Kardinali Walter Kasper ambaye hivi karibuni alipewa dhamana na Baraza la Makardinali
kuwamegea kuhusu uzuri wa ndoa na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo katika
mahojiano maalum na Gazeti la "Avvenire" linalomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki
Italia anasema kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kutambua na kuthamini wito, utume
na dhamana ya wanawake ndani ya Kanisa.
Ni matumaini ya Kardinali Kasper kwamba,
mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu Familia zitakazofanyika Mwaka
2014 na Mwaka 2015 zitatoa mwanya wa kuwasikiliza wanawake. Hii inatokana na ukweli
kwamba, bila mwanamke, Familia iko mashakani. Huu ni ujumbe mzito wakati huu Mama
Kanisa anapoendelea kuhimiza umuhimu wa kukuza na kuimarisha tunu msingi za maisha
ya ndoa na familia.
Kimsingi wanawake hawajasikilizwa kwa makini ndani ya
Kanisa. Umefika wakati anasema Kardinali Kasper kuwasikiliza na kuwashirikisha katika
maisha na utume wa Kanisa katika ngazi mbali mbali na hasa zaidi katika vikao vyenye
kutoa: sera, mikakati na maamuzi. Kanisa bila utume na ushiriki mkamilifu wa wanawake,
linaweza kukosa dira na mwelekeo sahihi.
Sifa na wasifu wa kuwashirikisha wanawake
katika maisha na utume wa Kanisa, ziwe ni sawa kama inavyotolewa kwa wanaume; yaani:
weledi, uzoefu wa kazi, ari na moyo wa huduma kwa Kristo na Kanisa lake. Ushiriki
wa wanawake anasema Kardinali Kasper unaweza kulisaidia Kanisa kuwa na mwono mpana
zaidi katika mikakati yake ya kichungaji.
Kardinali Walter Kasper anawapongeza
wanawake wanaoendelea kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Kanisa kwa kusimama kidete na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hawa ndio
Wamissionari wanaojisadaka katika huduma za elimu, afya na maendeleo ya Jamii hata
wakati mwingine wanajikuta katika mazingira hatarishi. Kanisa linapaswa kuwatambua
na kuwatia moyo ili kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi katika maisha na utume
wa Kanisa.
Kardinali Kasper anasema, sauti ya wanawake inapaswa kusikilizwa
kwenye vikao mbali mbali vya Kanisa vinavyotoa maamuzi kuhusu sera na mikakati ya
maisha na utume wa Kanisa.