Waziri wa ulinzi Filipe Nyusi kupeperusha bendera ya FRELIMO wakati wa uchaguzi mkuu
nchini Msumbiji
Chama cha Tawala cha FRELIMO nchini Msumbiji kimemteua Bwana Filipe Nyussi, Waziri
wa Ulinzi kupeperusha bendera ya chama hiki wakati wa kinyang'anyiro cha uchaguzi
mkuu nchini Msumbiji, unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2014. Kama mambo yote yakienda
sawa, basi Bwana Filipe Nyussi anatarajiwa kurithi kigoda cha Rais Armando Emilio
Guebuza.
Uamuzi huu umetolewa na Kamati kuu ya Chama cha FRELIMO katika kikao
chake kilichohitimishwa hivi karibuni. Katika kinyang'anyiro hiki, Bwana Filipe Nyussi
alikuwa anachuana na Waziri mkuu mstaafu Luisa Diogo ambaye kadiri ya duru za kisiasa
zinaonesha kwamba, alikuwa anaungwa mkono na kambi ya Rais mstaafu Joakim Chisano
wa Msumbiji.
Chama cha FRELIMO kimekuwa kikishinda uchaguzi mkuu tangu mwaka
1992. Bwana Filipe Nyussi anatarajiwa kupambana na nguri za upinzani: Alfonso Dhlakama
kutoka Chama RENAMO pamoja na Davis Simango kutoka Chama cha MDM.