Askofu mkuu Obbo wa Jimbo kuu la Tororo Uganda asimikwa rasmi
Askofu mkuu Emmanuel Obbo, hivi karibuni alisimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo
kuu la Tororo, Uganda, katika Ibada iliyohudhuriwa na Askofu mkuu Michael August Blume,
Balozi wa Vatican nchini Uganda, Maaskofu, watawa na waamini walei. Rais Yower Kaguta
Museveni alikuwa ndiye mgeni rasmi katika sherehe hizi. Ibada hii imeadhimishwa kwenye
Kanisa kuu la Mashahidi wa Uganda, Nyangole, Jimbo kuu la Toror, Uganda.
Askofu
mkuu Obbo katika mahubiri yake kwanza kabisa alimshukuru Mwenyezi Mungu, aliyemwita
na kumchagua kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tororo, Uganda na kwamba, kila Kristo
anaalikwa kwaza kabisa kuchuchumilia utakatifu wa maisha na baadaye miito mingine
ndani ya Kanisa. Hakuna sababu ya kuogopa kwani Mwenyezi Mungu anayemwita mja wake
atamkirimia neema na baraka anazohitaji katika kuwatakatifuza watu wa Mungu, kuwafundisha
na kuwaongoza kwa kufuata mfano wa Kristo mchungaji mwema.
Askofu mkuu Obbo
anasema Wakristo wanaalikwa kumpenda Mungu na jirani kwa kuwatumikia wananchi kwa
moyo mkuu, weledi, juhudi na maarifa. Katika kipindi hiki, Mama Kanisa anaendelea
kurudia ujumbe wa Kristo wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mwenyezi Mungu, kwa kujenga
na kuimarisha urafiki na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani.
Upendo unaobubujika
kutoka katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu hauna budi kumwilishwa katika
uhalisia wa maisha ya waamini ndani ya familia na Jamii katika ujumla wake. Chuki,
uhasama na magomvi ndani ya familia na Jamii ni mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa
na upendo wa Mungu kwa binadamu.
Rais Yoweri kaguta Museveni wa Uganda, katika
nasaha zake wakati wa kumsimika Askofu mkuu Emmanuel Obbo, amelishauri Kanisa kuendelea
kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli
za kilimo na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Uganda. Ameliomba Kanisa kusaidia
mchakato wa maboresho katika shughuli za uchumi na maendeleo, ili kuwajengea wananchi
uchumu utakaolisaidia hata Kanisa kuweza kujitegemea.
Rais Museveni anasema,
haogopi nchi za Magharibi kusitisha misaada yao kwa Uganda kwa sababu ya kupitisha
muswada wa sheria unaokataza vitendo vya kishoga nchini Uganda, bali anapania kuhakikisha
kwamba, wananchi wa Uganda wanasimama kidete ili kujiletea maendeleo yao wenyewe badala
ya kusburi misaada inayodhalilisha utu na heshima yao.