Maoni ya tume ya haki na amani Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhusu rasimu
ya Katiba Mpya
Yafuatayo ni maoni ya jumla ya rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
yaliyotolewa na Tume ya Haki na Amani Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja
na Chama cha Wanataaluma Wakristo Tanzania, CPT. A: Utangulizi Rasimu Na. 2
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitolewa na kuwasilishwa rasmi kwa Rais
Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 30 Desemba, 2013. Inawezekana kwamba, hadi sasa, si
wote tumepata fursa ya kuipitia angalau mara moja Rasimu hiyo. Nia ya andiko hili
ni kutoa maoni ya jumla juu yake. Maoni haya yameandaliwa na Sekretariati ya Tume
ya Haki na Amani ya TEC kwa kuzingatia tafakari na uchambuzi makini uliofanywa na
Christian Professionals of Tanzania (CPT). B: Tuliyohimiza, Kuonya na Kutahadharisha
Mwanzoni na Juu ya Rasimu Na. 1 Katika mapendekezo yetu ya mwanzo kabisa na yale
juu ya Rasimu Na. 1, tulihimiza, kusisitiza, na wakati mwingine kuonya na kutahadharisha
kiunyenyekevu lakini kwa makini na ufasaha wa maelezo, mambo muhimi yafuatayo, kati
ya mengine: Misingi thabiti na halali ya Katiba Mpya sharti iwe ni watu/utu,
uhuru, haki, ukweli/uwazi na mshikamano vinavyojenga hali ya amani na maendeleo yao/yake:
Wananchi kuwa na haki na uwezo zaidi wa kushiriki katika mambo ya maendeleo, uchumi
na ya utawala wa nchi yao kihalisia moja kwa moja na kwa njia za uwakilishi. Umuhimu
wa masharti ya kikatiba juu ya maadili mema, uwajibikaji, uwajibishwaji na miiko ya
viongozi na watumishi wa umma vikiendana na chombo (Tume) au maelekezo na masharti
muafaka ya utekelezaji wake kwa mujibu wa sheria inayozingatia masharti ya Katiba
Mpya. Umuhimu wa umoja wa Taifa letu na uzalendo katika uongozi na utumishi wa
umma kwa lengo la kutumikia vyema wananchi na nchi (vizazi vya sasa na vijavyo) kwa
ujumla: Sera, malengo, mipango na sheria za Jamhuri ya Muungano na za Nchi Washirika
kutakiwa na Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano kuzingatia maslahi ya nchi na wananchi
walio wengi na hasa wale walio katika hali hatarishi ya umaskini uliokithiri na jumuiya/makundi
yenye vipato vya chini na kufuata katika utekelezaji wake maelekezo na masharti ya
Katiba hiyo ya Jamhuri ya Muungano. Umuhimu wa haki za binadamu zilizopanuliwa
na kuboreshwa kwa kuzingatia maadili mema na bila kukiuka sheria ya kimaumbile, ambazo
yapasa zitekelezeke pasipo mikwara ya kisheria inayokinzana na nia na madhumuni msingi
ya Katiba na inayoacha mianya ya dola/uongozi kukwepa uwajibikaji na uwajibishaji;
umuhimu wa kuimarisha haki ya mtu kuishi tangu kutungwa mimba, masharti ya kufuata
na kuendesha mambo ya kiimani/kidini pasipo kutumia njia hasi dhidi ya imani/dini
za wengine; nk. Umuhimu wa Katiba Mpya kukomesha tatizo la Katiba na sheria kutoa
kwa viongozi na watumishi wakuu Serikalini mamlaka yasiyo na misingi, vigezo, taratibu
wala mipaka ungozi na muafaka ya kufuata katika utekelezaji wake au kutunga sheria/kanuni
za kuelekeza na kuongoza utekelezaji huo. Katiba Mpya kudhibiti mamlaka na madaraka
(yasiyo na vigezo, taratibu wala kikomo katika utekelezaji wake isipokuwa busara na
hekima kama sio hurka) ya Rais: Kwamba katika kutekeleza madaraka hasa ya kuteua na
kuwajibisha kinidhamu viongozi wa juu Serikalini na katika utumishi wa umma, hatua
za awali zichukuliwe na kukamilishwa na vyombo wakilishi na shirikishi vya umma vilivyoundwa
na vinavyofanya kazi kwa mujibu wa ama Katiba Mpya au sheria inayotimiza maelekezo
na masharti ya Katiba hiyo – likiwemo Bunge. Kazi ya Rais iwe ni kurasimisha yaliyofanywa
na vyombo hivyo husika kwa misingi bora kimaadili. Kwamba Idara ya Mahakama iwe
na haki ya kuwasilisha makadirio yake ya mapato na matumizi ya mwaka moja kwa moja
Bungeni kama Mhimili unaojisimamia ili kuimarisha uhuru wake, hadhi yake na utawala
wa kisheria nchini; na utaratibu wa kuteua majaji na viongozi katika Mhimili huu ufuate
mapendekezo kwenye kifungu cha 6 hapo juu. Kwamba na maeneo mengine ya utumishi
wa umma kama Bunge, ulinzi na usalama, polisi, utawala, maadili na uwajibikaji wa
uongozi na watumishi wa umma, usimamizi na uhakiki/udhibiti wa fedha za umma na mambo
ya vyama vya siasa yawekewe utaratibu wa kifetha na kuteua viongozi na watumishi waandamizi
wake unaofanana na ule unaotajwa kwenye kifungu cha 7 hapo juu. Tangu mwanzo, suala
la Muungano tulilichukulia msimamo wenye mambo ya kimsingi matatu :
Muungano wetu una mizizi mirefu ya kihistoria - kijamii, kiuchumi,
kisiasa na kiutamaduni -ikiwemo miaka hamsini (50) ya Jamhuri ya Muungano pamoja na
magumu na changamoto zake kubwa na ndogo. Umuhimu wa kuzingatia ukweli kwamba
wananchi wengi wa Bara na Zanzibar-Pemba ni maskini au wa kipato duni kisichokidhi
mahitaji. Hivyo, wanachohitaji ni maendeleo kutokana na rasilmali ya sehemu hizi mbili,
nyingi zikiwa Bara: Muungano sharti ulenge kuleta maendeleo yao na Taifa, si kuwapa
wachache (watumishi wao) madaraka na uhondo wa uhuru; sharti uwe ni wa manufaa kubwa
kwa maendeleo ya Wananchi wote wa enzi hizi na wa nyakati na vizazi vijavyo. (i)
Muungano wa aina ya serikali mbili umeghubikwa na matatizo mengi ambayo hayajawahi
kujadiliwa na kutatuliwa kwa njia halisi na muafaka za kidemokrasia: Lakini hiyo si
sababu ya kutamani kurudi nyuma bali ni sababu ya kupiga moyo konde na kutafuta suluhu
inayoimarisha, siyo inayoyumbisha, Muungano katika misingi yake ya ‘umoja ni nguvu
utengano ni udhaifu’;
(ii) Dhana ya ‘Serkali tatu’ tangu mwanzo ilionekana
haifai kwa sababu ya gharama, udogo wa mmoja wa nchi Washirika, na sababu hii ya pili,
pia, ilifanya dhana ya ‘Serikali moja’ isitumike kwa hofu ya nchi hiyo ndogo kumezwa;
na (iii) CPT na Kanisa zima (kupitia TEC) mwanzoni tulipendekeza dhana ya ‘Serikali
moja’ kwa njia ya mchakato endelevu wa mjadala na maafikiano juu ya mambo muhimu ya
Muungano usio na kikomo cha muda bali wenye nia thabiti na lengo mahsusi la umoja
kwa misingi muafaka ya kidemokrasia. Hivyo, muundo wa Serikali mbili ungeendelea kurekebishwa
huku, pia, mambo ya Muungano yakiendelea kuongezwa au kuboreshwa kwa nia na misingi
hiyo. Ingawa kwenye mapendekezo yetu (CPT-TEC) juu ya Rasimu Na. 1 tulitoa mawazo
yetu juu ya muundo uliopendekezwa na Tume ya Kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, tuliendelea kuonya na kusisitiza juu ya athari mbaya za muundo huo kwa
mustakabali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Umuhimu wa Serikali
kuwa ya kisekula (kutokuwa na dini teule) au kuruhusu masuala ya kidini katika utawala
wa nchi (Jamhuri ya Muungano na Nchi Washirika); kutoruhusu mahusiano na nchi nyingine
au taasisi kama OIC yanayoilazimu nchi au Serikali yetu kuvunja kanuni msingi hii
ya usekula.
C: Ulinganisho kati ya Tuliyohimiza, kuonya na kutahadharisha
na Maudhui ya Rasimu Na. 2 Kwa kiwango kikubwa, mambo yaliyotajwa katika vipengele
Na. 1 – 8 na 10 yamezingatiwa katika kuandaa Rasimu Na. 2, ingawa bado mtu angependa
uboreshaji wa hapa na pale. Lakini tunajua kuwa si kila tulilolipendekeza na hata
kwa msisitizo lingechukuliwa au kuwekwa kwa namna inayokithi matazamio na mapenzi
yetu; kwani pia yalikuwepo mapendekezo ya makundi na jumuiya nyingine ambazo mawazo
na mapendekezo yao ama yalikuwa yanafanana au yanatofautiana, au hata kukinzana, na
yale ya kwetu.
Tukipitia kila kipengele na kulinganisha tuliyopendekeza juu
ya Rasimu Na. 1 na yaliyomo katika Rasimu Na. 2 tutaona mara moja yaliyochukuliwa
kwa namna moja au nyingine hapa na pale na yaliyoachwa kabisa. Hapo, tujiulize ni
yepi kati ya yale yaliyoachwa kabisa yatupasa tuendelee kuyasisitiza na ni yepi tuyaache
kwa awamu hii ya mchakato wa kuunda Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mifano
michache, kati ya masuala ambayo bado yanaibua maswali ndani ya Wakatoliki na watu
wengine wenye mwelelekeo wa mawazo unaofanana na wa Kanisa Katoliki, ni kama ifuatavyo:
kulinda haki ya uhai tangu kutungwa mimba kwa mtu; kutajwa kwa “Mungu”
angalau katika Utangulizi; suala la mahusiano ya kimataifa kuwa ni sehemu ya mambo
ya nchi za nje na hivyo kuwa la Muungano na kupunguza uwezekano wa Nchi Washirika
kuwa na mahusiano yanayoweza kuimarisha utengano badala ya umoja hasa katika nyanja
za kidini; kukosa kanuni mahsusi ya kijumla ya kukomesha kikatiba tatizo la sheria
na kanuni nyingi zinazotoa madaraka yasiyo na mipaka na wajibu usio na masharti fasaha
na wazi ya taratibu, misingi, vigezo au adidu rejea na hatua za kinidhamu za kuchukuliwa
dhidi ya wasiowajibika na wasiowajibisha ipasavyo kwa mujibu wa Katiba na/au sheria
za nchi na, hivyo, kuacha mianya ya kukwepa uwajibikaji na uwajibishaji wa viongozi,
watumishi, mamlaka na vyombo vya umma. Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jaji Joseph S. Warioba, wakati
akiwasilisha Rasimu Na.2, suala lililoendelea kuitesa Tume hiyo hadi mwisho ni lile
la Muungano. Sisi pia na wengine wengi nchini lilitutesa na litaendelea kuibua hisia
za mashaka: Picha inayotoka ni kwamba moyo wa Watanzania wanaodaiwa na Tume kuwa pia
ni wengi kipindi hiki ni wa kuwa na muungano dhaifu wa aina ya Shirikisho si ya kuimarisa
na kuendeleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa nchi huru mbili, Tanganyika na Zanzibar,
zilizojivua utaifa wa kila mojawapo ili kuunda Taifa kubwa zaidi na lenye umoja, na
hivyo, nguvu zaidi kuliko kila mojawapo ingebaki katika hali yake ya awali ya utengano.
Huu, kama tulivyoonya na kutahadharisha awali, ni moyo wa kuelekea
kwenye kutengana si kuungana zaidi. Hapa, yatupasa Watanzania wote tujiulize maswali
yafuatayo na tuyatafakari kwa makini:
Je, Rasimu Na. 2 imejaribu
vipi kupunguza kasi ya kuporomoka kwa umoja wa kitaifa unaotegemezwa kwenye misingi
haba saba (7) iliyobaki? Na je, yale yaliyopendekezwa yakipita vema kwenye mchakato
wa ridhaa ya Wananchi wa Tanzania na kukubaliwa, mustakabali wa Muungano utasimama
na kuhakikishwa kwa misingi hiyo? Au, je, kama baadaye Nchi Mshirika mojawapo
ikitafuta uhuru zaidi kama si kujitoa kabisa katika Muungano, ile misingi iliyobaki
au itakayorekebishwa kukidhi ukiukwaji uliofanywa dhidi ya Katiba ya sasa, itaweza
kuhimili udidimiaji wa moyo wa kuuthamini umoja na kujenga hali na mazingira ya uongozi
na wananchi kuona hatari na hasara za utengano? Je, tuko tayari kuona umoja wetu
unasambaratika kama ilivyotokea na inavyotishia kwingineko Barani Afrika [Sudan, Ethiopia,
DRC, Libya) na hata nje ya Afrika (USSR,Yugoslavia, Czechoslavia, Muungano wa Kifalme
wa Uingereza (UKoGB) ambako Scotland na North Ireland zinatishia kujitenga na kuwa
nchi huru kabisa, nk.]? Tutajiepushaje hali ya kujikuta tunakabiliwa na vita vya wenyewe
kwa wenyewe kwa sababu ya tabia na mazoea hatarishi ya kutotumia njia adili za kuendesha
masuala muhimu na nyeti ya kitaifa likiwemo la Muungano?
Sababu zinazotolewa za kuendeleza utengano zina asili gani, ya matakwa ya
uhuru na maendeleo ya kweli ya wanyonge au ya wenye (uchu na/au) malengo ya madaraka,
maslahi binafsi na ya kitabaka yanayokuzwa na kufanywa maslahi ya kitaifa na ya umma?
Je, katika Awamu hii ya IV ya utawala ndani ya Muungano, Muungano una mtetezi
katika Dola kati ya wale waliokula viapo kuulinda na kuutetea na, kama wapo, inakuwaje
hatujawahi kuwaona au kuwasikia wakijitokeza kidhati na kwa hoja makini -
kuutetea kwa hoja makini ya kudhihirisha faida zake ambazo yapasa ziimarishwe,
kulindwa na kuendelezwa kwa manufaa na maslahi zaidi ya kizazi kilichopo na vijavyo?
kuhusu athari za kudhoofika na/au kuvunjika kwake kwa umma wa Watanzania wa kizazi
hiki na vizazi vijavyo? Zinzoelezea jitihada na hatua thabiti na za dhati za kushughulikia
mambo na masuala ya Muungano kwa njia za kidemokrasia zilizo adili na makini, shirikishi
na wakilishi kwa ngazi za Wananchi na za Serikali?
Tume ya Jaji Warioba
imeshindwa kujibu hoja yetu (CPT) ya kubainisha kiyakinifu faida na athari za Muungano
ambazo watu waliohojiwa walizitoa licha ya kuorodhesha, pasipo ulinganifu na faida,
kero zilizoelezewa (na wawakilishi? wa) pande mbili (Nchi Washirika) za Muungano. D: Yaliyo
Bora na ya Kuhofia Kimaadili na kwa Mustakabali wa Umoja wa Kitaifa Katika Rasimu
N. 2 Ya Kuhofia Kimaadili na kwa Mustakabali wa Umoja wa Kitaifa Kuna mambo
matatu muhimu ya kutafakari pamoja kwa njia ya kujiuliza maswali hasa baada ya kuyasikia
na kuyasoma yaliyotolewa taarifa na yaliyopendekezwa na Tume ya Kurekebisha Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Tume ya Jaji Warioba). Nayo ni kama ifuatavyo:-
Jambo
la kwanza na kuu kati ya mengineyo yanayotia wasiwasi kimaadili na ya kuhofia kwa
mustakabali wa umoja wa Taifa letu ni kwamba Tume ya Jaji Warioba imelazimika kupendekeza
mfumo/muundo wa Muungano wa serikali tatu badala ya mwendelezo wa serikali mbili kwa
sababu hasa ya kuzingatia hali halisi ya sasa ndani ya Muungano: Kwamba mojawapo ya
Nchi Washirika (Zanzibar) iliishafanya mabadiliko ya Katiba yake kinyume cha Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vile kwamba haiwezekani hata kufikiria kuendeleza
mfumo wa sasa wa Muungano wa serikali mbili ambao vilevile umenung’unikiwa kwa muda
mrefu kutokana na kinachoitwa “kero” nyingi za mfumo huo wa serikali mbili. Maana
yake ni kwamba tunalazimika kufumua muundo wa sasa pasipo Nchi Washirika kwa pamoja
na kwa njia muafaka kujiandaa na kukubaliana kwanza juu ya hatua hiyo kwa sababu mojawapo
wa Nchi Washirika imeishajichukulia madaraka tayari ya kuufitinisha na kuubatilisha
kwa kufanya mabadiko kadhaa makubwa katika Katiba yake kinyume cha masharti ya Katiba
kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyouweka muundo huo.
Hofu
na wasiwasi unaojitokeza kihalali kabisa ni kama bado kuna moyo thabiti wa kuendeleza
Muungano! Je, kilichotokea kinaashiria kwa upande wa uongozi wa Nchi Washirika zote
mbili utamaduni wa dhamira na maadili ya umoja au ya ulegevu na udhaifu wa moyo unaoleteleza
utengano? Uongozi wa Muungano unathamini na uko makini kwa kiwango gani kuhusu masuala
muhimu na nyeti ya kitaifa?
Jambo la pili la kuhofia kimaadili
na kwa mustakabali wa umoja wa Taifa letu linatokana na hilo la kwanza: Nalo ni kama
Muungano wa aina ya Shirikisho unaopendekezwa umewekewa misingi ya kutosha katika
Rasimu Na. 2 ya Katiba ya Jamhri ya Muungano ya kuhakikisha kwamba kilichojiri kwa
muundo wa sasa hakitajirudia chini ya mfumo huo unaopendekezwa? Katika hali ya udhaifu
wa dhamira na maadili ya umoja wa kitaifa kwa uongozi, kitakachozuia utovu kwa Nchi
Washirika au mojawapo kudiriki kwenda njia yake machoni pa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano ni nini? Rasimu ya Katiba Na.2 inajibu vipi swali hili na jibu hilo linatosheleza
kuondoa wasiwasi huo na hofu hiyo?
Jambo la tatu na
la mwisho kwa mada hii ni la Watanzania kujiuliza kama Katiba ya sasa au ile inayopendekezwa
na Tume katika Rasimu N. 2 na hata ya aina nyingine yoyote ile tunayoweza kuibuka
nayo mwishoni mwa mchakato wa sasa wa kuunda Katiba Mpya inaweza kujibu na kukidhi
mahitaji, matakwa na matumaini yetu yote ya kikatiba? Je, tunaweza kufikia hatua ya
kusema kwa pamoja kama Wananchi na Taifa bila kuwa na ngawanyiko wowote kwamba sasa
tunayo Rasimu ya Katiba aina ya mfano bora kuliko zote na ambayo ni muafaka kwa kila
mmoja wetu katika Nchi Washirika? Je, kuna nchi yoyote duniani ambayo ina katiba kama
hiyo?
Je, mjadala juu ya ni kipi kilicho bora kwa wananchi na nchi leo
na baadaye kikatiba unaweza kufikia kikoma au ukamilifu au kusitishwa na nguvu yoyote
ya kimaumbile? Je, hofu na wasi wasi wetu wa sasa kimaadili na kwa mustakabali wa
umoja wa Taifa letu iwe ni sababu ya kutopokea kwa moyo mkunjufu kile kinachoweza
kunusuru dhamira na maadili ya umoja katika hali iliyobadilika kihalisia?
Mlolongo
huu wa maswali unadai sehemu ya majibu na ni hiyo tunayogeukia hapo chini. Lakini
nia si kujibu kila mojawapo ya hayo maswali, kwani mengi yanaonyesha mwelelekeo wa
kutohitaji jibu mahsusi. Nia ni kuona kama Rasimu Na. 2 ina maudhui ya mambo bora
yanayoweza kuendeleza umoja, kuimarisha mahusiano, mshikamano na kuleta maendeleo
kwa wananchi ndani ya Shirikisho la Nchi Washirika.
Kama yapo, swali ni kama
yanaweza kuboreshwa na hivyo kutuwezesha kama Taifa, katika kipindi hiki kigumu cha
majaribu, kuvuka au kuyakabili magumu hayo kijasiri na hivyo kuendelea kukomaa zaidi
kitaifa kutokana na mchakato endelevu wa tafakari, mjadala na maamuzi muafaka ya kidemokrasia
kila inapowezekana au kuonekana ni bora kufanya hivyo kwa ajili ya maendeleo na amani
ya wananchi na nchi yetu.
Kuna busara kubwa na unabii katika usemi : ”Yaliyopita
si ndwele; tugange yajayo!” Tusije tukajitia hatiani kwa kosa la ‘kuifanya migumu
mioyo yetu’ na hivyo kushindwa kuzing’amua tunu zilizowasilishwa mbele yetu katika
Rasimu Na. 2 pamoja na changamoto zake Rasimu hiyo. Basi tuangalie kama Rasimu
Na. 2 imetuwekea misingi bora ya kuweza kuganga yajayo.
Yaliyo Bora Kimaadili
na kwa Umoja wa Taifa Yapo mambo kati ya maudhui ya Rasimu Na. 2 ambayo ni mazuri
na muhimu kiasi kwamba yapasa tuyachukulie kama mambo msingi yanayobeba na yanaweza
kudumisha na kuendeleza utamaduni, maadili na dhamira au moyo wa umoja wa nchi yetu
Tanzania katika hali halisi ya sasa. K`wayo, katika mazingira ya umoja wa aina ya
shirikisho, kuna uwezekano kwa Nchi Washirika (viongozi na wananchi wake) - kuendeleza
kidemokrasia mahusiano ya karibu kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na kwa kutambua
mema ya kushirikiana kwa namna hiyo zaidi na zaidi na magumu ya kufanya kinyume chake;
kutambua umuhimu wa kuheshimiana na kushirikiana kimshikamano kwa misingi iliyo
bora na iliyowekwa kikatiba kwa maridhiano muafaka; na kutambua na kuthamini vema
tunu na rasilmali za kila Nchi Mshirika zinazoweza kutumika kwa manufaa zaidi kwa
wananchi kwa kuongeza, kuimarisha na kuendeleza zaidi misingi ya mshikamano na umoja
kisiasa, kiuchumi na/au kiutamaduni.
Kwa ajili ya hayo, ni muhimu tutambue
mambo manne ya msingi zaidi kijamii kwa umoja wa Nchi Washirika katika aina yoyote
ya muungano au mashikirikiano: Mambo hayo hudhihirika katika kiwango cha juu cha kufanana
na kuzingatiwa katika nyanja nne (4) za maisha ya siku hadi siku. Na hayo mambo, pamoja
na nyanja hizo, ni kama ifuatavyo: (a) Utamaduni (lugha, maadili, mila na desturi
na historia ya pamoja ya mahusiano/ushirikiano wenye manufaa kwa Nchi/Wananchi Wahusika);
(b) Mifumo ya kisheria (Katiba, sheria na kanuni msingi); (c) Miundo ya dola
(wizara, idara, taasisi na asasi zake kuu na za kijamii); na, kubwa kuliko yote (d)
Moyo wa kuthamini umoja na ushirikiano kwa misingi thabiti na muafaka ya ‘toa na
pokea’ (toa chako anachohitaji mwenzako ili nawe upokee chake unachohitaji kwake),
uhuru, haki, ukweli na mshikamano kwa misingi ya kuheshimiana na kustahimiliana. Mambo
haya na nyanja hizi nne kati ya nyingine tukizitafakari na kuzijadili kwa makini tutagundua
siri ya udumifu wa umoja, ushirikiano na mshikamano wa dhati wa madola, taasisi za
kikanda na za kimataifa na hata kila dola na kila nchi iliyo na sifa au historia inayoashiria
uwepo wa mambo hayo. Nyanja hizi zinawezesha mazungumzo na mjadala endelevu wa kuelekeza
nchi ndogo au kubwa, moja au mbili na hata zaidi kwenye namna moja ya umoja au ushirikiano
kutoka viwango vya chini hadi vya kileleni. Kwa uhakika, misingi hii hii inaendelea
kusaidia dunia kujenga hali mpya ya mahusiano na ushirikiano wa kikanda na wa kimataifa
pasipo wakati wote utumiaji wa mabavu, mauaji na maangamizi ya kivita.
Kwa
kuzingatia maelezo hayo, tuangalie kwa kifupi, mambo yaliyo bora katika Rasimu Na.
2 yanayoweza kuwa ni nguzo za kuegemezea umoja na ushirikiano endelevu chini ya Katiba
Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nayo ni kama ifuatavyo: (1)Yale yote yaliyo
kwenye Sura ya Kwanza hadi Sura ya Nne; yaani: Jina, Mipaka, Alama,
Lugha na Tunu za Taifa; Mamlaka ya Wananchi, Utii na Hifadhi ya Katiba; Malengo
Muhimu, Misingi ya Mwelekeo wa Shughuli za Serikali na Sera za Kitaifa; Maadili
na Miiko ya Uongozi na Utumishi wa Umma; na Haki za Binadamu, Wajibu wa Raia na
Mamlaka za Nchi (na Mipaka ya Haki za Binadamu).
Kati ya hayo, yale yaliyo
katika Sura ya Kwana, Sura ya Pili na Sura ya Nne ni baadhi ya mambo sita (6) ambayo
hayawezi kufanyiwa mabadiliko - “hadi mabadiliko hayo yaungwe mkono na theruthi
mbili ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano
kwa Kura ya Maoni itakayoendeshwa na kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria za nchi”. Masharti kuhusu
Uraia wa Jamhuri ya Muungano yanafanya jambo hilo muhimu liwe na hadhi ya kikatiba,
ambapo hadi sasa halikuwa la kikatiba bali la sheria ya kawaida iliyotungwa na Bunge
la Jamhuri ya Muungano. Masharti kuhusu Serikali ya Jamhuri ya Muungano - Serikali,
Rais, Makamu wa Rais na Baraza la Mawaziri pamoja na Tume ya Uhusiano na Uratibu
wa Serikali hiyo - licha ya kuwa lina magumu na changamoto kadhaa za ‘’Shirikisho’’,
lina uzuri wa kuendeleza dhana na siasa ya umoja na mshikamano wa kitaifa ndani ya
Jamhuri ya Muungano-Shirikisho wa (Nchi Washirika) Tanzania. Bunge la Jamhuri ya
Muungano ni jambo kubwa lingine la kutilia maanani kama chombo kimojawapo cha kusaidia
kuendeleza mjadala, mahusiano, sheria, kanuni na taratibu rasmi za umoja wa kitaifa
katika hali iliyobadilika kikatiba kwenye muundo wa dola la Taifa na kupungua kwa
mambo ya Muungano au umoja wa kitaifa.
Mahakama (ya
Juu na ya Rufani) ya Jamhuri ya Muungano itakuwa chombo muhimu sana cha kujenga msingi
mpya na kuimarisha misingi iliyodhoofishwa ya kisiasa, kiutamaduni na hata ya kiuchumi
ya Jamhuri ya Muungano-Shirikisho. Masharti husika ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
ya sasa yanaunda Mahakama ya Jamhuri isiyo na madaraka juu ya raia na dola ya kuamua
mashauri na kuwajibisha bali ya kushauri na kusuruhisha tu. Hata hivyo, hayajawahi
kutekelezwa hadi leo. Masharti ya Katiba tarajiwa kwa Mujibu wa Rasimu Na. 2, yanaifanya
“Mahakama ya Juu [kuwa] ni ngazi ya mwisho ya rufani katika Jamhuri ya Muungano ...”.
Aidha, inatoa kwa Mahakama ya Juu hiyo madaraka ya–
(a) pekee na ya awali
ya kusikiliza na kuamua mashauri yanayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhyri
ya Muungano; (b) kusikiliza na kuamua mashauri yatakayowasilishwa na wananchi,
Serikali za Nchi Washirika kuhusu tafsiri au utekelezaji wa Katiba hii; (c)usikiliza
na kuamua migogoro baina ya Nchi Washirika na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; (d)kusikiliza
na kuamua rufani kutoka Mahakama ya Rufani [ya Jamhuri ya Muungano]; (e)kutoa ushauri
kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali za Nchi Washirika, pale itakapoombwa;
na (f)kusikiliza na kuamua shauri lolote litakalowasilishwa mbele yake kwa mujibu
wa Katiba hii au sheria nyingine yoyote itakayoipa Mahakama hiyo mamlaka. Vile
vile “Mahakama ya Rufani pamoja na mahakama za Nchi Washirka, isipokuwa Mahakama ya
Juu, zitalazimika kufuata maamuzi ya Mahakama ya Juu”. Pamoja na hayo, Ibara ya
167(1) inaipa Mahakama ya Rufani mamlaka ya- kusikiliza na kuamua
kila rufani inayowasilishwa mbele ya Mahakama ya Rufani kutokana na hukumu au uamuzi
wowote wa Mahakama Kuu za Nchi Washirika au Mahakama yoyote ya chini iliyopewa mamlaka
maalumu ya kusikiliza mashauri ambayo kwa kawaida husikilizwa na Mahakama Kuu; kufanya
mapitio ya maamuzi ya Mahakama Kuu za Nchi Washirika au mahakama yoyote ya chini iliyopewa
mamlaka kusikiliza mashauri ambayo kwa kawaida husikiliwa na Mahakama Kuu.
Jambo la Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano
Umuhimu wa
jambo hili kwa kuendeleza umoja wa kitaifa katika hali iliyobadilika ni mkubwa na
wa kimsingi kabisa. Kwa mujibu wa Ibara ya 1 ya Rasimu Na. 2, licha ya kwamba kinachopendekezwa
ni Muungano wenye muundo wa Serikali Tatu, bado umoja wa kitaifa kikatiba utabaki
kama hayo yote yaliyoelezwa tayari na yanayofuata hapa chini yanavyoashiria. Tukianza
na hiyo Ibara ya 1: (1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye
mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nch mbili za Jamhuri ya Tanganyika
na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya
mwaka 1964, zilikuwa nchi huru. Aidha, chini ya Ibara ya 71 kuhusu Rais wa Jamhuri
ya Muungano, (2) Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa
Serikali na Amiri Jeshi Mkuu na: (a) atakuwa taswira ya Jamhuri ya Muungano na
watu wake; (b) atakuwa alama ya umoja, uhuru wa nchi na mamlaka yake; na (c)
atakuwa na dhamana ya kukuza na kuhifadhi umoja wa kitaifa. Ibara ya 235(1) inatamka
kuwa «jukumu la ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano ni la kila rai». Hata hivyo,
Ibara ya 236 inaweka masharti kuhusu vyombo vya Ulini na Usalama wa Taifa: Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania; Jeshila Polisi la Jamhuri ya
Muungano; na Idara ya Usalama wa Taifa.
Chini ya Ibara ndogo ya 236(4)
na (5): Mtu hataruhusiwa kuanzisha taasisi, kampuni, jumuiya au shirika linalohusiana
na ulinzi na usalama wa Taifa au ushirika wa kijeshi, isipokuwa kama inavyoruhusiwa
na Katiba hii au sheria za nchi. Vyombo vya ulinzi na usalama wa Taifa vitakuwa
chini ya mamlaka ya Rais. Haya si mambo ya kubeza au kuchukuliwa kivyepesi bali
kuyaona kuwa ni baadhi ya misingi ya umoja wa Taifa letu kusimamia na kusonga mbele
katika hali mpya kikatiba, kisiasa na kiuchumi.
Jambo lingine
bora ambalo ni kubwa na la msingi kimaadili na kwa mustakabali wa umoja wa Taifa ni
masharti yanayohusu Tume (Huru), Mabaraza na Kamati mbalimbali zilizoundwa kikatiba
kwa ajili ya maeneo na sehemu zote muhimu za utumishi wa umma. Hivi ni vyombo vyenye
dhima ya kuweka kwa mujibu wa sheria misingi ya taratibu za uwazi, na iliyo shirikishi
na wakilishi katika uteuzi wa viongozi wa juu na watumishi waandamizi wa umma na masuala
husika ya kimaslahi na ya kinidhamu. Kwavyo, tatizo la Mhimili mmoja wapo (Serikali/Urais)
wa Mihimili mitatu ya Dola kuwa na madaraka yasiyo na mipaka, misingi, vigezo na taratibu
muafaka na wazi linaweza kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa.
Tume hizo muhimu
kwa majina ni kama ifuatavyo: Tume Huru ya Uchaguzi ya (Jamhuri ya)
Muungano; Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali; Tume ya Utumishi wa Bunge; Tume
ya Utumishi wa Mahakama; Tume [Huru] ya Maadili na Uongozi na Uwajibikaji; Tume
[Huru] ya Haki za Binadamu; Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania; Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi.
Kamati za Muungano ni
kama ifuatavyo:- Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti
na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi; Kamati Maalimu ya Uteuzi [wa Viongozi na Watumishi
Waandamizi wa Umma]; Kamati Maalimu ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti
na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu; Kamati ya Utekelezaji wa Katiba katika
Muda wa Mpito.
Kuna Baraza moja la Muungano lililopendekezwa, nalo ni:
Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
Rasimu imependekeza
miaka minne (4) ya Kipindi cha Mpito. Mauthui ya Ibara husika ni mazuri na kwa kiwango
kikubwa yanakidhi mapendekezo yetu na bila shaka na ya watu na asasi nyinginezo zilizowasilisha
maoni kwa Tume ya Jaji Warioba. Kamati maalumu ya kusimamia na kuratibu utekelezaji
wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa, pia, itashughulikia mapendekezo
ya sheria muafaka mbalimbali zinazolengwa na Katiba Mpya hiyo pamoja na urekebishaji
wa sheria nyingine zitakazoathiriwa na Katiba hiyo.
Kipindi hiki
muhimu kitatoa fursa ya kwanza kwa Wananchi na viongozi wao kujipanga upya baada ya
Katiba Mpya kupitishwa kulingana na masharti ya Katiba hiyo. Kitakuwa ni kipindi cha
kuendelea kujadiliana, kutafautiana bila kuzozana na kukubaliana kwa misingi ya kidemokrasia
na katika hali ya amani na utuluvu. Hii itatokea kama tutafanikiwa kukabili vema changamoto
za mchakato kabla na wakati wa kuijadili na kuipitisha Katiba Mpya tarajiwa katika
hatua za awali mbili zilizobaki, ya Baraza la Kutunga Katiba na Kura ya Maoni. Hivyo,
pia, utakuwa ni wakati muafaka wa kutahini moyo wetu wa umoja na ukomavu wetu wa kisiasa
kama Taifa. TUOMBE MUNGU!
F: Hitimisho Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, 2013 ilitegemewa kuibua mjadala wenye msisimko wa aina yake;
kwani umechangiwa mawazo, maoni na hata mapendekezo maalumu yaliyotolewa kwa mdomo,
kwa maandishi na kwa njia nyingi mbalimbali zilizokaribishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Jambo moja la wazi tangu Rasimu Na. 1 kutangazwa ni la Wananchi kugawanyika katika
makundi makuu manne.
Jambo hilo ni lile la muundo wa Jamhuri ya Muungano:
Baadhi, wanapendelea muundo wa sasa wa Serikali mbili uendelee; baadhi, ule wa Serikali
moja (mara moja, katika muda mfupi au, kimchakato, baada ya muda usiotabilika sasa),
baadhi, ule wa Serikali tatu, kama Rasimu inavyopendekeza, na baadhi, Muungano wa
mkataba. Haijulikani hatima ya mjadala huu kipindi hiki itakuwa nini au vipi: Je tutaibuka
na Katiba Mpya au tutarejea kwenye Katiba tata ya sasa? Itakumbukwa kuwa tulijiuliza
swali hili tangu mwanzo wa mchakato wa kushughulikia suala la Katiba Mpya chini ya
Sheria husika na ya Tume ya Jaji Warioba; na bado linatukabili! Lakini hali hii
isitutishe wala kutupa wasiwasi kwani inaashiria jinsi watu walivyoamka kisiasa na
kwamba kweli wanataka mabadiliko. Hata hivyo, mabadiliko hayo wanayotaka kwa dhati
hayaashiriwi hasa na mawazo kuhusu muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kwa
kuichambua Rasimu kwa makini tumeona kwamba yako mambo yaliyo muhimu na ya msingi
zaidi kimaadili na kwa maendeleo na mustakabali wa Taifa letu katika hali ya umoja
kuliko inavyoonekana kijuujuu.
Cha kuhofia ni kama katika Nchi Washirika kuna
moyo wa dhati wa umoja, hasa kwenye ngazi ya viongoi wa kisiasa, wa kuyathamini hayo
yaliyo muhimu na ya msingi zaidi na kukubali ‘tugange yajayo’. Kuwania madaraka na
umaarufu wa kisiasa, na hivyo, kuweka mkazo katika mambo ya kimuundo na kuhofia mabadiliko
ya kimsingi katika mgawanyo wa madaraka ya kiutawala kunaweza kuteka mjadala na mchakato
mzima. Hivyo, tusipokuwa makini, tunaweza kuingizwa au kujikuta tumesukumizwa kwenye
bwawa la tope la malumbano na hoja zisizo na tija wala maslahi halisi kwa umma wa
Wananchi pande zote mbili za Muungano. Je, CPT na Mama Kanisa Katoloki chini ya
TEC kwa ujumla wetu tuko tayari kusimama, kuungana na wengine wenye mapenzi mema na
kutetea yote yaliyo bora, kushauri namna ya kushughulikia yanayotia hofu kwa njia
adili na kuhadharisha umma, kukemea na kuonya, panapolazimu, kiadilifu? Wanaotaka
kujenga nguvu ya hoja na sio hoja ya nguvu, tuwasikilize na tujadiliane pamoja kihoja.
Wale watakaoendekeza hoja ya nguvu, ya kulazimisha kimabavu, tuwakemee na
kuwaonya ipasavyo kihoja vivile na kwa unyenyekevu wa moyo. Nyakati hizi ni za demokrasia,
uwazi, kujenga mshikamano kwa ridhaa ya wenye mamlaka na Wananchi katika Nchi Washirika
zote mbili kwa busara, hekima, unyenyekevu na ustahimilivu wa moyo mpana. Kwa
vyovyote vile na kama alivyoasa Mwadhama Policarp Kardinali Pengo kwenye mkutano wa
Hija wa WAWATA majuzi, yatupasa tusali na kuomba Mungu atuepushe na janga linaloweza
kutokea kutokana na kutengana kwa shari na chuki kwa kinachoitwa “kero za Muungano
za muda mrefu”.
Tusisahau tahadhari na maonyo ya Hayati Baba wa Taifa, Julius
K. Nyerere anayebezwa na kudhihakiwa na maadui wa umoja wa Jamhuri ya Muungano kwa
maneno makali na mengi ya uzushi na ya kashfa. Aliyosema ni ya kinabii: dhambi ya
kubaguana kwa misingi ya Utanganyika na/au Uzanzibari inaweza kuzaa balaa la wananchi
na uongozi baguzi kubaguana ndani kwa ndani ya Nchi Washirika au Nchi Mshirika itakayoitenda
dhambi hiyo kwa hasara na madhara kwa wote, Wananchi na Nchi Washirika. Hivyo, hata
kama mtenda dhambi hiyo ni mojawapo ya hizo Nchi Washirika, madhara yake yataathiri
vibaya Nchi Washirika zote mbili kutokana na jinsi zilivyo kijamii!