Hija ya Papa Francisko nchini Korea ilete matumaini ya upatanisho wa kweli!
Kardinali Andrew Yeom Soo-jung, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini,
amepokea taarifa rasmi ya hija ya kitume itakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko
nchini humo kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya sita ya Vijana Barani Asia kwa moyo
mkuu na wa shukrani.
Anapenda kuchukua fursa tangu wakati huu kumkaribisha
Baba Mtakatifu nchini Korea kwa mikono miwili, ili kuweza kukutana, kuzungumza na
kusali na vijana kutoka Barani Asia, watakaokuwa wanakusanyika kwenye Jimbo Katoliki
la Dejeon, bila kuwasahau waamini na watu wenye mapenzi mema wanaoendelea kuonesha
hamu ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko.
Kardinali Yeom Soo-jung anasema,
wakati wa Ibada ya Misa ya shukrani baada ya kusimikwa kuwa Makardinali, Baba Mtakatifu
alimshirikisha upendo wake mkuu kwa wananchi wa Korea na kwamba, sasa ameamua kufanya
hija ya kitume nchini mwao, jambo ambalo linaonesha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi
Mungu kwa ajili ya wananchi wa Korea.
Ni matumaini ya wananchi wa Korea kwamba,
hija ya Baba Mtakatifu itasaidia kukoleza mchakato wa upatanisho kati ya Korea ya
Kusini na Kaskazini sanjari na Bara zima la Asia kusikia dhamana ya kulinda na kujenga
amani, upendo na mshikamano kati ya watu.
Hija hii iwe ni fursa kwa maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kuwa na matumaini mapya katika maisha na
vipaumbele vyao.