Yaliyojiri katika mazungumzo kati ya Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni
na Papa Francisko
Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Ijumaa tarehe
7 Machi 2014 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika
mazungumzo yake na Baba Mtakatifu Dr. Tveit amekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha
majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo ili kujenga na kudumisha umoja.
Dr Tveit amempongeza
Baba Mtakatifu Francisko kwa juhudi zake katika kuombea amani nchini Syria, changamoto
na mwaliko kwa Makanisa kusimama kidete kujenga uchumi unaojimbanua katika misingi
ya haki. Itakumbukwa kwamba, Baraza la Makanisa Ulimwenguni lina jumla ya Makanisa
wanachama 345 yaliyoenea katika nchi zaidi ya 110.
Katibu mkuu wa Baraza la
Makanisa Ulimwenguni alikuwa mjini Vatican kwa mwaliko wa Baraza la Kipapa linalohamasisha
Umoja wa Wakristo. Anakiri kwamba, katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo,
Mwenyezi Mungu anaendelea kufungua njia za majadiliano ya kiekumene, ili kwa pamoja
Wakristo waweze kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya huduma
makini hasa zaidi miongoni mwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na
hali yao ya maisha. Wakristo wahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kushikamana
ili kuweza kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha.
Kwa upande wake,
Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, amefurahishwa kwa namna ya
pekee na mwaliko na changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika mshikamano
na ushuhhuda wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upendo kati ya Wakristo na Walimwenguni
katika ujumla wao. Injili inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa Wakristo.
Dr.
Tveit amezungumzia Nyaraka mbali mbali zilizokwishawahi kutolewa na Baraza la Makanisa
Ulimwenguni, kwa kukazia umuhimu wa Kanisa kuwa ni mhudumu; Kanisa ambalo linapaswa
kuwa ni nyumba ya wote, ili kuwashirikisha wengine wote Habari Njema ya Wokovu.
Dr.
Tveit amezungumzia kuhusu hija ya kichungaji itakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko
kwenye Nchi Takatifu, ili kukutana, kusali na kuzungumza na Patriaki Bartolomeo wa
kwanza wa Costantinopoli. Amempongeza Baba Mtakatifu kwa ujasiri wake unaoonesha jinsi
ambavyo anakereketwa na ukosefu wa amani na utulivu huko Mashariki ya Kati.
Ni
matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, hija hii ya kichungaji ya Baba
Mtakatifu itasaidia kukoleza mchakato wa amani, utulivu na upatanisho huko Mashariki
ya Kati. Kwa miaka mingi Baraza la Makanisa Ulimwenguni limesali na kujielekeza katika
ujenzi wa misingi ya haki na amani huko Nchi Takatifu.
Dr. Olav Fykse Tveit
anakazia kwamba, dini na imani vina mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao
ya wengi. Haki, amani na upatanisho ni mambo yanayowezekana kwani ni tunu msingi za
maisha ya dini mbali mbali duniani. Israeli na Palestina ni nchi mbili zinazoweza
kuishi kwa amani na utulivu kwa kuheshimiana.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni
linaendelea kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika
hija ya haki na amani, changamoto kubwa iliyotolewa na wajumbe wa mkutano mkuu wa
Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliohitimishwa kunako Mwaka 2013 huko Busan, Korea
ya Kusini. Mabadiliko ya tabia nchi ni kati ya masuala ambayo pia yanapaswa kufanyiwa
kazi na Wakristo katika umoja wao, sanjari na ujenzi wa mkakati wa uchumi wa haki.
Ikiwa kama tunu hizi msingi zitashindwa kumwilishwa katika vipaumbele vya mwanadamu,
watakaoendelea kuumia ni maskini wanaoishi katika nchi maskini zaidi duniani.
Baraza
la Makanisa Ulimwenguni linawaalika wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanaibua
mbinu mkakati wa kulinda na kutunza mazingira. Dr. Tveit anasema, ameridhika sana
na mazungumzo aliyofanya na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji
mjini Vatican.