Mshikamano wa Kanisa na wagonjwa wa Ukimwi nchini Tanzania
Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa
ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya, hivi karibuni, alizindua mradi wa kupima
na tiba kwa wagonjwa wa Ukimwi, Jimbo Katoliki Shinyanga, Tanzania. Ni mradi unaoendeshwa
kati ya Mfuko wa Msamaria mwema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Kampuni
ya dawa kutoka Marekani ijulikanayo kama Gilead Sciences.
Zaidi ya
watu 120, 000 wanatarajiwa kufaidika na mradi huu inayojikita katika: sheria na kanuni
za tiba; maadili na utu wema. Watoto yatima watapewa kipaumbele cha pekee. Mradi huu
ni kielelezo cha mshikakano wa dhati katika mchakato wa kumhudumia mtu mzima: kiroho
na kimwili unaofanywa na Makanisa mahalia kama sehemu ya Uinjilishaji wa kina. Baraza
la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya linapenda
kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Jimbo
Katoliki la Shinyanga.
Hizi ni juhudi zilizofanywa kwa ushirikiano mkubwa
kati ya Marehemu Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga pamoja na Monsinyo
Jean Marie Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji
kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya, ambaye mara kadhaa alitembelea Tanzania
ili kuangalia uwezekano wa utekelezaji wa mradi huu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa
wa Ukimwi nchini Tanzania.
Askofu mkuu Zygmunt Zimowski anasema, Baraza la
Kipapa linaendelea kushirikiana na kushikamana na Kanisa Barani Afrika katika huduma
kwa wagonjwa kwa kutoa msaada wa hali na mali kadiri ya nafasi na uwezo uliopo. Kati
ya miradi hii ni ule wa “Africae Munus” Dhamana ya Afrika, unaovijumuisha vyuo vikuu
saba vya Kikatoliki Barani Afrika kwa lengo la kujenga mtandao wa majiundo makini
kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Baba Mtakatifu
Francisko anaendelea kulikumbusha Kanisa kwamba, hata wagonjwa katika shida na mahangaiko
yao, bado ni sehemu muhimu sana ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wanapaswa
kuheshimiwa, kuthaminiwa na kusaidiwa katika mahangaiko yao: kiroho na kimwili. Kumbe,
Vatican itaendelea kushirikiana na Makanisa mahalia katika huduma za kiroho na kimwili
kwa wagonjwa Barani Afrika.
Kati ya mambo yanayoendelea kupewa kipaumbele cha
kwanza kwa wakati huu na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi
katika sekta ya afya ni maandalizi kwa ajili ya ushiriki wa wagonjwa kwenye Ibada
ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu
hapo tarehe 27 Aprili 2014.
Huu ni mwanga wa imani na matumaini yanayobubujika
kutoka kwenye utakatifu na ushuhuda wa maisha ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili;
ni kiongozi ambaye hakuficha kuonesha ugonjwa wake, akakubali kuubeba Msalaba wa maisha
na utume wake kwa imani na matumaini, hadi siku ile alipoyamimina maisha na kujikabidhisha
kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake.