2014-03-01 07:54:57

Vijana wapokelewe, wasikilizwe na waalikwe kumfuasa Yesu!


Changamoto zilizojitokeza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 ni kati ya tema zilizofanyiwa kazi na Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini katika mkutano wake wa Mwaka uliokuwa unafanyika mjini Vatican. Lengo lilikuwa ni kuweka mikakati ya shughuli za kichungaji ili kuwajengea vijana uwezo wa maisha kwa njia ya elimu makini. Mikakati ya elimu ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, kama sehemu ya mchakato wa kurithisha imani.

Mama Kanisa anatekeleza yote haya kwa lengo ya kutaka kumuiga Kristo aliyetoa kipaumbele cha pekee kwa vijana katika maisha na utume wake. Vijana wanahamasishwa kumfuasa Kristo, kwa kujitosa bila ya kujibakiza katika maisha na huduma; katika upendo sanjari na kusimamia misingi ya ukweli na haki. Kanisa lina amini kwamba, mwalimu makini wa vijana ni Yesu Kristo, mwaliko kwa vijana kuachana na ubinafsi, kwa kujitahidi kutekeleza mapenzi ya Kristo kwa kumfahamu vyema zaidi. Mfano wa maisha yao, uelenge kuwajengea uwezo wa kuwa kweli ni wafuasi amini na wamissionari ambao wako tayari kutoka kifua mbele kuwatangazia vijana wenzao Injili ya Furaha.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 28 Februari 2014, wakati alipokutana na kuzungumza na Wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini waliokuwa wanafanya mkutano wao wa Mwaka mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Yesu alipokutana na yule kijana tajiri alimwonjesha mambo makuu matatu: ukarimu, usikivu na mwaliko.

Yesu alipomwona yule kijana alimpenda na kumwonjesha upendo usikuwa na mipaka. Hivi ndivyo Yesu anavyoendelea kufanya katika kila maisha ya mwamini, anapenda kuwa karibu na vijana wanapokuwa kazini, shuleni au katika familia, kwa kuwa makini kusikiliza mahitaji yao msingi, matumaini bila kusahau mahangaiko yao ya ndani.

Vijana wengi anasema Baba Mtakatifu Francisko wanakumbukana na matatizo makubwa pamoja na changamoto za maisha ya ujana. Baadhi yao wanapata shida katika masuala ya elimu, hawana fursa za ajira, wanaoishi na wazazi ambao wametengana. Zote hizi ni nyakati ambazo zinawafanya baadhi ya vijana kuchanganyikiwa na hatimaye kupoteza dira na mwelekeo wa maisha na hatimaye kujikuta ni "mateja wa matumizi haramu ya dawa za kulevya", ukahaba na matumizi ya nguvu.

Kanisa limepewa changamoto ya kuhakikisha kwamba, linawasaidia vijana hawa katika hija ya maisha yao ya kiroho na kiutu. Waheshimiwe, waeleweke na kupendwa kutokana na utu wao kama binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu alipata fursa ya kuzungumza na yule kijana tajiri, akamsikiliza kwa makini yale aliyokuwa anazungumza mintarafu mwanga wa Maandiko Matakatifu. Yesu anaonesha mfano wa kuigwa na Kanisa kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linawajengea vijana uwezo wa kujisikia kwamba wako nyumbani wanapokuwa Kanisani.

Vijana wafunguliwe milango ya Kanisa na viongozi wa Kanisa wawe mstari wa mbele kwenda kuwatafuta vijana huko waliko, kwenye "vijiwe vyao", Vijana wasikilizwe kwa makini kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Mama na kwamba, hawezi kamwe kuwapatia kisogo, lazima asikilize mahangaiko yao ya ndani ili kuweza kuyaweka mbele ya Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, vijana wanapaswa kusikiliza kutoka kwa viongozi wa Kanisa kuhusu maneno ya Yesu aliyomwambia yule kijana, nenda ukauze vyote kisha njoo unifuate, wakitambua kwamba, Yesu yu hai na anataka kuwashirikisha katika maisha na utume wake. Vijana wajengewe uwezo mkubwa wa kumfahamu Yesu na Injili yake, ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha kwa kuwa makini na watu wenye malengo makubwa katika maisha.

Vijana wanataka kuona mabadiliko katika maisha kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko haya; wanataka kujenga Jamii bora ambamo: rushwa na ufisadi vitakomeshwa na watu watajikita katika upendo na mshikamano wa dhati. Kanisa Amerika ya Kusini inafumbata hazina kubwa kwa maisha na utume miongoni mwa vijana kiasi cha kuweza kuthubu kuchangia mchakato wa maendeleo endelevu miongoni mwa vijana, ili hatimaye, kujenga Familia kubwa inajikita katika upendo na upatanisho wa kweli.

Kwa njia hii, Yesu atapata nafasi ya kuweza kukutana na kuzungumza na vijana kwa kuwapatia nguvu na ujasiri wa kuweza kukabiliana na changamoto za maisha. Vijana wasaidiwe kujenga urafiki na Yesu, ili waweze kuwa ni mahujaji wa imani wanayowamegea jirani zao katika medani mbali mbali za maisha. Vijana hawa wasikie kwamba, wanapokelewa na kusaidiwa na Mama Kanisa ili kuvuka wasi wasi na mashaka ya maisha, ili hatimaye, vijana waweze kupata tena "tabasamu la kukata na shoka".

Baba Mtakatifu anawaambia wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini kwamba, vijana wanawasubiri kwa hamu na moyo mkuu, wapokee changamoto hizi na kuzifanyia kazi. Kanisa Amerika ya Kusini, lijifunze kwa bidii kuwasindikiza, kuwafundisha na kuwalea vijana. Kanisa liendelee kuwajengea vijana uwezo kwa njia ya elimu pamoja na kuwainjilisha, ili siku moja waweze kuwa kweli ni Mitume na Wamissionari, dhamana inayohitaji udumifu na fadhila ya unyenyekevu. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba ambayo amewakabidhi wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na kuwaomba kuwafikishia vijana salam na matashi mema.









All the contents on this site are copyrighted ©.