2014-03-06 12:38:05

Ndani ya Kanisa , muda wote ni wakati wa huruma ya Mungu , wito wa Papa kwa Mapadre wa Roma.



Baba Mtakatifu Francisko asubuhi hii ya Alhamisi 6 March, alikutana na Mapadre wa Jimbo la Roma, katika ukumbi wa Paul VI, mjini Vatican, kama zoezi la kiroho la kuanza kipindi hiki cha kwaresima. Na walitafakari juu ya huruma ya Mungu.
Katika hotuba yake , Papa amekiri kwamba kila binadamu anaihitaji huruma ya Mungu , hasa kwao Mapadre, wanao hitajika kuwa kielelezo cha huruma ya Mungu kwa watu wengine wengi . Papa alieleza kwa kurejea kifungu cha somo kutoka Injili ya Matayo, iliyosomwa kwao, akisema , kinawafanya wageuze fikira zao kwa Yesu, anaye tembea katika mitaa ya mijini na vijijini.
Papa amesema, aya hizo zinazua udadisi wa kutaka kujua ni wapi Yesu alipendelea kwenda mara nyingi zaidi, na inaonekana kama Yesu hakuwa na makazi maalum. Daima alikuwa barabarani . Maisha ya Yesu yalikuwa ni njiani na mitaani. Na hivyo, aya hizo zinatoa mwaliko wa kufahamu kina cha moyo wake ,kile ambacho yeye anajaribu kukitoa kwa umati wa watu, wanao tafuta kukutana nae njiani na mitaani, kwa ajili ya kutaka kujenga mahusiano ya upendo wa ndani , katika huruma ya Mungu isiyokuwa na kipimo , kama Injili inavyosema, aliyatazama makutano ya watu na kuwaonea huruma, kama kondoo wasiokuwa na Mchungaji.
Papa aliwataka Mapadre kupanua upeo wa macho yao si tu katika jiji la Roma na Italia, lakini kwa dunia zima. Wingi wa watu katika mataifa mbalimbali wanaoteswa na hali mbovu na ngumu zaidi ....Kwa hiyo wanapaswa kuwa na uelewa mpana kwamba uwepo wao katika mkutano huo, si tu kwa ajili ya kufanikisha zoezi la kiroho la kukianza kipindi cha kwaresima , lakini kusikiliza sauti ya Roho ambaye anazungumza kwa Kanisa zima katika nayakti hizi , ambao kweli ni wakati unao hitaji Huruma ya Mungu.
Na aliongeza kwamba, kwa Kanisa zima, kipindi hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu, kama ilivyokuwa maono ya Mwenye Heri Yohana Paulo II ambaye alikitangaza kipindi hiki rasmi kwa ajili ya Huruma ya Mungu, wakati akitoa homilia yake ya kumtaja kuwa Mwenye Heri na Mtakatifu Sista Faustina Kowalska.
Papa amewaambia Mapadre, ni juu yao, kama wahudumu wa Kanisa , kuweka ujumbe huu hai hasa katika mahubiri na maamuzi mengine ya Kichungaji , kwa mfano uchaguzi wa kutoa kipaumbele, Sakramenti ya Upatanisho , na wakati huo huo, kuonyesha utendaji wa huruma ya Mungu. Kupatanisha na kwa ajili ya kurejesha amani kwa njia ya sakramenti , na hata kwa maneno na matendo ya huruma.








All the contents on this site are copyrighted ©.