Kipindi cha Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho ya siku arobaini inayowakumbusha
Wakristo safari ya Waisraeli kutoka Utumwani Misri, wakatembelea Jangwani kwa miaka
arobaini kabla ya kufika kwenye Nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali. Wakristo wanakumbuka
siku arobaini ambazo Yesu alikaa Jangwani akifunga na hatimaye akaribiwa na Ibilisi,
kabla ya kuanza utume na maisha yake ya hadhara. Hizi ni siku arobaini za: kusali,
kufunga, kutafakari na kutenda matendo ya huruma.
Baba Mtakatifu Francisko
katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii anawakumbusha waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kwamba, furaha ya kweli inapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo:
mwaliko wa kukaa, kutembea pamoja na kuwa mfuasi wake mwaminifu.