Dhamana na wajibu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume ndani ya Kanisa
Hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko alikutana na kuzungumza na Wakuu wa Mashirika
ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa waliokuwa wamehitimisha maadhimisho ya mkutano
mkuu wa 82 uliofanyika mjini Roma.
Ni mkutano
uliojikita katika majadiliano ya kina kati ya Baba Mtakatifu na Wakuu wa Mashirika
katika hali ya kidugu, kwa kutambua kwamba, watawa kama sehemu ya binadamu wengine
wote ni Wadhambi na Manabii katika ulimwengu mamboleo.
Baba Mtakatifu akizungumzia
kuhusu utambulisho na utume wa watawa anasema, wanapaswa kuishi maisha yanayotoa ushuhuda
wenye mvuto na mashiko unaojikita katika maisha ya kujisadaka; upendo na ukarimu kwa
jirani, lakini zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Watawa
wawe makini ili wasije wakamezwa na malimwengu kwani hapa watalichefua Kanisa!
Ushuhuda
adili na amini wa maisha ya kitawa na kazi za kitume ulete harufu nzuri yenye mvuto
kwa watu kulipenda na kulithamini Kanisa; kwa kujitosa kinaganaga kuleta mabadiliko
yanayokusudiwa na Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Ili kufanikisha azma hii,
watawa hawana budi kwanza kabisa: kujikita katika maisha na tunu msingi za Kiinjili,
ingawa huu ni mwaliko na changamoto kwa Familia yote ya Mungu.
Watawa wawe
ni watu safi, wakweli na wa wazi kwa kutambua kwamba, ulimwenguni kuna uwepo wa neema
na dhambi. Hakuna mtu mkamilifu hapa duniani, kila mtu ana kasoro na mapungufu yake
na hii ni sehemu ya ubinadamu. Kwa kutambua kasoro na karama zao, watawa wanaweza
kujitosa kifua mbele kushuhudia Kweli za Kiinjili bila ya kuwa na makunyanzi.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaalika watawa kuondokana na misimamo mikali ya maisha ya kitawa
na badala yake wawe ni njia na mwanga kwa siku za usoni. Watawa wawe tayari kujifunza
mahangaiko ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili waweze kuwashirikisha
upendo na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watawa wajikite
katika maisha ya Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, tayari kuwaonjesha jirani
zao Injili ya Furaha.
Baba Mtakatifu anasema kipaumbele cha kwanza kwa Watawa
katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuhakikisha kwamba, wanajitosa
kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na kushiriki katika mchakato wa
ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani kama walivyofanya watawa wengi katika utume na maisha
ya Kanisa. Watawa wawe waaminifu kwa karama za Mashirika yao; wajitahidi kuwa wagunduzi
na tayari kusoma alama za nyakati kama wanavyokazia Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican.
Baba Mtakatifu anasema, takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa
ya miito ya kitawa Barani Asia na Afrika, jambo linalotoa changamoto nyingi katika
mchakato wa utamadunisho wa karama za Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Mashirika
yanapaswa kuwa makini katika uteuzi wa vijana wanaoomba kujiunga na mashirika yao.
Waangalie na kukoleza majadiliano ya kidini sanjari na kuangalia uwakilishi wa Mashirika
ya Kitawa katika taasisi zinazoongozwa na kusimamiwa na Serikali mbali mbali.
Baba
Mtakatifu anawahimiza watawa wasihofu kukufanya makosa katika kumwilisha karama ya
mashirika yao kwani hii ni sehemu ya ubinadamu; jambo la msingi ni kuomba msamaha
tayari kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza ili kusonga mbele kwa imani na matumaini
zaidi. Vijana wanaoomba kujiunga na maisha ya kitawa hawana budi kulelewa vyema kwa
kuangalia tamaduni na mazingira ya watu husika, tayari kutamadunisha karama ya shirika
husika. Hapa watawa watambue kwamba, utamadunisho wa karama ni jambo muhimu sana katika
maisha na ustawi wa Mashirika husika.
Baba Mtakatifu ameonya kuhusiana na biashara
haramu ya binadamu inayoweza kufanywa na Mashirika ya Kitawa yanayotafuta vijana wa
kujiunga na mashirika haya kwa udi na uvumba kutoka katika Nchi changa zaidi duniani
na kuwapeleka Ulaya. Onyo hili liliwahi kutolewa na Maaskofu kutoka Ufilippini wakati
wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maisha ya Kuwekwa wakfu iliyoadhimishwa kunako Mwaka 1994.
Baba
Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, wito wa “Ubruda” bado haujafahamika na kupokelewa
kwa moyo chanya na waamini wengi. Hii ndiyo maana wito huu unaendelea kufifia siku
hadi siku ndani ya Kanisa. Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume,
lilipewa dhamana ya kuangalia kwa kina na mapana changamoto zinazojitokeza katika
maisha ya kitawa; wajitahidi kusoma alama za nyakati na kujitahidi kufahamu Mwenyezi
Mungu anataka nini kwa Kanisa?
Baba Mtakatifu Francisko anasema malezi ni jambo
la muhimu sana, linalohitaji: hekima na busara; upendo na subira; sala na bidii. Ikumbukwe
kwamba, nyumba za malezi si “Kituo cha Polisi”. Vijana wenye nia ya kutaka kuwa watawa
hawana budi kufundwa: Kiroho, kiakili na kiutu; Maisha ya Kijumuiya na kazi za kitume;
utamadunisho na majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi na kwamba, unafiki
ni sumu ya maisha ya kitawa. Vijana wapewe fursa na kusaidiwa kutafakari kuhusu maisha
na wito wao, ili hatimaye, waweze kutoa uamuzi wenye busara.
Watu wa Mungu
wajengewe ukomavu na uhuru katika maisha yao ya Kikristo. Seminari na nyumba za malezi,
ziwe ni jukwaa la majadiliano ya kina, ukweli na uwazi bila woga. Walezi wajitahidi
kufahamu lugha inayotumiwa na vijana ili waweze kuwasiliana vyema zaidi kutoka katika
undani wa mioyo yao na wala si katika hali ya kujisikia tu! Malezi yalenge ukomavu
wa mtu mzima na hatima ya maisha yake. Lengo ni kuhakikisha kwamba, watawa wanakuwa
kweli ni mashahidi wa Kristo Mfufuka. Vijana watambue kwamba, wanaandaliwa kuwa ni
viongozi wakuu wa Familia ya Mungu na wala si mameneja katika kampuni Fulani.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kuna changamoto kubwa katika malezi, yaani tatizo
la kumpokea Mseminari aliyefukuzwa kutoka Shirika au Jimbo Fulani na kumpatia tena
nafasi ya kuendelea na majiundo yake ya maisha ya kitawa. Kanisa linatambua kwamba,
watoto wake si wakamilifu, ni wadhambi, lakini Kanisa haliwezi kukubali watoto wake
wawe mafisadi! Hii inaonesha kwamba, malezi yanakabiliwa na changamoto nyingi, hasa
baada ya kuibuka kashfa za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa.
Watawa
wanapaswa kujifunza kuishi kwa pamoja kama ndugu katika Kristo kwa kujitahidi kufisha
ubinafsi na kasoro zao ili kuondokana na kinzani pamoja na migogoro isiyokuwa ya lazima.
Masilahi ya Jumuiya hayana budi kupewa kipaumbele cha kwanza, kwani maisha na mshikamano
wa Kijumuiya una nguvu ya kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na utume.
Kinzani na misigano ni mambo ya kawaida katika maisha ya mwanadamu. Mambo
haya yanapojitokeza, yajadiliwe kwa kina na mapana kwa kuzingatia: upendo, ukweli
na uwazi, tayari kuendeleza umoja na mshikamano wa Jumuiya. Watawa watambue kwamba,
umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Pale kinzani zinapojitokeza, wanajumuiya watafute
ushauri wa kiroho, wakijikita katika upole na unyenyekevu, ili kuganga misigano hii
inayoweza kuacha madonda makubwa katika maisha ya watawa!
Baba Mtakatifu anakemea
ukatili unaofanywa kwenye Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, kwani hii ni sumu
kali dhidi ya maisha ya Kijumuiya. Watawa wasijitafute wenyewe na mafao yao binafsi,
daima wajitahidi kuongozwa na moyo mnyofu! Udugu na umoja katika maisha ya kitawa
ni jambo nyeti linalohitaji moyo wa mtu kujisadaka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu
ili kuona na kutambua ukweli wa mambo!
Baba Mtakatifu akizungumzia kuhusu uhusiano
kati ya Mashirika ya Kitawa na Makanisa mahalia anasema, Waraka wa kichungaji uliochapishwa
kunako Mwaka 1978 kuhusu uhusiano kati ya Watawa na Maaskofu bado ni muhimu sana na
wala haujapitwa na wakati. Watawa wanapaswa kujenga uhusiano wa dhati na Makanisa
mahalia, ili kulinda na kuendeleza karama za Mashirika haya katika Makanisa mahalia.
Karama hizi ziheshimiwe na kuthaminiwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia.
Maaskofu
watambue kwamba, Watawa ni wadau wa Uinjilishaji; watu wenye karama na utajiri mkubwa
katika utume na maisha ya Makanisa mahalia. Maaskofu na watawa wajenge utamaduni wa
mawasiliano. Kuna haja kwa Maaskofu na Watawa kupitia uhusiano wao ili kurekebisha
kasoro zilizojitokeza, kwa kutambua kwamba, watawa ni wadau muhimu sana katika Unjilishaji
Mpya. Hawa ni watu wanaojitoa kwa hali nam ali kwa ajili ya huduma kwa: Maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; katika sekta ya elimu, afya na maendeleo
endelevu. Katika huduma kwa maskini, Baba Mtakatifu anasema, huko wapelekwe watawa
wenye sifa, ari ya kuhudumia; watu wa Sala na tafakari ya Neno la Mungu, kumbe haitoshi
kuwa mtawa tu!
Baba Mtakatifu Francisko anatambua fika umuhimu wa sekta ya
elimu kwani hapan i mahali pa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiutu na kiimani;
ni mahali muafaka pa kutangazia Injili ya Kristo. Watawa wawe makini katika majiundo
ya wanafunzi wanaohudhuria masomo kwenye taasisi zao kwani kuna changamoto nyingi
katika maisha ya ndoa na familia; mambo ambayo wakati mwingine yanagumisha malezi
na makuzi ya watoto, kiasi cha kuwafanya kukosa amani, utulivu na furaha. Watoto wasilishwe
sumu ya kuchukia imani.
Mwishoni mwa mazungumzo kati ya wakuu wa Mashirika
ya Kitawa na Kazi za Kitume, Baba Mtakatifu alitangaza kwamba, Mwaka 2015 utakuwa
ni Mwaka wa Watawa; dhana inayoanza kufanyiwa kazi kwa sasa. Baba Mtakatifu anaendelea
kuyashukuru Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa mchango wao katika maisha na
utume wa Kanisa.
Mazungumzo haya yamehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP. S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.