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote”. Sio tunarudi kwa mashakamashaka au tunamrudia kwa kujaribisha au kukejeli, ila asema nirudieni kwa mioyo yenu yote.

Katika kipindi hiki cha Kwaresma, tunataka kuongea na Mungu zaidi, kutafakari wema wake wa kila siku na kuukiri ukuu na uweza wake kwa maneno na matendo ya maishani mwetu. Tunafanya hivyo kwa njia ya sala na tafakari. Lakini sala yetu ili ipate kibali mbele za Mungu lazima iwe nadhifu na kunjufu. Sala nadhifu ni ile ambayo ina nia njema na inaendana na hulka ya Mungu mwenyewe, yaani upendo, wema, upole huruma, uaminifu na uvumilivu. Hatuwezi kumkejeli Mungu kwa kumwomba atusaidie tufanikiwe katika maovu, au kumwomba awatendee maovu wenzetu, hiyo siyo hulka ya Mungu. Sala kunjufu ni sala yenye nguvu ya kinabii, ni sala inayompa Mungu Utukufu na kumtakatifuza mwanadamu. Tunaalikwa kusali kwa nidhamu ya akili, mwili na roho.

Bwana asema “tena msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia ili waonekane na watu. Amini nawaambia wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukisha kufunga mlango wako usali mbele ya baba yako aliye sirini atakutuza” (Mt. 6-6).
Neno hili litukumbushe sote juu ya unadhifu wa sala zetu. Tunaalikwa kukwepa kabisa kishawishi cha nyakati zetu hizi cha kupenda kusali kwa matamasha na TV, ili tuonekane na watu na kuyapendezesha macho ya watu badala ya kuupendezesha moyo wa Mungu. Siku zetu hizi kuna kishawishi cha kusali kwa kelele nyingi za viigizo, na kurukaruka kwingi, badala ya kusali kwa ibada na tafakari. Kusali kwa aina hiyo hakuna thawabu machoni pa Bwana. Sala ya kweli, hutoka katika vilindi vya mioyo yetu, nayo hufanyika katika utulivu. Mungu wetu, sio Mungu wa kelele.

Na tena, Neno la Mungu latukumbusha kusali kila wakati. Tunakatazwa kusali kwa matukio au kwa msimu tu. Neno anasema “Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu (Ef. 6:18) na pengine asema, salini kila wakati na kushukuru katika kila jambo (1Thes 5:17-18).

Neno hili ‘salini kila wakati’, na likae mioyoni mwetu kipindi hiki cha kwaresma na nyakati zote. Mpendwa msilikizaji, ikumbukwe kwamba Mungu wetu sio Mungu wa matatizo. Huweza kutokea kwa baadhi yetu, tukawa watu wa kusali pale tu tupatwapo na matatizo. Yaani matatizo yanakuwa ndiyo teke la kutukumbusha juu ya uwepo wa Mungu na umuhimu wa sala. Tukipatwa na shida, ndio tunamkumbuka Mungu. Katika mazingira hayo, hiyo inakuwa sio sala bali ni kelele za kumsimulia Mungu matatizo yetu. Imani ya matatizo haina thawabu mbele za Bwana.

Mpendwa msikilizaji, sasa tuielekeze tafakari yetu katika familia zetu. Uhalisia unashuhudia kwamba, familia nyingi zimeacha kuwa shule ya sala. Baba Mtakatifu Francisco mara nyingi ameonesha sikitiko juu ya ukosefu wa sala katika familia, ambapo wazazi na wote wenye dhamana ya malezi, wamesahau kuwafundisha watoto sala, hata ishara ya msalaba tu inakosekana. Dini gani hiyo isiyokuwa na sala? Ni muamini wa aina gani huyo asuifahamu sala za dini yake? Kwaresma hii tukumbushwe tena, familia ni shule ya sala. Tuwafundishe watoto wetu KUSALI. Nasi sote tujibidishe kufahamu sala na namna ya kusali.

Familia iwe ni kanisa linalosali! Ukweli unashuhudia kwamba, familia nyingi zimeacha kusali pamoja. Hatuwezi kusingizia sana utandawazi, bali namna yetu ya kupima mambo kwa vipaumbele. Kuna mambo mengi sana ambayo familia hufanya pamoja, lakini ugonjwa mbaya wa kiroho umeingia katika familia nyingi, hawawezi kusali pamoja tena. Tunakumbushwa wanafamilia, tukutanike pamoja, tuliite jina la Bwana pamoja, tulitaje jina la Mungu wetu kwa pamoja (Zab 34:1-7). Kulitaja jina la Bwana kwa pamoja kama familia kuna maana na uzito wake.

Kuwa na utengano katika sala, yule mwovu anaweza kukujaribu vibaya mno, ndipo hapo mtu unapopata kishawishi cha kumwombea mabaya mwenzako (mama unamwombea baba apatwe na mabaya, na baba unamwombea mama maangamizi), lakini mngesali kwa pamoja, nyote mngetamka, utupe leo mkate wetu wa kila siku.

Kipindi hiki cha kwaresma tunataka kupiga vita roho ya uvivu katika sala inayoelekea kuota mizizi mirefu sana katika familia zetu. Tunataka pia kupiga vita roho ya kuionea aibu sala. Wengi wanaona aibu kusali. Imani yetu bila sala, itanyauka na kufa kabisa na mwovu anapata nguvu ya kutupepeta apendavyo.

Sala inatupatia nguvu ya ndani ya kustahimili mitikisiko ya maisha. Sala inatuliza akili zetu wakati wa mahangaiko. Sala inatupatia ujasiri wa ajabu hata mbele ya matatizo makubwa. Sala inatupatia amani hata kama tunapita motoni na majini. Sala ni mlango wa tumaini jema daima. Sala ni afya ya roho na ya mwili. Tusali daima kwani kusali ni heri.

Kutoka katika studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.