Kwaresima kiwe ni kipindi cha kusaidia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa, akizungumza na Waandishi
wa Habari waliokuwa wamefurika mjini Vatican kufuatilia mchakato wa uchaguzi wa Khalifa
wa Mtakatifu Petro, alisema amechagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assis, kwani
alikuwa ni mtu fukara, mpenda amani na mazingira.
Hii ndiyo
changamoto inayofanyiwa kazi katika Kipindi hiki cha Kwaresima na Baraza la Maaskofu
Katoliki India, kuhakikisha kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanashirikishwa
katika kulinda na kutunza mazingira. Waamini wanahimizwa kupunguza uzalishaji wa hewa
ya ukaa kama sehemu ya ushiriki wao katika kulinda na kuendeleza kazi ya Uumbaji ambayo
Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu ili aweze kutunza kwa ajili yake na kwa kizazi
kijacho.
Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India
anasema, Kipindi cha Kwaresima: muda wa kusali na kufunga, kutafakari na kumwilisha
Neno la Mungu kama kielelezo cha imani tendaji katika matendo ya huruma, iwe ni fursa
ya kujenga na kuimarisha uhusiano mwema kati ya mwanadamu na Muumba wake pamoja na
mazingira.
Uharibifu wa mazingira ni kati ya changamoto kubwa zinazowakabili
wananchi wa India kwa sasa. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya viwanda na uzalishaji;
mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira. Kanisa kwa nyakati zote
limekuwa ni mdau mkubwa wa utunzaji wa mazingira, kumbe halitaweza kukaa pembeni na
kuona mazingira yakiharibiwa.
Jimbo kuu la Bombay, India, hivi karibuni lilianzisha
Idara ya Mazingira ili kuweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi
pamoja na athari zake. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, Idara ya mazingira inaendelea
kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema umuhimu wa kulinda na kutunza
mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi na ustawi wa wananchi wote wa India na dunia
katika ujumla wake.