Kampeni ya Kwaresima, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa Mwaka 2014
Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu,
ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Ndiyo
kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresma
kwa Mwaka 2014, kinachoanza rasmi kwa Jumatano ya Majivu, tarehe 5 Machi 2014 hadi
tarehe 17 Aprili 2014. Hiki ni kipindi
cha toba na wongofu wa ndani; kipindi cha kusali, kufunga na kutenda matendo ya huruma.
Ni kipindi ambacho waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kufanya tafakari ya kina
ya Neno la Mungu, ili kuweza kuimwilisha kama sehemu ya Imani tendaji! Baraza la
Maaskofu Katoliki Kenya katika Kampeni yake kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2014
linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa kina kuhusu mafao
ya wengi na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Akifafanua kuhusu Kampeni
ya Kwaresima kwa mwaka huu, Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki
na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anasema, kwamba, Juma la kwanza, waamini
wanaalikwa kutafakari na kujadiliana kuhusu matumizi bora na sahihi ya maliasili inayopatikana
nchini Kenya kwa ajili ya mafao ya wengi. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kenya
inaendelea kugundua utajiri mkubwa wa maliasili ambao unaweza kuwa ni baraka au balaa.
Ikiwa kama wananchi wa Kenya wataungana kwa dhati wanaweza kuwashinikiza viongozi
wa Serikali kuhakikisha kwamba, utajiri huu unatumika kwa ajili ya mafao ya wengi. Baba
Mtakatifu Francisko ameitisha Sinodi Maalum kwa ajili ya Maaskofu, itakayokuwa na
dhamana ya kupembua na kuchambua changamoto za kichungaji zinazojitokeza katika maisha
na utume wa familia. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, katika Juma la Pili, wanawaalika
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kuhusu. Familia na Imani. Taasisi
ya familia kwa sasa inakabiliana na changamoto nyingi katika maisha na utume wake.
Askofu mkuu Okoth wa Jimbo kuu la Kisumu, Kenya anasema, hivi karibuni wananchi
wa Kenya wameshuhudia baadhi ya wabunge wakijadili muswada wa sheria unaogusa na kutikisa
misingi ya maisha ya ndoa na familia inayosigana kimsingi na tunu, mila na tamaduni
njema za Kiafrika na Kikristo. Katika majadiliano na tafakari, waamini na watu wenye
mapenzi mema wajadili kwa kina na mapana jinsi ya kupambana na tabia hizi zinazotaka
kuhalalisha mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema zinazotaka kubomoa
na kusambaratisha familia. Wananchi wanapaswa kuungana na kushikamana kwa pamoja ili
kukabiliana na changamoto hizi katika maisha na utume wa ndoa na familia. Katika
kampeni ya Kipindi cha Kwaresima, Juma la tatu, waamini wanaalikwa kujikita zaidi
katika tafakari inayolenga kujenga na kudumisha misingi ya umoja na mshikamano wa
kitaifa pamoja na Amani, zawadi kutoka kwa Mungu lakini inamshirikisha na kumwajibisha
binadamu. Wananchi wa Kenya wanahamasishwa kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa,
kwa kung’oa uchoyo na ubinafsi; chuki na uhasama, ili kuimarisha umoja wa kitaifa.
Ikumbukwe kwamba, Amani inashamiri pale ambapo haki imepewa kipaumbele cha kwanza. Askofu
mkuu Okoth anawaalika waamini katika Juma la nne kujikita zaidi katika tafakari inayopembua
kuhusu utawala bora. Kuna kasoro nyingi zinazoendelea kujitokeza katika masuala ya
uongozi ndani ya Serikali, Vyama vya Kisiasa pamoja na Taasisi mbali mbali nchini
Kenya. Utawala bora ni kigezo msingi cha ustawi na maendeleo ya nchi. Utawala bora
unapaswa kupata chimbuko lake ndani ya familia na katika Kanisa. Lengo ni kujikosoa
ili kuimarisha nguvu ya kimaadili, ili kuweza kufuatilia masuala ya utawala bora kutoka
kwa wengine! Wananchi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika kukuza na kuimarisha
utawala bora; mada itakayojadiliwa kwa kina na mapana katika Juma la tano la Kipindi
cha Kwaresima. Jamii inashuhudia kishawishi cha watu kutaka kujitajirisha wenyewe
kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia kila fursa inayopatikana kwa ajili ya mafao binafsi.
Kanisa linawahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi, kwa
kujielekeza zaidi katika uwajibikaji, ukweli na uwazi katika matumizi ya fedha na
mali za Serikali. Kwaresima ya Mwaka 2014 anasema Askofu mkuu Zacchaeus Okoth,
Mwenyekiti wa Tume ya haki na Amaniya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, kiwe ni kipindi
kwa ajili ya kufunga na kusali ili kuiombea Kenya. Lengo ni kujenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa kitaifa, kila mwananchi akiheshimiwa na kuthaminiwa utu wake. Imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.