Maadhimisho ya Jumatano ya Majivu: Rarueni mioyo na si mavazi..
Jumatano kwa ajili ya Maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, mwanzo wa kipindi cha siku
arobaini za Kwaresima , Baba Mtakatifu Francisko , aliongoza Ibada ya Majivu na Misa
, katika Kanisa la Mtakatifu Sabina la Aventino la hapa Roma. Katika mahubiri
yake , Papa alitoa mwaliko wa kumrudia Mungu, kwa sababu leo hii ndani ya jamii na
Kanisa, mambo hayaendi sawa. Papa alionya, tunahitajika kutubu na kuongoka, maana
tunaishi katika dunia bandia zaidi na zaidi. Bila kutambua hilo, tunamtenga Mungu
kutoka upeo wa macho yetu. Kwaresima hivyo, unakuwa ni wakati wa kuamka na kutoka
katika hali hiyo ya kuwa waovu siku hadi siku, na kuanza kuwa watu wema . Papa kabla
ya Ibada ya Misa aliongoza Maandamano ya toba, kutoka Kanisa la Mtakatifu Anselm
la Aventine. ahubiri ya Papa yalizungumzia zaidi mambo matatu Mkristu anayotakiwa
kuyafanya wakati huu wa kwaresima kuwa ni sala, kufunga na kutoa sadaka. " Rarueni
mioyo yenu na wala si mavazi yenu " ( Joel 2:13). Kwa maneno hayo ya nabii Joel
,yaliyokuwa utangulizi wa liturujia , Papa alisema, yanaonyesha tabia ya uongofu
wa moyo, wakati huu wa neema. Ni wito wa kinabii unatoa changamoto kwetu sote , bila
ubaguzi, wenye kutukumbusha kuwa uongofu wa kweli si mabadiliko tu ya kuonekana kwa
nje au kuwa mtu wa kutoleweka eleweka, lakini hasa ni kuwa na mageuzi ya moja kwa
moja na kamili, kidhamiri na katika kutenda. Na hivyo Nabii Joel anatoa mwaliko kwetu
sote wakati huu, tunapoianza safari ndefu na ngumu , ni wakati wa kufungua macho yetu
na masikio, lakini hasa moyo , kuzamisha zaidi mtima ndani ya Neno la Mungu. papa
aliendelea kufafanua maana ya kujifunua kwa Mungu na kwa wengine akisema, wakati huu
tunapoishi katika dunia inayozidi kuwa ya bandia, katika utamaduni wa kutenda bila
ya kujali uwepo wa Mungu, Utamaduni unaopenda kumtenga Mungu kutoka upeo wa macho
yetu, Kwaresima, inatoa wito kwetu sote, kustuka na kuamka , kukumbuka kwamba sisi
ni viumbe tu, tulioumbwa na Mungu. Papa alieleza na kuonya dhidi ya kujifungia
wengine nje, pia hatari za kuyasahau matatizo na mateso ya watu wengine , kuwa ni
changamoto kwetu , wakati wa kuanza safari yetu ya kubadilika katika kipindi hiki.
Kipindi hiki kina ratiba kutembea pamoja na msalaba na sadaka. Na kwamba, Injili
ya ( Mt 6,1-6.16-18 ) inaonyesha vipengere muhimu katika safari hii ya kiroho kuwa
ni sala, mafungo na sadaka. Vyote vitatu, havina haja ya kujionyesha kwa nje , wala
kuonekana kwake kwa nje kutoa maana au thamani ya maisha kutegemea na wengine wanasema
nini , au juu ya mafanikio lakini hasa ni jinsi gani tulivyo kwa ndani. Papa aliyataja
maombi kuwa ni nguvu ya Kikristo na kwa kila mtu anaye amini. Katika unyonge na udhaifu
wa maisha yetu , tunaweza kumgeukia Mungu na kuwa na ujasiri kuwa wana wa Mungu
na kuingia katika ushirika pamoja naye. Katika uso wa majeraha mengi yanayotuumiza
na kuufanya moyo kuwa mgumu , tunahimizwa kupiga mbizi katika bahari ya maombi ambayo
ni bahari ya upendo wa Mungu, ulio mkubwa kupita kiasi, kufurahia huruma yake. Kwaresima
ni wakati wa sala, sala na ibada iliyo makini zaidi ambamo unakuwa ni wakati wa kuwa
wakarimu zaidi kwa watu wahitaji waliopungukiwa , ni wakati wa kuwaombea mbele ya
Mungu, wanao ishi katika hali nyingi ya umaskini na mateso.