2014-03-05 10:00:30

Kwaresima ni kipindi cha mshikamano wa kidugu!


Kipindi cha Kwaresima ni fursa ya kuonesha mshikamano wa dhati na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kwa njia ya tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma; kwa kusali na kufunga . Kuna zaidi ya watoto 250, 000 wanaosumbuliwa na utapiamlo wa kutisha nchini Ufilippini. RealAudioMP3

Watoto hawa wanaweza kuokolewa kwa njia ya mshikamano wa upendo wakati wa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2014, kwa waamini kufunga na kujinyima kwa ajili ya kuwasaidia watoto hawa. Hii ndiyo Kampeni ya Kwaresima kwa mwaka huu inayotolewa na Kardinali Luis Antonio Tagle wa Jimbo kuu la Manila, nchini Ufilippini kwa siku ya Jumatano ya majivu, ambao kadiri ya Mapokeo ya Mama Kanisa, waamini wanatakiwa kufunga na kile ambacho wanajinyima kwa siku hii, kinatolewa sadaka kama kielelezo cha mshikamano wa upendo na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Jimbo kuu la Manila linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Jumatano ya majivu, kuhakikisha kwamba, wanajinyima, ili kuchangia fedha ya kununua chakula kwa ajili ya watoto 250, 000. Kardinali Luis Antonio Tagle anasema, yeye anapenda kuwa mstari wa mbele ili kuonesha mfano unaopaswa kuigwa na waamini wakati wa Kipindi cha Kwaresima.

Watoto 50, 000 watakaofaidika kutokana na mshikamano wa upendo na ukarimu kwa waamini ni wale wanaotoka katika maeneo ambayo hivi karibuni yaliathirika vibaya kutokana na maafa asilia. Watoto wanaoshughulikiwa kwa sasa ni wale wenye umri kati ya miezi sita hadi miaka kumi na miwili. Watoto hawa watakuwa wanapewa msaada wa chakula kwa kipindi cha miezi sita.

Wazazi na walezi wataelimishwa jinsi ya kuwalisha watoto wao pamoja na kuwajengea uwezo wa kiuchumi ili baadaye waweze kuanza kujitegemea wenyewe. Taasisi ya Pondo ng Pinoy ya Jimbo kuu la Manila tangu mwaka 2004 imetenga rasilimali fedha na watu ili kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Takwimu zinaonesha kwamba katika kipindi cha Mwaka 2012 hadi mwaka 2013 Taasisi hii ilikusanya kiasi cha Euro 280, 000. Hiki ni kielelezo cha ukarimu na upendo kutoka kwa wananchi wa Ufillippini.








All the contents on this site are copyrighted ©.