Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani kutembelea Sudan ya Kusini
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani anatarajiwa kufanya
hija ya kichungaji nchini Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 18 Machi hadi tarehe 23 Machi
2014 kama kielelezo cha mshikamano wa upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa
wananchi wa Sudan ya Kusini wanaokabiliwa na maafa makubwa kwa sasa.
Taarifa
kutoka katika Idara ya Habari ya Shirikisho la Maaskofu Afrika Mashariki na Kati,
AMECEA inaonesha kwamba, habari hizi zimetolewa na Askofu mkuu Paolino Lukudu Loro
wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini. Akiwa nchini humo, Kardinli Turkson ataadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutabaruku Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yosefu,
Jimbo kuu la Juba. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, tukio hili linatarajiwa kufanyika
hapo tarehe 19 Machi 2014.
Alhamisi tarehe 20 Machi, Kardinali Turkson anatarajiwa
kukutana na kuzungumza na Taifa la Mungu nchini Sudan ya Kusini. Ijumaa tarehe 21
Machi atakutana na kuzungumza na Rais Salva Kiir Mayardit pamoja na viongozi wengine
wa Makanisa nchini Sudan ya Kusini.
Hija hii ya kichungaji inayofanywa na
Kardinali Turkson nchini Sudan ya Kusini, itakamilika kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Theresa, Kator na baadaye, Jumatatu, tarehe 23 Machi,
Kardinali Turkson atarejea mjini Vatican kuendelea na shughuli zake za kichungaji.