Rasilimali asilia ni kwa ajili ya mchakato wa maendeleo ya watanzani wote!
Serikali ya Tanzania imeahidi kuangalia uwezekano wa kuwafadhili wanafunzi wapatao
20 kutoka katika mikoa ya Lindi na Mtwara wanaosoma katika chuo kikuu kishiriki cha
Stella Maris Mtwara (STEMUCO) ambao hawana uwezo wa kulipa ada ya masomo yao.
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi alipokuwa
akijibu ombi lililotolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha STEMUCO Padre Dkt. Aidan Msafiri
alipokuwa akiwasilisha mada yake ya Tunu na maadili katika rasilimali za gesi, mafuta
na madini kwa amani na maendeleo ya Tanzania wakati wa siku ya pili ya kongamano la
viongozi wa dini kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara.
Katibu Mkuu Maswi alisema
kuwa serikali ipo tayari kuhakikisha kwamba, inawapatia elimu hiyo ili waweze kuhudumia
jamii ya Wanalindi na Mtwara katika kujiletea maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla.
Lengo kubwa la kongamano hili lilikuwa ni kutoa elimu zaidi kwa viongozi wa dini kuhusiana
na rasilimali za gesi asilia, mafuta na madini kwa ajili ya maendeleo ya watanzania
wote.
Elimu hiyo ililenga kuwaelimisha viongozi hao wa dini ambao wanaushawishi
mkubwa kwa waumini wanaowaongoza ambapo mada mbalimbali zilitolewa ili kuwajengea
uwezo wa kuwaelimisha waamini wao juu ya masuala ya gesi asilia, mafuta na madini.
Mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo ili kufanikisha uelewa wa pamoja
kwa viongozi wa dini ni pamoja na Mtazamo wa kitaalimungu juu ya rasilimali za gesi
asilia, mafuta na madini iliyowasilishwa na Sheikh Abubakar Zuberi, Maelezo ya jumla
ya Wizara ya Nishati na Madini kuhusu za gesi asilia, mafuta na madini iliwasilishwa
na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Eliakim Maswi, Tunu na maadili katika za gesi asilia,
mafuta na madini iliwasilishwa na Padre Dkt. Aidan Msafiri, Ushuhuda wa mwakilishi
aliyehudhuria mafunzo ushirikishaji mang’amuzi ya uchumi wa gesi nchini Thailand iliwasilishwa
na Hassan Gobbosi.
Mada nyingine ni Mipango ya matumizi ya gesi asilia katika
mikoa ya Lindi na Mtwara iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (TPDC) Yona Killagane, Uzoefu wa ushiriki wa wazawa katika masuala
ya gesi asilia iliwasilishwa na Sultan A. Sultan na Maelezo ya Wizara yaliyowasilishwa
na Mwara Shoo na Ally Samaje.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini imeridhia kuendelea kuwapeleka vijana wa mikoa hiyo kusoma VETA kwa muda wa
miaka mitatu ili waweze kutumia fursa ya kugunduliwa kwa rasilimali mbalimbali katika
mikoa hiyo. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Yona Killagane akiwasilisha
mada juu ya mipango ya matumizi ya gesi asilia Lindi na Mtwara alisema kuwa zipo faida
nyingi za mradi wa gesi kwa wananchi.
Killagane alizitaja faida hizo kuwa
ni kujenga shule za chekechea, wanafunzi wanapata udhamini wa kusomeshwa shule za
sekondari, kujengewa hospitali, kuwapatia maji safi, ajira na kupata umeme unaotokana
na gesi aktika maeneo yao. Kongamano hili la siku mbili la viongozi wa dini wa mikoa
ya Lindi na Mtwara liliandaliwa na viongozi wa dini wa mikoa hiyo ikiwa ni mwendelezo
wa Kongamano la kitaifa la viongozi hao lililofanyika mwezi Januari mwaka huu Jijijni
Dar es salaam. Makongamano haya yote mawili yaliongozwa na kauli mbiu ya “Rasilimali
zetu za gesi asilia, mafuta na madini kwa amani na maendeleo ya Tanzania.