Ziara ya Kardinali Tauran nchini Benin inalenga kukoleza majadiliano ya kidini
Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali nchini Benin; Mafundisho
Yakinifu kuhusu Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam pamoja na waamini
wa dini za jadi ni kati ya mambo msingi yakayojadiliwa na Kardinali Jean Lous Tauran
wakati wa safari yake ya kikazi nchini Benin, kuanzia tarehe 2 Machi hadi tarehe 5
Machi 2014. Majiundo haya makini yanaratibiwa na Padre Didier Affolabi kutoka Benin..
Kardinali
Tauran anatarajiwa pia kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Benin,
ili kuwashirikisha uzoefu na mang'amuzi yake kuhusu mikakati ya majadiliano ya kidini.
Kardinali pia atakutana na kuzungumza na viongozi wa dini mbali mbali nchini Benin
pamoja na kuangalia sifa za mwamini wa dini ya asili ambaye anaheshimiwa kuwa ni "mtakatifu".
Jumatano ya Majivu, siku ya kufunga na kufanya toba, Kardinali Tauran atatembelea
Kanisa kuu la Benin, lango la watu waliokuwa wamekata tamaa kwa kusafirishwa kwenda
utumwani. Hili ni eneo linalokumbusha madhara ya biashara ya utumwa kwa utu na heshima
ya binadamu. Hapa historia inaonesha kwamba, kuna mamillioni ya watu waliosafirishwa
kwenda utumwani.
Akiwa nchini Benin, Kardinali Tauran atapata nafasi ya kuadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Gallo na baadaye atakwenda
kusali kwenye kaburi la Kardinali Bernadin Gantin, kutoka Benin, Kardinali na Mwafrika
wa kwanza kupewa dhamana ya kuongoza Baraza la Kipapa la haki na amani, kunako mwaka
1976 na baadaye alikuwa ni Dekano wa Makardinali.
Itakumbukwa kwamba, hata
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipotembelea Benin ili kuzindua Waraka wa Dhamana
ya Afrika, Africae Munus alitembelea na kusali kwenye kaburi la Kardinali Bernadin
Gantin, ambaye walifanya naye utume kwa miaka mingi mjini Vatican.