2014-03-05 10:33:49

Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2014 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2014 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania unaoongozwa na kauli mbiu "Ukweli utawaweka huru. Yn. 8:32". Maaskofu wanazungumzia kuhusu umuhimu wa wongofu wa kweli unaomweka mwamini huru; wajibu wa kuuishi, kuulinda na kuusimamia ukweli kishuhuda mintarafu hali halisi ya Tanzania.

UTANGULIZI

Wapendwa Taifa la Mungu,


“Ukweli utawaweka huru”. Safari ya maisha ya mwanadamu ni safari ya kutafuta uhuru, uhuru ambao unamfungua mtu kutoka katika minyororo inayomfunga na kumfanya kuwa mhudumu wa mazingira na hali yake. Chimbuko la uhuru wa kweli ni Mungu mwenyewe katika mpango wake wa milele na huruma yake ya milele. Mungu ndiye asili na chanzo cha uhuru wa kweli na tunafanywa kuwa huru kweli pale tunapoamua kwa dhati kuupokea ukweli utokao kwa Mungu. Mungu ndiye ukweli wenyewe: “Ukweli wowote, bila kujali anayeusema, unatoka kwa Roho Mtakatifu”, na popote tunapoukuta ukweli huo ni mali ya Mungu.


Wapendwa Taifa la Mungu, tunapoanza safari ya Kwaresima ya mwaka huu, sisi Maaskofu wenu, tungependa kuwakumbusheni ninyi na watu wote wenye mapenzi mema juu ya umuhimu wa kuishi katika ukweli. Kuuishi ukweli na kuishi maisha yaliyojengwa juu ya msingi wa ukweli ni kushiriki hasa maisha ya Mungu. Kama tunataka kujenga jamii yenye utu, haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli, ni lazima tuanze kwanza kujenga dhamiri zinazothamini na kuuenzi ukweli. Pasipo ukweli jamii itasambaratika kwa sababu itakuwa imejengwa bila msingi.


Wapendwa Taifa la Mungu, Ukweli utawapeni uhuru kwa kuwa toka kuumbwa kwa ulimwengu, Mungu aliye ukweli wenyewe alipanga na kunuia kwamba mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, aishi katika uhuru kamili akimiliki na kuutiisha ulimwengu wote (Mwa 1:28 ). Ni katika ukweli tunamjua, tunampenda na kumtumikia Mungu. Ni katika ukweli tunadhihirisha kuwa tumeitwa kuwa wana huru katika ufalme wa Baba wa milele.


Ukweli na uhuru ni dhana zinazoenda pamoja. Penye ukweli pana uhuru na penye uhuru pana ukweli. Kama vile mtu huru awezavyo kuuishi ukweli kwa kuwa uhuru wake humfanya ajitegemee kifikra, kimaamuzi na kiutendaji ndivyo pia jamii ya watu na hata taifa huru liwezavyo kujitegemea kifikra, kimaamuzi na kiutendaji.


Kwa maisha, kifo na ufufuko wa Kristo, waamini wamewekwa huru na wanaitwa kuutafuta na kuusimamia ukweli. Waamini wanaalikwa kuutafuta, kuujua na kuulinda ukweli katika nyanja zote za maisha.


SURA YA KWANZA
WONGOFU WA KWELI HUTUWEKA HURU


Mungu alipenda kujifunua kwa wanadamu kupitia manabii na mwanawe wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Hata leo, Roho Mtakatifu analiongoza Kanisa katika kuendelea kuujua ukweli wa kiimani katika safari ya pamoja ya kiroho kuelekea uhuru kamili wa roho zetu. Ukweli wa kiimani huleta uhuru wa kiroho. Mwaka uliopita Kanisa liliadhimisha Mwaka wa Imani ikiwa ni sehemu ya kuwakumbusha wanakanisa wote juu ya wajibu wao wa kiimani katika Kanisa na katika jamii.

Kwa kuishi ipasavyo imani yetu ya kikristo tunashiriki wajibu wa kuujenga Ufalme wa Mungu ambao mojawapo ya nguzo zake saba za msingi ni ukweli! Hakika, ufalme wa Mungu, kama Mama Kanisa anavyotangaza katika utangulizi wa Misa ya sherehe ya Kristo Mfalme ni ufalme wa UZIMA na KWELI, ufalme wa NEEMA na UTAKATIFU, ufalme wa HAKI, MAPENDO na AMANI. Mungu wetu ni UKWELI na ni MKWELI. Tunasadiki na kukiri kwamba hadaganyi wala hadanganyiki. Imani ni wajibu wa kushiriki kuujenga Ufalme wa Mungu, ufalme ambao msingi wake ni ukweli, kwa sababu Mungu ni ukweli.

Mwanadamu aliyekombolewa kwa damu ya thamani kubwa sana ya Kristo iliyomwagika pale Kalvari, amepata kurudishiwa hadhi ya kuwa mwana huru wa Mungu akikombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Uhuru anaoupata mwanadamu una gharama kubwa na thamani kubwa. Uhuru wa kweli ni uhuru ndani ya Mungu; ni uhuru katika Mungu. Uhuru wa kweli huambatana na utii wa sheria ya Mungu na uwajibikaji unaodai unyenyekevu na nidhamu ya hali ya juu. Uhuru huu ni kinyume na uhuru usio na mipaka ambao jamii ya sasa inadai,uhuru ambao hupingana na malengo ya Muumba na taratibu na miongozo halali mbele za Mungu iliyowekwa na jamii.
Kanisa, ukweli na uhuru

Kanisa ambalo ni ishara ya wokovu na alama ya uwepo hai wa Kristo aliye njia, ukweli na uzima katika ulimwengu wa sasa ni sisi tulioalikwa kuwa Familia ya Mungu. Kwa kumkiri Kristo na kwa kubatizwa kwetu tumekuwa Rafiki na wadau wake Yesu Kristo (Yn 15: 14). Kwa namna hiyo sisi sote Familia ya Mungu – Wakleri, Watawa na Waumini Walei – tu chombo mikononi mwa Kristo kwa kushiriki kikamilifu kazi ya Kristo ya kuwakomboa watu.

Kwa mantiki hiyo, Kanisa linao wajibu wa kwanza kabisa kuulinda ukweli, kuusimamia, kuushi na kuutangaza. Kanisa ni chombo kiletacho wokovu kwa ulimwengu na kuwaweka huru wanadamu walio katika utumwa unaojidhihirisha katika sura mbalimbali kama vile, umasikini, ufisadi, rushwa, ushirikina, magonjwa, siasa chafu, kutokuwajibika, ubinafsi,nk.

Kanisa ni chombo cha Kristo cha kuwaletea watu uhuru wa kweli. Roho wa Bwana, aliye juu ya Yesu (Lk 4:18,19) yuko pia juu ya Kanisa lake ambalo analituma kuwafungulia watu vifungo vyao mbalimbali na kuwaachia huru waliosetwa (Lk 4:18-19).

Ukweli kama tunu ya kimungu lazima uote mizizi katika mioyo ya wanadamu walioumbwa kwa sura na mfano wake (Kut 1:26). Ni wajibu wa kila mwanadamu kuutafuta ukweli na kuujua. Kwa njia ya ufahamu, mwanadamu anaalikwa kuutafuta ukweli kwani ndio njia pekee ya kumweka huru na kuufikia wokovu. Maana Mungu amemwachia mwanadamu uhuru kusudi aifuate nia yake (YBS 14:15), na hivyo amtafute Muumba wake kwa hiari, na hatimaye aufikie ukamilifu ulio bora na wenye heri, pasipo shuruti na kwa kuambatana na Mungu. Kanisa linamsaidia mwandamu kufanikisha kuufikia ukweli na kwa uhuru kupitia neema za Mungu.



SURA YA PILI
WAJIBU WA KUUISHI, KUULINDA NA KUUSIMAMIA UKWELI KISHUHUDA

Waamini waliowekwa huru na Kristo, wanao wajibu wa kuujua ukweli, kuutafuta, kuulinda na kuusimamia kwa lengo la kuleta huru wa kweli kwa manufaa ya wote. Huko ndiko kuwa mfuasi wa Kristo aliyesema: “Mimi nilikuja ulimwenguni; ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu” (Yn 18:38).

Jamii leo hii imegawanyika juu ya uhuru ambao wanajamii wanapaswa kuwa nao. Wazazi wanaamini kuwa uhuru ni kutenda jambo lolote bila kubughudhiwa na yeyote, hata kama tendo hilo ni kinyume na misingi ya maadili. Watoto wanataka uhuru binafsi katika kupanga na kuamua mambo yanayowahusu. Watoto wasingependa kupokea malezi na maelekezo iwe ni ya wazazi au ya jamii. Vijana wanapenda kuamua mambo yao kama wanavyoona, wakipuuzia uzoefu na ushauri wa wakubwa wao. Tujiulize: Je, huu ndiyo uhuru tuutafutao? Katika mazingira kama haya kinachotafutwa si uhuru bali kuishi kwa kuheshimu vionjo binafsi. Ni muhimu sana kwa wanafamilia kuwa na uhuru wa pamoja katika kupanga na kuamua masuala kifamilia.

Tukijiruhusu kama wanajamii kuishi katika uholela upendo unatoweka. “Usikubali kitu chochote kuwa ni ukweli kama kinakosa upendo. Na usikubali kitu chochote kuwa ni upendo kama kinakosa ukweli! Hali moja bila nyingine ni uongo unaoharibu”. Kwa sababu “ni katika ukweli tu ndipo upendo inang’aa, ni katika ukweli tu ndipo tunapoweza kuuishi upendo kwa hakika”.
SURA YA TATU
HALI HALISI YA TAIFA LETU


Taifa lenye umri wa miaka 50 ya uhuru ni taifa lililokwishavuka uchanga. Ni taifa kijana lililo katika umri wa kujenga juu ya misingi iliyowekwa kwa manufaa ya wote. Ni taifa linalojitegemea. Bila msingi huo, mengine yote, hata kama yanaonekana yanang’aa yatakuwa yanasaliti mustakabali wa kweli wa taifa letu. Tusijidanganye. Bila msingi wa kujitegemea na kutafuta manufaa ya wote (common good) taifa hili litaanguka. Kama halianguki leo, kesho ni lazima litaanguka. Tunajiuliza, uko wapi ujasiri wa Taifa letu? Imepotelea wapi fahari ya kujitawala, si kisiasa tu, bali kiuchumi, kifikira na kijamii? Imepotelea wapi ile mbegu ya uzalendo iliyopandwa na waasisi wa taifa letu? Imeishia wapi heshima ya kuthamini utu, kuheshimu imani ya asiyeamini kile nisichokiamini na kutafuta ufumbuzi halisi wa matatizo yanayotukabili?


Tumepoteza dira ya kujitegemea kimaamuzi na kimkakati. Tumefikia mahali pa kuamini kwamba maendeleo yataletwa kwa kaulimbiu zinazobadilika badilika kila siku. Katika mazingira ya sasa, watu wachache, kwa sababu binafsi na kwa manufaa binafsi wanapotosha ukweli na kutafuta njia za kulinda maslahi yao kwa kutumia mifumo isiyokubalika, lakini inayosimikwa na kuhalalishwa ili kulinda maslahi binafsi. Hali hii inajidhihirisha kupitia matumizi mabaya ya madaraka, mikataba mibovu, kupindisha sheria, kufumbia macho uhalifu, nk. Uhuru wa kweli haujengeki katika misingi dhaifu ya ubinafsi na haulengi kumfanya mtu yeyote yule awe juu ya sheria za haki na taratibu za uadilifu. Na kimsingi, hakuna maendeleo ya kweli kama watu hawaheshimu haki ya msingi ya kuujua ukweli na kuishi kadiri ya ukweli huo.

Katika mazingira kama haya Kanisa haliwezi kukaa pembeni na kutazama tu kwa sababu nalo lina wajibu wa kuijenga jamii. Kanisa lina wajibu wa kuangalia, kuboresha na kuikosoa mienendo ya kijamii na kisiasa inayohatarisha ustawi wa jamii nzima na hivyo kuathiri kazi ya Kristo ya kumkomboa mwanadamu na kuusimika Ufalme wa Mungu; ufalme unaojidhihirisha katika kutamalaki kwa ukweli, haki na amani. Kanisa litaendelea kusisitiza ukweli huu kwamba; “Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote”. Hapa tungependa kuelezea mambo machache yanayoivuruga nchi yetu.
Uvunjifu wa amani

Taifa letu linazidi kupoteza tunu bora ya amani ambayo waasisi wa taifa letu wametuachia. Katika siku za karibuni yamekuwepo matukio ya mauaji, watu kumwagiwa tindikali kwa sababu ya imani yao au visasi na hata mauaji kwa kutumia mabomu. Uhasama wa kidini na matukio ya kijasusi na ugaidi dhidi ya raia yanaonekana kushamiri. Kumekuwapo na matumizi makubwa ya nguvu upande wa vyombo vya dola vikitumia silaha za moto na za kivita. Wimbi la wananchi kutotii sheria na taratibu za nchi linakua. Tunakwenda wapi?

Amani lazima ilindwe ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. Hata hivyo, amani sio tunu inayojitegemea peke yake kwa kuwa amani ya kweli inazaliwa ndani ya mioyo yenye kujali misingi ya utu, haki, heshima, ukweli na umoja. Fikra tofauti na hizo, huzaa mioyo potofu, na mioyo potofu haiwezi kutoa amani.
Rushwa na madawa ya kulevya

Mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya yamegeuka kuwa wimbo unaochosha kwa sababu hakuna dhamira ya dhati ya kuitokomeza. Uongozi wa juu unapotamka hadharani kuwafahamu watoa rushwa, wapokea rushwa na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa ni hali inayotisha sana. Wakati umefika ambapo lazima tuwe wakweli kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Hatuwezi kuwa huru kuhusu rushwa na madawa ya kulevya kama hatujawa wakweli kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Wanaopiga vita rushwa majukwaani, ndio wanaoomba na kupokea nje ya jukwaa. Isitoshe rushwa ndiyo ngazi waliyoitumia na wanayoitumia kufika jukwaani. Katika mazingira kama haya hatujengi Taifa bali tunalibomoa na historia itatuhukumu. Hatuna budi kuunda misingi imara ya utawala bora. Tukumbuke daima kuwa utawala bora bila uwajibikaji na kuwajibishana ni kiini macho.
Kukua kwa matabaka katika jamii

Tofauti kubwa sana za kiuchumi zinazidi kupanua utengano wa kimatabaka kati ya wenye nguvu za kiuchumi na wasio na kitu. Wenye nguvu kiuchumi sasa wanamiliki uchumi, wanamiliki siasa na hatima ya fukara, na kwa fedha wananunua haki ya wanyonge.


Mgawanyo mbovu wa rasilimali za nchi unatisha. Ardhi inamilikiwa na wachache kwa kivuli cha uwekezaji mkubwa huku wananchi wakiahidiwa ajira kwa kuwa vibarua kwenye mashamba hayo badala ya kuwezeshwa kumiliki ardhi na kuitumia kwa faida. Haya ni masuala yanayomtia hofu mtu yeyote anayejali na kuthamini mustakabali wa taifa letu.
Siasa kuingilia weledi

Tatizo la siasa kutawala mifumo ya ujenzi wa misingi ya maendeleo linakua kwa kiwango cha kutia hofu. Kwa mfano, siasa na wanasiasa wanaathiri mfumo wa utoaji wa elimu nchini kiasi cha kulifanya taifa hili kuwa kama taifa lisilojali mustakabali wake. Yamekuwepo maneno mengi na mipango ya zimamoto isiyofanyiwa utafiti wa kina na utendaji umekuwa hafifu sana. Uthabiti katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo hauonekani na badala yake porojo zimetawala. Imejitokeza hali ya wale waliopewa dhamana ya kusimamia masuala ya elimu kwa mfano kukosa unyenyekevu wa kuwasikiliza na kushauriana na wataalamu katika nyanja hizi. Kila mara zinaibuka sera ambazo msingi wake ni ubunifu usiozingatia weledi na hivi kuifanya elimu kudidimia.
Mchakato wa Katiba mpya

Katiba kama moyo wa taifa ni chombo kinachopaswa kutengeneza misingi ya mfumo wa maisha mazima na uhai wa Taifa letu. Ukweli wote na uhuru wote wa Taifa unabebwa na Katiba. Iwapo mchakato wa katiba mpya hautaendeshwa kwa ukweli na uhuru, hatutaweza kupata katiba yenye kubeba ukweli na uhuru wote kuhusu taifa letu. Tunarudia tena kutamka kuwa zoezi hili adhimu na la muhimu kwa mustakabali wa Taifa limeharakishwa mno. Sasa tunaona zoezi zima limehodhiwa na wanasiasa. Mchakato wa katiba mpya unadai kuwepo kwa fadhila ya kijamii ya kutafuta manufaa ya wote (common good). Katiba si mali ya wanasiasa bali ni mali ya wananchi. Tunapenda kuialika jamii yote kuitendea haki nchi yetu. Tukae chini na tuzipime kila hatua zetu katika zoezi hili na tuone kama zinakidhi kipimo cha «Hekima, Umoja na Amani». Hekima ituongoze kulinda umoja wa Taifa letu na utuepushe na kishawishi cha kubaguana na kutengana. Kwa kuzingatia hilo umoja huo utatuongoza katika njia ya amani.

Uharibifu wa mazingira

Tishio kubwa la kimaangamizi kwa vizazi vijavyo linatokana na ukweli kuwa kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira. Maendeleo yanagharama yake. Kiu ya kweli ya maendeleo ni lazima iambatane na ulazima wa kuwa makini katika kutunza mazingira na uthabiti wa uumbaji. Vyanzo vya maji na kingo za mito zimeharibiwa kwa kuruhusu shughuli za kilimo kufanyikia maeneo hayo, kwa kuruhusu makazi ya watu, viwanda kujengwa na kuruhusu takataka ya sumu kutoka viwandani na migodini kutiririkia kwenye vyanzo vya maji, nk. Ukataji wa miti umeshamiri na baadhi ya misitu ya asili imepotea. Kwa sababu hiyo tumechangia sana katika kusababisha mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake sasa zinajionesha waziwazi. Ukame, njaa, mafarakano kati ya wakulima na wafugaji na kuenea kwa jangwa ni vitisho vilivyo dhahiri mbele yetu. Huu ni ukweli kuwa tumeshindwa kuzingatia agizo la Mungu la kuitawala na dunia kuutiisha ulimwengu. Tunahitaji sasa kubadilika ili ukweli utawale, tupate uhuru kamili kwa kuwajibika kuyalinda na kuyatunza mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Ni wajibu wetu Waamini Wakatoliki kuulinda ukweli na kuusimamia kiushuhuda. Jitahada za namna hii zina gharama yake kwa kuwa zinahitaji ujasiri wa kinabii na utayari wa kuteseka na hata ikibidi kutoa sadaka kubwa ya uhai.
HITIMISHO

Wapendwa Taifa la Mungu, tunapenda kuwahimiza kwa maneno haya tukisema: “Inunue kweli, wala usiiuze. Naam, hekima na mafundisho na ufahamu” (Mith 23:23). Ukweli ni msingi wa lazima na unapaswa kuwa wa kudumu kwa tendo lolote ili liweze kuitwa kuwa ni adilifu. Ukweli unapaswa kuzijenga dhamiri zetu ili kumsaidia mwanadamu kupata mwanga unaofukuza mikanganyiko.


Katika ulimwengu usiojali ukweli, uhuru unapoteza msingi wake na mwanadamu anakuwa mhanga wa vurugu ya vionjo na kutawaliwa kwa hila, iliyojidhihirisha waziwazi au iliyojificha. Hivi ni mwaliko kwetu sote “tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo” (Efe 4:15). Kwa sababu upendo “haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli” (1Kor 13:6).










Ni sisi Maaskofu wenu,

Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Iringa
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam
Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu, Arusha
Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora
Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap, Mwanza,
Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro
Mhashamu Askofu Gabriel Mmole, Mtwara

Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar
Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga

Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba
Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba
Mhashamu Askofu Damian Dallu, Geita
Mhashamu Askofu Ludovick Minde, OSS, Kahama
Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe

Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi
Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Mbulu
Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma
Mhashamu Askofu Issack Amani, Moshi
Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga
Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Same
Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam
Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda
Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Dodoma
Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa
Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga
Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.