Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasadizi wake wa karibu, Jumapili jioni waliondoka
wote kwa Mabus mawili kuelekea mjini Arricia, nje kidogo ya Roma kwa ajili ya mafungo
ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya mchakato wa kujitakasa. Mafungo haya yanaongozwa
na Monsinyo Angelo de Donatis, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Marko, Jimbo kuu la
Roma.
Hiki ni kipindi
cha kufunga ili kuzuia vilema vya kibinadamu, tayari kuinua mioyo ili kuomba neema
na nguvu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Hiki ni kipindi cha kujinyima
ili kuwaondolea kiburi kwa kutambua kwamba, kama binadamu wanaweza kuogelea katika
dhambi, hivyo wanahitaji kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.
Mafungo
haya yameanza rasmi, Jumapili tarehe 9 Machi na yanatarajiwa kukamilika Ijumaa tarehe
14 asubuhi. Hii ni nafasi maalum kwa Baba Mtakatifu Francisko kuweza kufanya tafakari
ya kina, mwaka mmojua tangu alipoteuliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, hapo tarehe 13
Machi 2014. Mafungo haya yanasheheni: Ibada ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Tafakari
pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; mambo msingi katika mafungo.
Papa
Paulo wa sita, aliwahi kusema kwamba, mafungo ya maisha ya kiroho kwa Wakatoliki
yanakwenda sanjari na Sakramenti ya Upatanisho kwa Mungu na jirani, kama njia ya kujipatia
neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kusaidia kuwaongoza watu wake wanaopambana
na ubinadamu ulioathiriwa kutokana na dhambi ya asili; ni jitihada za kuomba huruma
ya Mungu ili aweze kuponya madonda ya ubinadamu pamoja na kuimarisha malengo na matumaini
ya watoto wake siku kwa siku.
Mafungo yanawasaidia waamini kuwa na moyo mpya
unaojikita katika neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kushinda vilema na
udhaifu wa kibinadamu. Waamini wanaalikwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, kila
wakati wanachunguza dhamiri zao mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kushukuru, kusifu na
kumwabudu Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo.
Ni wakati wa kuchunguza
ahadi ambazo mwamini ameziweka mbele ya Mungu na jirani zake, ili kuangalia kama kweli
amejitahidi kuzitekeleza au amekwama. Mafungo ya kiroho, yawe ni fursa kwa waamini
kuthamini utendaji wa majukumu yao kwa Mungu na mbele ya Jamii; wawe tayari kubadilisha
na kujipanga upya kwa mambo ambayo hayaendi kwa kuamini kwamba, bado kuna uwezekano
wa kutenda vizuri zaidi badala ya mtu kujikatia tamaa.
Baba Mtakatifu Francisko
katika mahojiano maalum na Gazeti la “Corriere della Sera” linalochapishwa kila siku
nchini Italia. Anasema, alipokuja mjini Roma kushiriki katika mkutano wa Baraza la
Makardinali kwa ajili ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hakuwa na wazo kwamba,
angeweza kuchaguliwa na hivyo kulazimika kuhama kutoka Argentina hadi mjini Vatican.
Anasema ameanza kutekeleza utume wake wa kuliongoza Kanisa Katoliki kwa kutekeleza
kwanza kabisa ushauri uliokuwa umetolewa na Makardinali katika vikao vyao elekezi
kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ameendelea kumtegemea Mwenyezi Mungu
katika utendaji wa shughuli zake za kichungaji.
Baba Mtakatifu anasema, kati
ya mambo msingi yaliyokaziwa na Makardinali ni huduma ya maisha ya kiroho kwa wasaidizi
wake wa karibu waliopewa dhamana katika kusimamia na kuongoza Mabaraza ya Kipapa na
Taasisi mbali mbali zinazomwezesha kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro.
Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, kila mwezi wanapata fursa ya
kujitenga na shughuli za kila siku, ili kufanya mafungo ya maisha ya kiroho. Kila
mtu anayo haki ya kupata siku tano za mafungo ya kiroho. Mafungo ya Kipindi cha Kwaresima
kwa wakati huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa maazimio ya Mikutano Elekezi ya Makardinali
iliyofanyika kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu
anasema katika mahojiano hayo kwamba, Mafungo ya maisha ya kiroho yanamwezesha mwamini
kujitenga na marafiki, mazingira na shughuli za kawaida, ili kuweza kupata muda wa
kusali, kutafakari na kufanya maamuzi ya kina katika maisha na utume wa Kanisa. Mafungo
yana faida kubwa zifuatazo: kwanza kabisa yanamwezesha mwamini kupata muda zaidi wa
kumshuruku, kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu pamoja na kuendelea kujifunza kwa
njia ya ukimya kutoka kwake.
Pili ni nafasi ya kutuliza mawazo, ili hatimaye,
kujenga na kuimarisha utashi wa kupenda kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa moyo na akili
zako zote. Tatu katika mazingira ya upweke chanya, mwamini anapata nafasi kubwa zaidi
ya kushikamana na Mwenyezi Mungu pamoja na Yesu Kristo, ili kujichotea neema na nguvu
ya kutekeleza nyajibu mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa.