Ushiriki wa AMECEA katika mkutano mkuu wa SIGNIS mjini Roma
Mkutano mkuu wa Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia
limehitimishwa hivi karibuni mjini Roma. Huu ni mkutano unaofanyika kila baada ya
miaka minne. Mwaka 2013 mkutano huu ulikuwa umepangwa kufanyika mjini Beirut, Lebanon,
lakini haikuwezekana kutokana na sababu za kiusalama huko Mashariki ya Kati na matokeo
yake umeadhimishwa mjini Roma kuanzia tarehe 25 Februari hadi tarehe Mosi, Machi 2014.
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican Padre Chrisantus Ndaga, Katibu wa Idara ya Mwasiliano, Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA anasema, mkutano
huu ulikuwa umegawanyika katika sehemu kuu mbili: Sehemu ya kwanza ilikuwa ni warsha
kuhusu vyombo vya habari na sehemu ya pili ilijikita zaidi katika mikutano na chaguzi
za kikanda. AMECEA kimsingi si mwanachama wa SIGNIS bali inasaidia kuratibisha mawasiliano
kati ya SIGNIS na nchi waachama wa SIGNIS, Afrika Mashariki na Kati.
Padre
Ndaga anasema, Nchi za AMECEA katika mkutano mkuu wa SIGNIS zilikuwa na uwakilishi
mzito, uliosaidia pia kupata wajumbe wawakilishi wa nchi za AMECEA katika vikao vya
SIGNIS. Huu ni mkutano ambao umeangalia mwelekeo wa tasnia ya habari kwa siku za usoni;
mambo yanayoibuliwa na tamaduni mpya ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia
pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa vijana wa kizazi kipya.